26.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Mabweni, maji yawaliza wanawake Mwanza, Amani Girls yatia mkono

Na Mwandishi wetu, Mwanza

Tatizo la upatikanaji maji na upungufu wa mabweni katika shule za sekondari mkoani Mwanza yamewaibua wanawake ambao wameiomba Serikali kutatua changamoto hizo pamoja na nyingine zinazokwamisha kushiriki kwenye shughuli za maendeleo na kujikwamua kiuchumi.

Hayo yameelezwa Machi 8, 2024 na Zaena Seif alipokuwa akisoma risala kwa niaba ya wanawake wa mkoa wa Mwanza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani, ambayo mkoa wa Mwanza yamefanyika leo katika Uwanja wa Amani wilayani Misungwi.

Zaena amesema mkoa huo unazo shule 30 tu za bweni za wasichana kwa shule za sekondari na tano za msingi na kusisitiza kwamba uwepo wa mabweni mengi utasaidia wasichana wengi kutimiza ndoto zao na kuwa na wanawake bora wenye elimu na maarifa, huku tatizo la upatikanaji maji likisababisha watumie muda mwingi kuyasaka na kushindwa kushiriki shughuli za maendeleo.

“Tuna changamoto za kuachiwa majukumu makubwa na mazito ya kulea na kuendesha familia, mila potofu na mfume dume unaomkandamiza mwanamke na kumfanya asishiriki masuala ya maendeleo, na mmonyoko wa maadili umesababisha wanawake kutotimiza majukumu yao,” amesema Zaena

Afisa Habari wa Shirika la Amani Girls, Rachiel Alute akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani ambayo Mkoa wa Mwanza yamefanyika katika Uwanja wa Amani wilayani Misungwi.

Akizungumzia baadhi ya changamoto hizo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla amesema Serikali inaendelea kuzifanyia kazi huku akibainisha kwamba uwekezaji sekta ya maji unaendelea kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 upatikanaji wa maji maeneo ya vijijini unafikia asilimia 85 kutoka 70 ya sasa.

“Miaka 63 baada ya uhuru hali ya usawa ni ya kuridhisha katika nyanja zote na tumeshuhudia wanawake wanapewa kazi na wanachapa kazi, changamoto zenu nimezipokea na zote zitafanyiwa kazi mmeeleza changamoto saba, Serikali tunaendelea kuhakikisha wanawake wanaelimishwa katika shughuli za kiuchumi na wapewe fursa sawa kwenye miradi ya maendeleo.

“Niwaombe wanawake washiriki kwenye nafasi mbalimbali za kugombea uongozi, wasaidiane na wasiangushane, wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi za uongozi kwenye chaguzi zinazokuja pia mshiriki kwenye malezi na kuwa kioo,” amesema Makalla

Akizungumzia namna Shirika la Amani Girls la Mwanza lilivyowawezesha wanwake, Mkuu wa Idara ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto, Margareth Cyprian, amesema tangu mwaka 2013 wamewajengea uwezo wanawake kupitia program za elimu, afya na uhifadhi wa jamii.

Amesema wanashirikiana na wanawake kuunda vikundi vya ujasiriamali kujikwamua kiuchumi na kusiaida kutoa lishe kwa elimu ya awali, kuwahamasisha kufikisha elimu ya afya ya uzazi kwa vijana wao waliopo kwenye rika balehe pamoja na kujikinga na vitendo vya ukatili wa kijinsia na kushiriki shughuli za maendeleo ili kujisimamia wenyewe kiuchumi.

“Kwenye elimu tumeanzisha vikundi vya wanawake ambao wamepatiwa elimu ya ujasiriamali ili wajikwamue kiuchumia ngazi ya familia na kijamii mpaka sasa zaidi ya 5,300 wamefikiwa. Kwenye uhifadhi wa jamii wanawake na wasichana wanashiriki katika shughuli za uzalishaji mali ili wasiwe tegemezi ambapo hapa tumewafikia zaidi ya wanufaika 5,000.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla (Kulia) akifurahia wakati akikagua banda la Shirika la Amani Girls kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Dunia, Mkoa wa Mwanza ambayo yamefanyika uwanja wa Amani wilayani Misungwi.

“Katika eneo la afya tumeshirikiana na wanawake kuwapatia elimu ya afya ikiwemo vita dhidi ya Malaria, wakiwa wazazi wa rika balehe tunashirikiana nao kuhamasisha vijana wao kushiriki katika huduma za afya ya uzazi na tunatoa elimu za lishe zinazowasaidia kuwekeza katika watoto wao ili kutatua udumavu kwenye jamii na katika hili tumewafikia akina mama zaidi ya 6,000,” amesema Margareth na kuongeza kuwa;

“Nawaomba wanawake wawe na utayari fursa hizi zinapokuja katika maeneo yao wasiziache wajiingize na wanufaike kuleta maendeleo katika maeneo yao, na sisi tunaendelea kuwekeza kwao ili kupata jamii yenye maendeleo na kupata maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii kwa ujumla,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles