24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MAGONJWA YA KITROPIKI YANAYOPUUZWA, KUATHIRI WENGI

picha

Na JOACHIM MABULA,


 

TROPIKI ni ukanda wa dunia uliopo pande zote mbili za ikweta kati ya latitudo za 23.5° za kaskazini na za kusini. Nchi zilizo kwenye ukanda wa tropiki ni pamoja na nchi za Afrika Mashariki, Afrika ya kati, Afrika Magharibi, Karibiani na India. Shirika la Afya Duniani (WHO) limeanzisha kampeni ya kutoa uelewa kuhusu maradhi 17 yanayoathiri ukanda wa tropiki ambayo yanaathiri watu bilioni 1.5 duniani.

Magonjwa ya kitropiki yanayopuuzwa yanajulikana kitaalamu Neglected Tropical Diseases (NTDs) ni kundi la magonjwa ya vimelea na bakteria ya kuambukiza yanayoathiri zaidi ya watu bilioni 1.6 ambao ni masikini duniani, ikiwa ni pamoja na watoto milioni 875. Magonjwa hayo husababisha maumivu makali, ulemavu wa muda mrefu na ni chanzo cha vifo kwa watu zaidi ya 500,000 kwa mwaka.

Kwa watoto, maambukizi hayo husababisha utapiamlo, kuharibika kwa utambuzi, kudumaa na kutokuwa na uwezo wa kuhudhuria shule. Watu wazima wanaougua hutengwa na jamii inayowazunguka na kushindwa kufanya kazi. Upungufu wa damu unaosababishwa na NTDs husababisha ongezeko la hatari ya vifo vya kinamama. Maambukizi ya NTD ni makubwa kuliko yale ya malaria au kifua kikuu, magonjwa haya yanashika safu ya juu kati ya makundi manne makubwa zaidi ya magonjwa ya kuambukiza.

The End Fund ni shirika binafsi ambalo linalenga kudhibiti na kuzuia magonjwa matano ya kitropiki yanayopuuzwa (NTDs ) ingawa hutokea mara kwa mara. Tangu mwaka 2014, shirika hili limekuwa mwenyeji wa mikutano yenye mpango wa kuongeza uelewa wa magonjwa hayo.

Dola za Marekani 300,000 zimetolewa kwa ajili ya kuzuia na kudhibiti NTDs nchini Tanzania, nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, Yemen na India.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Kiufundi wa The End Fund, Dk. Peter Hotez, anasema NTDs ni chanzo kikubwa cha umaskini miongoni mwa watu maskini zaidi katika mataifa yanayoendelea.

“Shirika letu ni muhimu kwa kugundua utaratibu mpya wenye ufanisi na gharama nafuu wa kuhusisha sekta binafsi katika kuinua chini watu zaidi ya bilioni kutoka kwenye umaskini,” anasema.

Anafafanua kuwa Shirika la The End Fund limejikita katika kudhibiti magonjwa matano yanayopuuzwa ingawa yanaathiri watu wengi zaidi, ambayo ni minyoo, kichocho, matende, trakoma na Onchocerciasis.

MINYOO

Minyoo ni NTD ya kawaida duniani kote. Husababishwa na kundi la minyoo vimelea inayojulikana kama safura, minyoo ya duara (roundworm) na whipworm (trichuriasis) ambayo huambukizwa kwa udongo ulio na minyoo hiyo au kwa kula mayai vimelea yaliyochanganyikana na chakula wakati wa kula.

Duniani kote, kuna watu milioni 700 wameambukizwa na minyoo ya safura ikiwa ni pamoja wajawazito milioni 44, watu milioni 807 wameambukizwa minyoo ya duara (ascariasis) na watu milioni 604 wameambukizwa minyoo ya trichuriasis. Minyoo hii hutokea na kusambaa hasa katika hali ya hewa ya kitropiki na ambapo usafi wa mazingira ni mbaya.

Maambukizi ya safura kimsingi husababishwa na kutembea peku juu ya udongo wenye minyoo, maambukizi ya minyoo ya duara na whipworm yote husababishwa na kula mayai ya vimelea kupitia chakula. Mara baada ya kuingia ndani ya mwili, minyoo mikubwa huishi katika utumbo na kuzalisha maelfu ya mayai kila siku. Ingawa dalili kutofautiana mtu na mtu, dalili hizo zinatia ndani upungufu wa damu, utapiamlo, upungufu wa vitamini A, tumbo kujaa, kupungua uzito, kuhara na kuvimba utumbo. Uchunguzi umeonyesha kuwa watoto walioambukizwa safura, mahudhurio yao shuleni hushuka kwa asilimia 23.

Ingawa njia ya kupima maambukizi ya minyoo ya tumboni ni kwa kutambua mayai vimelea katika kinyesi kupitia darubini, WHO inapendekeza kunywa dawa za minyoo hasa kwa makundi ya watu yote yaliyo katika hatari ya kuambukizwa kama watoto chini ya miaka mitano na wajawazito. Matibabu ni ama mara moja au mbili kwa mwaka kutegemeana na kiwango cha maambukizi katika eneo.

KICHOCHO

Kichocho pia hujulikana kama homa ya konokono ni ugonjwa sugu unasababishwa na minyoo vimelea ambavyo huishi katika aina fulani ya konokono maji. Kichocho ni cha pili kwa malaria kwenye orodha ya magonjwa ya vimelea katika nchi za kitropiki na ni moja ya magonjwa ya minyoo ya kudhoofisha hasa kwa wakazi wa vijijini.

Dalili ya kawaida ya maambukizi makali ya kichocho ni damu katika aidha mkojo au kinyesi. Kwa sababu maambukizi hutokea zaidi kwa vijana waliobalehe, basi mkojo wenye damu ambayo ni ishara ya maambukizi makali mara nyingi huchukuliwa vibaya kama ishara ya kuwa mtu mzima katika jamii ambapo ugonjwa huo hujitokeza zaidi.

Mara baada ya kukutwa na kichocho, matibabu ya haraka, salama na yenye ufanisi ni dawa iitwayo praziquantel. Kimsingi, utoaji wa maji salama na usafi wa mazingira huongozana na matibabu ya praziquantel. Ugonjwa unaweza kuzuiwa na maambukizi kudhibitiwa kwa dozi moja kila mwaka ya praziquantel.

 MATENDE

Huu husababisha ngozi na  tishu zilizo chini ya ngozi ya  mwanadamu kuwa nene. Huathiri  miguu, mikono, figo, korodani  na kusababisha korodani kuvimba na kuwa kubwa.

Ugonjwa wa matende husababishwa  na vimelea vya minyoo vinavyoitwa kitaalamu Wuchereria bancrofti, Brugia malayi, B. timori ambavyo huenezwa na mbu jike aina ya Culex quinquefasciatus na jamii fulani ya mbu dume (Anopheles species) wakati minyoo aina ya Brugia roundworms huenezwa  na mbu wanaoitwa Mansonia. Mbu hawa hueneza ugonjwa huu kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.

Dalili kubwa ya ugonjwa huu ni kuvimba sehemu ya chini ya mwili yaani kwenye miguu na vidole. Pia mtu anaweza kuvimba sehemu ya mikono au mkono wote pamoja na vidole vya mkononi. Wengine huvimba kwenye korodani. Dalili zingine hutia ndani kuhisi uzito na kukamaa kwa mikono au miguu kutokana na uvimbe uliopo, ngozi kuwa nene na ngumu kwenye mikono au miguu, kupata maambukizi ya mara kwa mara kwenye sehemu iliyovimba, maumivu au kutohisi vizuri kwenye mikono au miguu, maumivu ya viungo, kichwa, homa na kutapika.

Ili kubaini ugonjwa wa matende kipimo cha kuangalia damu kwenye darubini hufanyika  ili kuangalia kama kuna mabuu ya ugonjwa huu wa matende. Kwa wale ambao wana ugonjwa huu kwa muda mrefu, mabuu hayaonekani kwenye damu kwani tayari yatakuwa yameshaingia kwenye mfumo wa limfu. Tiba ya matende hutegemea sehemu husika mgonjwa alipo, sehemu ya mwili iliyoathirika, wagonjwa walioathirika ngozi na korodani wanaweza hitaji upasuaji wa kurekebisha sehemu hizo.

 TRAKOMA

Ni ugonjwa unaongoza kwa kusababisha upofu wa kuambukiza duniani kote. Ugonjwa huo ni maambukizi ya bakteria katika jicho yanayosababishwa na chlamydia trachomatis, ingawa husababisha upofu, trakoma inaweza kutibiwa kama ikigundulika mapema. Trakoma huenea kwa njia ya kugusana moja kwa moja na watu walioathirika na njia ya inzi mwenye maambukizi kugusa jicho.

Dalili za Trakoma ni kuwashwa na kuchonyota macho na kigubiko cha jicho kiasi, kutoka uchafu wenye tongo au usaha ni baadhi ya dalili za kwanza za ugonjwa. Kadiri ugonjwa unavyozidi kuendelea dalili kama kuogopa mwanga (photophobia), kuona kiza/kiwi au maumivu ya macho.

Katika sehemu zenye rasilimali duni, njia bora ya kubaini trakoma ni kwa kutumia mfumo wa madaraja uliotengenezwa na WHO. Mfumo wa madaraja ni msingi wa kupima kwa kuangalia na unaweza kufanyika katika ngazi mbalimbali na mtu aliyepitia mafunzo. Kutokana na ukweli kuwa trakoma ni maambukizi ya bakteria, mkakati kwa ajili ya matibabu, kinga na udhibiti yanahusisha mtu binafsi na jamii kiujumla.

 UPOFU

Onchocerciasis pia hujulikana kama upofu mto, ni maambukizi ya jicho na ngozi yanayosababishwa na vimelea minyoo (Onchocerca volvulus), huenezwa kwa kuumwa na inzi mweusi anayepatikana kwenye mifugo iliyo pembezoni mwa mito na vijito. Wakati onchocerciasis si sababu moja kwa moja ya vifo, matokeo ya kijamii na kiuchumi huongeza zaidi idadi ya watu walioathirika, na kuathiri familia na jamii kwa ujumla.

Watu wengi huwashwa ngozi, vipele, vinundu chini ya ngozi na maono kuharibika. Kama ikiachwa bila kutibiwa, ngozi inaweza kuwasha na kusababisha vidonda na maambukizi ya bakteria ambayo yataiendeleza ngozi kuwa mbaya yenye viraka. Maono kuharibika hutokea tu baada ya miaka mingi ya maambukizi makali na kwa hiyo ni kawaida kwa watu zaidi ya umri wa miaka 30.

Mbu mweusi anapomuuma binadamu, hueneza mabuu machanga ya minyoo vimelea. Katika mwili wa binadamu, vinundu vyenye mabuu hutokeza katika tishu na ngozi ambapo minyoo hukomaa na kuzaliana. Mpango endelevu kutoa madawa (ivermectin) kwa jamii kwa sasa ndio msingi wa kudhibiti ugonjwa huu na WHO ina lengo la kudhibiti onchocerciasis kufikia 2020.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles