23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

MABOMU YATAWALA UCHAGUZI WA MARUDIO

*Dereva wa Mbunge Chadema ajeruhiwa, CCM yaongoza Ubunge, udiwani

Na Waandishi Wetu


 

mtz1UCHAGUZI mdogo wa Jimbo la Dimani, Wilaya ya Magharibi “B”,  Mkoa wa Mjini Magharibi  Zanzibar na ule wa udiwani katika kata 20 Tanzania Bara, umefanyika huku mabomu ya machozi na vurugu vikitawala vituoni.

Kutokana na hali hiyo baadhi ya wananchi walijikuta wakijeruhiwa kwa mabomu na wengine kupigwa na vitu vyenye ncha kali.

Takribani maeneo yote ambapo uchaguzi huo wa marudio ulifanyika jana kuanzia asubuhi mpaka saa 10 jioni vituo vilipofungwa.

Wananchi walikuwa wakijitokeza kwa uchache tofauti na idadi ya watu walioandikishwa kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Kahama

Katika Kata ya Isaghehe Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Jackson Peter  ambaye ni dereva wa Mbunge wa Viti Maalimu Chadema, Salome Makamba, alishambuliwa na vijana wasiojulikana na kumkata shingoni na kitu chenye ncha kali.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema), alisema dereva huyo alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Land Cruiser yenye namba za usajili T 581 BJB akizungukia vituo vya kupigia kura kwenye kata hiyo, ndipo kundi la vijana lilipozuia gari hilo na kuanza kumshambulia.

“Green Guard wa CCM wameshambulia gari ya mheshimiwa Salome Makamba na kumjeruhi vibaya dereva wake ambae tumempeleka Hospital ya Kahama mpaka sasa hajitambui,” alisema Heche.

Kagera

Katibu Mwenezi wa Jimbo la Muleba Kusini, Hamis Yusuph pamoja katibu wake,  Elisha Kabombo (Chadema) wamekamatwa na polisi wakiwa kwenye harakati za kuzungukia vituo vya kupigia kura katika Kata ya Kimwani wilayani Muleba mkoani hapa, huku chanzo cha kukamatwa kwake kikiwa hakijaelezwa.

Taarifa kutoka Kata ya Kimwani kulipokuwa kukifanyika uchaguzi, zilisema viongozi hao walikamatwa wakiwa kwenye harakati za kufuatilia uchaguzi huo katika vituo mbalimbali.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kagera Augustine Ollomi hakupatikana jana kuzungumzia hali hiyo, simu yake ya mkononi haikuwa hewani.

Morogoro

kwa upande wa Kata ya Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro, polisi walitawanya watu kwa mabomu katika mitaa ya Lusogo na Ngazengwa hatua iliyochukuliwa baada ya wafuasi wa vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo kuonekana wakiwa kwenye  makundi makundi waksubiri.

Katika uchaguzi huo watu waliojitokeza walikuwa wachache tofauti na ilivyozoeleka kwenye chaguzi nyingine.

Arusha

Katika Kata ya Mateves iliyopo katika jimbo la Arumeru Magharibi na Ngarenanyuki-Arumeru Mashariki mkoani Arusha, wananchi waliojitokeza  katika vituo vya kupigia kura walikuwa wachache tofauti na ilivyozoeleka katika chaguzi zilizopita.

Katika Kata ya Mateves, upigaji kura ulianza mapema huku kukiwa na idadi ndogo ya wapiga kura.

Akizungumzia hali hiyo mmoja wa wasimamizi wa kituo cha kupigia kura katika kata hiyo ambaye hakuwa tayari kujitambulisha akidai si msemaji,  alisema tangu walipofungua kituo chao wananchi walikuwa wakijitokeza ingawa hawakuwa wengi.

Uchaguzi wa Mateves unafanyika baada ya Mahakama kutengua udiwani wa kata hiyo ambapo wagombea waliochuana ni Jeremia Ole Leken (Chadema), Saing’orie Mollel (CCM), Phil Klerruu (NCCR- Mageuzi) na Rashid Daa (CUF).

Na kwa upande wa Kata ya Ngarenanyuki iliyopo Arumeru Mashariki nako hali ya usalama wakati wa zoezi la upigaji kura mpaka mchana usalama na amani viliendelea kutawala katika vituo vingi.

Wakati tukiwa tunakwenda mtamboni taarifa kutoka katika kata hiyo zinaeleza kuwa CCM imefanikiwa kutetea kiti hicho kwa mgombea wake Saing’orie Mollel kuibuka na ushindi dhidi ya wagombea wa vyama vingine.

Dar

Jijini Dar es Salaam pia uchaguzi wa udiwani Kata ya Mtoni Kijichi, waliojitokeza kupiga kura walikuwa wachache ikilinganishwa na uchaguzi uliopita.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya aliyekuwa Diwani wa Kata hiyo, Charles Anderson (CCM), kufariki dunia mwaka jana.

Katika Kituo namba nane kilichoko katika ofisi ya Mtendaji wa Mtaa wa Kijichi, wapigakura walioandikishwa walikuwa 475 lakini hadi saa 8:37 mchana waliokuwa wamepiga kura ni 76 tu.

“Mwitikio wa watu ni mdogo sana, mwaka jana muda kama huu (saa 8:37 mchana) ungekuta hapa watu wamejaa, lakini sasa hivi unatuona tunapiga story (tunazungumza),” alisema Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Mtoni Kijichi, Frank Komba.

Uchaguzi Dimani

Katika uchaguzi wa kujaza nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Dimani, wananchi walijitokeza kwa uchache kwenye vituo vingi huku kukiwa na askari wengi waliokuwa wakirandaranda mitaani kwa magari yao.

Katika uchaguzi huo, Chama cha Wananchi (CUF), walilalamika kufanyiwa hujuma kwa mawakala wao kutolewa kwenye vituo vya kupigia kura.

Mkurugenzi wa Uchaguzi CUF, