25.4 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

MADIWANI KONDOA WAMNG’OA MWENYEKITI WA HALMASHAURI

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Kondoa, Alhaj Omar Kariati

Na Khamis Mkotya

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa (KDC), wamepiga kura ya kutokua na imani na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Alhaj Omar Kariati.

Uamuzi huo ulifikiwa Februari 3, mwaka huu, ambapo madiwani 23 kati ya 31 walipiga kura ya kumkataa mwenyekiti huyo, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kwadelo kupitia CCM.

Mwenyekiti huyo ameondolewa baada ya madiwani wenzake kumtuhumu kushindwa kutimiza wajibu wake ikiwa ni pamoja na kusaini mkataba tata kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara ya Gubali- Haubi- Ntomoko na Haubi- Pahi.

Mwenyekiti huyo anadaiwa kutengeneza mazingira ya ufisadi kwa kuingiza kipande cha barabara ya Gubali-Haubi katika zabuni ya pili ya Sh milioni 900, wakati kipande hicho kipo kwenye zabuni ya kwanza na mkandarasi wake yupo kazini, akiwa ameshalipwa.

Diwani wa Kata ya Bumbuta, Bashiru Mtoro (CCM), aliwasilisha tuhuma tatu dhidi mwenyekiti huyo, katika kikao maalumu kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti, Hija Suru. Wakati kikao hicho kikiendelea Kariati hakuwepo ukumbini.

Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Mtoro alizitaja tuhuma hizo kuwa ni mwenyekiti kutumia nafasi yake vibaya, kushindwa kutekeleza majukumu yake na ukosefu wa adabu.

Kuhusu kutumia nafasi yake vibaya, Mtoro alisema mwenyekiti huyo kwa kushirikiana na aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo (jina tunalo) walitangaza zabuni ya barabara ya Gubali- Haubi- Ntomoko na Haubi – Pahi, wakati kipande cha Gubali- Haubi mchakato wake ulishakamilika na mkandarasi yupo kazini.

“Mwenyekiti alifanya kikao cha Kamati ya Fedha akiwa na Mkurugenzi ambaye alishaondolewa, walisaini mkataba wa zabuni ya barabara Julai 18, 2016 wakati mkurugenzi akiwa si mtumishi, alishaondolewa kupitia tangazo la Rais Magufuli la Julai 7, 2016 wakati akitangaza wakurugenzi wapya.

“Wakati wanasaini hii zabuni, mkurugenzi mpya alishawasili Kondoa Julai 15, sasa inavyoonekana hawa jamaa walisaini mkataba wakiwa nje, kwa sababu mkurugenzi halali alikuwepo ofisini,” alisema.

Kuhusu ukosefu wa adabu, Mtoro mwenyekiti huyo alikaidi agizo la Mkuu wa Mkoa la kumtaka atengue uamuzi wa kikao cha Kamati ya Fedha cha Julai 15,2016 kilichobariki zabuni hiyo.

“Tarehe 4/8/2016 aliitisha kikao cha Baraza, wajumbe walihoji barua ya Mkuu wa Mkoa, tukataka iletwe isomwe ili tusikie Mkuu wa Mkoa alishauri nini. Majibu yaliyotolewa kwamba barua haipo, wajumbe wakasema hatuwezi kuendelea na kikao hadi barua iletwe, mkutano ukavunjika.

“Badala yake mwenyekiti aliandika barua 18/8/2016 kwenda PPRA akiomba ushauri yenye kichwa cha habari Yah: kupata ushauri wa uvunjaji wa mkataba wa ujenzi wa barabara ya Haubi-Ntomoko- Haubi- Pahi,” alisema.

Kariati

MTANZANIA lilipomtafuta Kariati ili kuzungumzia uamuzi huo, alikanusha tuhuma hizo na kusema zabuni ya barabara hiyo ilifuata taratibu zote za kisheria, huku akisema katika suala hilo kuna hila za kisiasa ndani yake.

Kariati alisema, hakuna makosa yoyote yaliyofanyika katika utangazwaji wa zabuni hiyo na kwamba mzozo huo umesababishwa na uelewa kuhusu jina la mradi wa barabara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles