22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 14, 2024

Contact us: [email protected]

Madhara wanayopitia kinamama waliofunga tumbo baada ya kujifungua

Na AVELINE KITOMARY

UFUNGAJI wa tumbo baada ya kujifungua imekuwa ni utamaduni na desturi kwa muda mrefu katika jamii za Kiafrika hasa nchini Tanzania.

Baada ya kubeba ujauzito kwa miezi tisa kina mama wengi huamini kufunga tumbo ni njia salama zaidi kwaajili ya kuzuia  kutanuka au kuwa kubwa.

Utamaduni huo ulikuwapo miaka yote ya mabibi huku faida pekee ya ufungaji tumbo ikiangaliwa zaidi bila kujali kama kuna madhara yoyote.

Licha ya kuwapo kwa imani mbalimbali kama vile ukubwa wa tumbo humfanya mama aweze kula chakula kingi zaidi lakini hakuna uhakika wa hilo, wengine hukandwa maji ya moto ili kuondoa uchafu tumboni.

Kwa miaka ya nyuma, mwanamke anapojifungua alikuwa akitumia shuka au kanga kujifunga tumbo lakini kwa miaka ya hivi karibuni wanawake hasa wa maeneo ya mijini wamekuwa wakitumia mikanda maarufu kwa jina la belti.

Sio kwa wanawake waliojifungua pekee, bali hata wale ambao hawajajifungua hutumia mikanda hiyo ili kuminya nyama za tumbo na kuonekana warembo zaidi au nguo wanazovaa ziweze kuwakaa vizuri.

“Mimi nilipojifungua mtoto wangu wa kwanza nilishauriwa na mama mkwe wangu nifunge tumbo ili lipungue na nilijaribu lakini baada ya siku kadhaa nikashindwa kutokana na kutokuwa huru hasa katika upumuaji na ulaji.

“Tangu wakati huo, sijarudia tena kufunga tumbo nikasema hata kama litakuwa kubwa sintajali kuliko kuvumilia shida ya kufunga,” anasimulia mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Consolata.

Consolata ambaye ni mama wa watoto wanne anakiri kuwa ufungaji tumbo umekuwa ukiwasaidia kina mama waliojifungua kurudisha tumbo katika hali zao za awali.

“Ingawa tumbo langu sio kubwa ni la kawaida tu lakini pia siamini kuwa ukiwa na tumbo kubwa kama watu wanavyoamini utakuwa unakula chakula kingi naona kiwango kitakuwa kile kile,” anasema.

Katika jamii Consolata ni kati ya wanawake wachache ambao hawafungi tumbo, asilimia kubwa zaidi hufunga tumbo baada ya kujifungua.

“Marafiki zangu na ndugu zangu huwa wanafunga tumbo baada ya kujifungua na wengi wanapenda kwani hakuna anayependa kuonekana kuwa na tumbo kubwa,” anasema.

Mwanamke mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Julieth Minja, yuko tofauti kabisa na Consolata kwani anasema yeye katika uzazi wake wa watoto wanne alifunga tumbo.

“Yaani kufunga tumbo kwetu ni kitu cha  kawaida na huwa tunashauriwa mimi nilipojifungua tu nilifunga tumbo na kwa watoto wangu wote wanne nilifunga,” anaeleza Julieth.

WANAWAKE WANGAPI WANAELEWA MADHARA YA KUFUNGA TUMBO?

Julieth  anasema: “Sijawahi kusikia kuhusu   madhara yoyote ya ufungaji tumbo ila faida yake ni kupungua tumbo na sidhani kama kuna madhara.

Kwa upande wa Consolata naye anasema hajawahi kabasi kujua kama kuna madhara ya kufunga tumbo baada ya kujifungua.

Hata hivyo, swali hilo linajibiwa na Mtaalamu wa Masuala ya Fiziotherapia wa Idara ya Kina Mama katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk. Elieka Kaaya, ambapo anaainisha madhara ya ufungaji tumbo. 

Kwa mujibu wa Dk. Kaaya, tafiti za kisayansi zinaonesha kuwa kuna faida chache lakini pia kuna hasara nyingi zaidi ya ufungaji tumbo baada ya kujifungua. 

Anasema sababu hasa inayofanya mama kutanuka tumbo ni mabadiliko baada ya homoni zinazoachiwa kuruhusu misuli ya tumbo kutanuka ili kuruhusu mtoto kukua.

Anaeleza kuwa kitu kingine kinachotokea ni pingili za mgongo kuruhusu tumbo kuwa kubwa na kumbeba mtoto kwa uzito wake. 

“Kwenye ufungaji wa matumbo, hasara zinakuwa nyingi kuliko faida ambayo ni kurudisha misuli katika hali ya kawaida  ingawa baada ya muda umeharibu misuli ya ndani. 

“Hasara mojawapo ni  kupunguza mfumo  wa upumuaji kwa sababu kuna msuli  unaitwa diaphragm ambao uko juu ya  tumbo, huu una asilimia 60 ya kumfanya mwanadamu aweze kupumua, utakapokuwa umefunga unaweza kukuzuia kupumua vizuri (shallow breathing).

“Hasara nyingine ni  misuli  ya tumbo  kulegea baada ya kukosa nguvu hivyo kupunguza ufanyaji kazi kwa ufanisi kutokana na misuli hiyo  kuumbwa kuwa imara kubeba pingili za mgongo,” anabainisha Dk. Kaaya. 

Anasema ufungaji tumbo huweza kuzuia mzunguko wa damu eneo la chini ya miguu na kuifanya ivimbe hatimaye kusababsha mgando wa damu mwilini. Pindi unapobana unaweza kuzuia mzunguko wa damu chini ya miguu na hata kusababisha kifo. 

“Kwa wale ambao walifanyiwa upasuaji na kuanza kufunga tumbo kabla ya muda unaotakiwa, anaweza kupata ugonjwa wa ngiri (hernia) kutokana na presha kubwa iliyopo baada ya kufunga. 

“Athari nyingine ni mwili kutokuwa huru, pia kasi ya damu kutoka kuongezeka  kwa sababu ya ukandamizaji wa kizazi, kingine unaweza kupata madhara kwenye ngozi  kama vipele na kupoteza maji mengi.

“Kumbuka kuwa mama huyu ananyonyesha kwahiyo anaweza kupoteza maji mwilini (dehydration),” anabainisha.

Anasema kuwa madhara ya baadae ya ufungaji tumbo ni kuumwa mgongo na uwezekano wa kupata ganzi.

“Wanawake wengi  wamekuwa wakilalamika kuumwa mgongo na kupata gazi bila kujua nini sababu, ukisikiliza historia zao utagundua kuwa baada ya kujifungua alifunga mkanda tumboni na utakapomfanyia uchunguzi wa kitaalamu utakuta misuli ya tumbo haina nguvu ya kubeba pingili za mgongo.

“Wapo pia wanaoshindwa kumaliza mkojo wote kwa  sababu misuli sio mizuri na haina nguvu,” anaeleza Dk. Kaaya.

Consolata na Julieth wanakiri kukutana na wanawake waliojifungua wengi wao wakilalamikia kuumwa mgongo bila kujua sababu ni nini. 

Hivyo, wanashauri haja ya kina mama kulielewa hili ili waweze kuepuka hilo.

“Ni kweli kuna wanawake wengi wakijifungua huwa wanalalamikia maumivu ya mgongo, wengine nyonga na hata ganzi lakini kunahaja ya wanawake kupewa elimu ya namna hii wanapofika hospitali kujifungua.  

WANAOTAKIWA KUFUNGA TUMBO

 Dk. Kaaya anasema sio kila mwanamke anatakiwa kufunga tumbo baada ya kujifungua, bali wapo wanaotakiwa kufunga baada ya kushauriwa na mtaalamu wa afya na wengine hawapaswi kabisa.

“Faida za ufungaji tumbo ni chache na  inamuhusu mwanamke ambaye kabla ya ujauzito alikuwa na tatizo la kuumwa mgongo, huyu anatakiwa kuelekezwa na fiziotherapia  jinsi ya kufunga. 

“Faida ya pili ni kufanya misuli ya tumbo kusinyaa baada ya tumbo kurudi, pia inasaidia mama kuzuia pingili za mgongo kutokufyatuka kutokana na misuli kukosa nguvu baada ya kubeba uzito kwa muda mrefu.  

“Mama aliyefanyiwa upasuaji hatakiwi kabisa kufunga tumbo kwa sababu uponaji wake huchukua muda wa wiki nane, ukifunga kabla ya hapo kunadalili za kutoruhusu uponaji wa misuli iliyokatwa,” anasema Dk. Kaaya.

Anasema tafiti zinashauri kufunga tumbo baada ya kutoka leba, lakini zipo nyingine zinasema lazima kupumzika  siku tatu na nyingine zinasema asifunge kabisa.

“Sisi wataalamu tunasema ufungaji huu wa matumbo baada ya kujifungua uruhusiwe na mtaalam wa afya, yeye ndio ataona umuhimu wa  kufunga tumbo au la.

