25.2 C
Dar es Salaam
Saturday, January 29, 2022

MADUDU YA ELIMU YAFICHUKA BUNGENI

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Prof. Joyce Ndalichako

 

 

Na WAANDISHI WETU-DODOMA

WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, jana imewasilisha bajeti yake ya Sh 1,366,685,241,000.00 bungeni, ikiwa pungufu kwa asilimia 4.2, ikilinganishwa ile ya mwaka jana, huku baadhi ya wabunge wakiorodhesha madudu yanayoiandama.

Madudu hayo ni pamoja na yale ya kimfumo na kiutendaji, ikiwa ni pamoja na katika kutekeleza bajeti, kuporomoka kwa kiwango cha elimu, ikichangiwa na makosa ya kwenye vitabu na madeni ya walimu.

Awali kabla wabunge hawajaorodhesha madudu hayo, Waziri anayeongoza wizara hiyo, Profesa Joyce Ndalichako, aliliomba Bunge liidhinishe Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2017-2018 ya jumla ya Sh trilioni 1,366,685,241,000.00 ili kutekeleza majukumu yake katika mchanganuo ufuatao;

Shilingi 88,544,398,736.00 kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya Wizara, bilioni 70,202,722,328.00 mishahara, huku bilioni  18,341,671,408.00 kwa ajili ya matumizi mengine.

Kwa upande wa Wakala na Taasisi zilizo chini ya Wizara, Sh 331,299,025,264.00 zimeombwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na kati ya fedha hizo, Sh 318,393,044,000.00 ni kwa ajili ya mishahara na Sh 12,905,981,264.00 za matumizi mengine.

Katika eneo hilo hilo, Prof. Ndalichako alisema Sh 916,841,822,000.00 zinaombwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo Sh 606,769,616,000.00 ni fedha za ndani, huku Sh 310,072,206,000.00 kutoka kwa washirika wa maendeleo.

“Nimeliomba pia Bunge lako tukufu  liidhinishe jumla ya shilingi 663,123,262,000.00 kwa ajili ya Tume ya Taifa ya UNESCO, kati ya fedha hizo shilingi 330,830,000.00 ni kwa ajili ya mishahara na shilingi 332,292,000.00 ni kwa ajili ya matumizi mengine,” alisema Profesa Ndalichako.

Wakati Profesa Ndalichako akiomba fedha hizo, wabunge wamebaini kuwa katika bajeti ya mwaka 2016-2017 ambayo Bunge liliidhinisha shilingi 1,396,929,798,625.00 kwa Wizara hiyo, ni asilimia 46 tu ndiyo iliyotekelezwa.

Wakati Ndalichako akiwasilisha bajeti yake, taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na ile ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imeinyooshea kidole Wizara hiyo kushindwa kutekeleza ipasavyo bajeti iliyopita.

Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mjumbe wa Kamati  hiyo, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alitolea mfano wa miradi mitano ambayo kamati ilitembelea na kubaini kuwa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) licha ya Wizara hiyo kukitengea bajeti, kwa miaka 10 hakijawahi kupokea fedha yoyote.

Bashe alisema miradi hiyo mitano ni kati ya 16 ambayo ilitengewa fedha kwa mwaka 2016-2017.

Aliitaja miradi hiyo ambayo imechukua asilimia 12 tu ya fedha iliyotengewa kuwa ni wa upanuzi na ukarabati wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mradi wa Hosptali ya kufundishia na kutoa huduma za afya Mloganzila.

Mingine ni Ujenzi wa DIT Teacher Tower na wa Mfuko wa Utafiti wa Maendeleo (COSTECH).

Katika tathmini yake, kamati hiyo imesema ni bora wizara ikachagua miradi michache ya kipaumbele na kuhakikisha inakamilika kabla ya kuanza kwa miradi mingine.

Kuhusu hali ya elimu nchini, Kamati imebaini kuwa ni mbaya na kwamba uwezo wa kusoma na kuandika umezidi kushuka.

Katika hilo ilitolea mfano wa kiwango cha ufaulu, ikieleza kuwa imebaini wastani wa asilimia 80 ya wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka jana walipata kati ya daraja la nne na sifuri, huku daraja la kwanza hadi la tatu wakiwa ni asilimia 23 tu ya watahiniwa wote.

Kutokana na hali hiyo, kamati ilipendekeza mapitio ya uboreshaji upya wa mfumo wa elimu nchini, kwani matokeo yamekuwa sio mazuri na hayaendani na ulimwengu wa kizazi cha teknolojia.

“Kamati inaona kwamba, kuwa na mfumo mbovu wa elimu tusitarajie miujiza katika kupata elimu bora, ni lazima kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika suala la elimu, bila kufanya hivyo tutatoa watu ambao ni wabovu,’’ alisema Bashe.

Kamati hiyo pia imeitaka Wizara hiyo kuufuta waraka unaopiga marufuku watoto wa kike wanaopata mimba kurudi shule.

Katika suala la utekelezaji wa elimu bila malipo, kamati ilishauri serikali kujitahidi kuongeza miundombinu pamoja na motisha katika shule za msingi na sekondari.

Pamoja na hilo, alisema takwimu zinaonesha kuna upungufu wa vyumba vya madarasa 146,106 katika shule za msingi, vyumba vya sekondari 12,568 na matundu ya vyoo 350,110 katika shule za msingi na 27,761 sekondari.

“Si hivyo tu, pia kuna upungufu wa nyumba za walimu 182,899 wa shule za msingi na nyumba za walimu 69,794 wa shule za sekondari,” alisema.

Bashe alisema Kamati hiyo inashauri Serikali kupitia Wizara ya Elimu ishirikiane na Tamisemi kuharakisha uhakiki wa madeni ya walimu ili waweze kuendelea kufanya kazi vizuri.

“Madeni ya walimu wa shule za msingi shilingi trilioni 1.6 yamekuwa ni ya muda mrefu, pamoja na taarifa iliyotolewa na Wizara kwa kipindi cha Oktoba hadi Machi, serikali imelipa madeni yasiyokuwa na mishahara shilingi bilioni 33.1, sawa na asilimia 2 tu ya deni,’’ alisema.

Kamati hiyo pia imeshauri serikali kuongeza bajeti ya Bodi ya Mikopo ili wanafunzi wengi wanaostahili waweze kupata mikopo, lakini pia kuwapa uhuru wanafunzi kuchagua vyuo wanavyotaka.

Wakati huo huo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ililalamikia vitabu vyenye makosa na kutaka Serikali iviondoe mashuleni.

Katika maoni ya kambi hiyo yaliyowasilishwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Lyimo (Chadema), alisema vitabu vyenye makosa ni vile vilivyochapishwa na Taasisi ya Elimu Tanzania.

Alivitaja vitabu hiyo kuwa ni pamoja na kilichoandikwa ‘Najifunza kuhesabu’ cha darasa la kwanza, ‘Najifunza kusoma’, kitabu cha kwanza na cha pili, Najifunza kuandika, Najifunza afya na mazingira na kitabu kilichoandikwa ‘Najifunza michezo na sanaa’.

Pia alikitaja kitabu cha darasa la pili kilichoandikwa ‘Najifunza kuhesabu’ na kitabu cha darasa la tatu kiitwacho ‘I learn English language’.   

“Kuhusu kitabu cha ‘I learn English language’ katika ukurasa wa 16 kinasema ‘these are my parent’, ukurasa wa 35 umeandikwa ‘writing letters of English alphabet,’ ukurasa wa 61 umeandikwa ‘which is long between a pen and a ruler’ na ukurasa wa 143 una maneno yanayosomeka ‘which is the big city of Tanzania’ akimaanisha capital city.

“Katika ukurasa wa 128 kuna mahali panasomeka ‘it catches mosquito’, ukurasa wa 129  ‘he sleeps without mosquito net’, ukurasa wa 130 ‘it eats grasses’ na ukurasa wa 138 pameandikwa ‘the driver is taken the police station’,” alisema Lyimo.

Makosa hayo ya vitabu, yalionekana kuwachefua wabunge wengi ambao wamesema endapo vitaachwa elimu ya Tanzania itaendelea kushuka, kwa kuwa wanafunzi wanafundishwa makosa.

Aliyepata kuwa Naibu Waziri wa Elimu katika utawala wa awamu ya nne, Phillipo Mulugo, ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Songwe (CCM), aliishangaa Serikali kuruhusu vitabu hivyo vyenye makosa vitumike shuleni wakati kuna uwezekano wa kuviondoa.

Katika maelezo yake, Mulugo alivitaja vitabu vingine vyenye makosa kuwa ni vile vya jiografia vya kidato cha tatu na kitabu cha Kiingereza cha kidato cha nne.

 “Haiwezekani mbili mara mbili mtu aseme ni sita wakati sisi tunajua ni nne. Kwa hiyo, hili suala la vitabu mliangalie vizuri kwa sababu haliko vizuri,” alisema Mulugo.

Pamoja na hayo, Mulugo alizungumzia michango inayotozwa katika shule binafsi na kusema ni mingi na Serikali inatakiwa kuipunguza kwa kuwa inawakatisha tamaa wamiliki wa shule hizo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alikitaja kitabu cha Kiingereza cha darasa la tatu kilichoandikwa Kiingereza chenye makosa.

“Kuna kitabu cha Kiingereza cha darasa la tatu kwenye cover yake kimeandikwa ‘I learn English Language’, hiki ni Kiingereza gani hiki? Kitabu kingine ni cha Kiswahili cha darasa la kwanza kimeandikwa maneno kwa kuunganisha.

“Kwa mfano, taja majina ya wanyama, wameandika 'taja majinayawayama’ na pia kuna eneo wameandika kataumeme badala ya kata umeme,” alisema Mbatia.

Pamoja na hayo, Mbatia ambaye amejijengea sifa ya kukosoa masuala ya elimu, alisema mfumo wa elimu ya Tanzania unaharibika kwa sababu kila waziri anayeshika wizara hiyo, anakuja na mambo yake na kusahau ya mtangulizi yake.

Awali Profesa Ndalichako wakati anawasilisha bajeti yake, alisema Serikali imeshatambua uwepo wa vitabu hivyo na kwamba utaratibu wa kuwachukulia hatua za kinidhamu waliohusika katika suala hilo umeshaanza.

 “Kwa hiyo, napenda kulihakikishia Bunge, kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika ili kukomesha uzembe kwenye kazi muhimu za Taifa,” alisema Profesa Ndalichako.

Kuhusu upatikanaji wa vitabu, alisema katika mwaka wa fedha 2016-17 ilitoa nakala 6,862,800 za vitabu vya darasa la pili na nakala 6,818,181 vya darasa la tatu.

Alisema kwa upande wa shule za sekondari Wizara ilitoa jumla ya nakala 1958,628.

Katika bajeti iliyowasilishwa, Prof. Ndalichako alisema Wizara yake itasomesha wahadhiri 100 katika Shahada ya Uzamivu katika fani zilizo na uhaba mkubwa wa wahadhiri katika Vyuo Vikuu vya Umma.

Kuhusu matumizi ya bajeti ya mwaka 2016-2017, wizara yake imegharamia ukarabati wa shule za sekondari 25 pamoja na vyuo 10 vya ualimu.

Alivitaja vyuo hivyo kuwa ni Tabora, Korogwe, Kleruu, Butimba, Morogoro, Tukuyu,Mpwapwa, Kasulu, Songea, na Marangu.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
177,227FollowersFollow
532,000SubscribersSubscribe

Latest Articles