“Baada ya elimu tunayoitoa hasa hapa  Muhimbili, wengi wamepunguza ufungaji wa mikanda na hata hapa idadi  ya wanawake wanaojifungua na baadaye kuja katika idara hii kutokana na matatizo ya migongo wamepungua kwa kiasi kikubwa.

“Kwahiyo, sisi tulichokifanya ni kuzuia madhara baada ya kujifungua na kupunguza gharama za kutoka nyumbani kuja hospitali kwaajili ya kutibu maumivu ya mgongo. 

“Kwa kiasi kikubwa sasa idadi ya kina mama waliokuwa wanajifungua na   kufunga matumbo wanaokuja hospitali wakiumwa migongo imepungua kwa sababu ya elimu tunayoitoa hapa,” anaeleza Dk. Kaaya.

MAZOEZI NI SALAMA ZAIDI

Kwa kawaida, sio jambo rahisi kubadilisha mitazamo ya jamii fulani ila inawezekana kulingana na mapokeo ya elimu itakayotolewa.

Dk. Kaaya anasema mama aliyejifungua anaweza kufunga mkanda baada ya kushauriana na mtaalamu aina ya mkanda  na sehemu ya kufunga. 

“Kuna mikanda mingine unaweza kufunga chini ya kitovu na kuna mwingine unafunga chini ya maziwa kwa lengo la kutaka kuondoa kiribatumbo cha chini ya kitovu, pia kuna mikanda mingine ni ya kuimarisha pingili za mgongo na tumbo. 

Anasema pia huwa wanawashauri kina mama wanaojifungua badala ya kufunga mikanda wafanye mazoezi ya tumbo kwa kelekezwa na mtaalamu wa afya.

“Tunatoa huduma za mazoezi kulingana na uchunguzi tunaomfanyia hivyo, kila mama anafanya mazoezi kulingana na kazi anayofanya. 

“Ili kupunguza tumbo inahitajika kufanya mazoezi kulingana na jinsi utakavyoelekezwa na mtaalamu wa afya na kubadilisha aina ya ulaji, hata kufunga mikanda wanatakiwa kushauriwa na wataalamu wa afya.

“Kwa kinamama wa ofisini tunawafundisha namna ya kufanya mazoezi ya tumbo tunaita kitaalam ‘isometric exercise’  mfano; ukiwa umesimama, umekaa au unatembea basi unavuta tumbo lako ndani halafu unaachia unahesabu moja hadi 15… mazoezi kama haya hayakulazimu uje kumwona fiziotherapia kila wakati.

“Mazoezi mengine yanaitwa ‘sit ups’ haya hutolewa baada ya kufanya uchunguzi sahihi kwa mhusika, unaweza kushuriwa ulale kwa kukunja miguu au ukunje ukiwa umelala ubavu au chali, lakini kuna mwingine anaweza kuwa na matatizo ya mgongo kwahiyo aina hii ya mazoezi hayamfai. 

MATUMIZI DAWA ZA ASILI 

Dk. Kaaya anasema sio suala rahisi kuzungumzia kuhusu dawa za asali, kwa sababu ya kutokujua utendaji kazi wake kisayansi.

“Lakini ninaweza kuzizungumzia katika ufanyaji kazi kwenye misuli, kwa sababu ili misuli iwe imara na kujirudi ni lazima mafuta yapungue, na mtaalamu wa lishe aangalie aina ya vyakula na mazoezi yanayopaswa kufanywa. 

ATHARI  KWA AMBAO HAWAJAJIFUNGUA 

Wapo wasichana ambao hawajawahi kujifungua lakini wanafunga tumbo kwa kutumia mkanda ili kuwa na mwonekana mzuri.

Dk. Kaaya anasema ufungaji tumbo kwa wasichana ambao hawajajifungua bado unaweza kuwasababishia madhara katika mifumo ya ndani kama figo, mbavu na mfumo wa upumuaji. 

“Hali hiyo inaweza kufanya misuli kutofanikiwa kufanya kazi inavyostahili kwa sababu unakuwa umeibana na unapotembea unalemaza misuli ya tumbo  na mgongo hivyo, hautumii nguvu ya misuli. 

“Nawashauri namna bora ya kutengeneza muonekano mzuri ni kufanya mazoezi  na ulaji bora.

“Na kwa mazoezi ya mtu ambaye hajajifungua ni lazima kwanza ujue mwili wako ukoje hasa afya ya moyo, pia ni vema ukaonana na mtaalamu wa mazoezi ili akufundishe namna bora ya kufanya mazoezi kulingana na atakavyokuelekeza,” anashauri Dk. Kaaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles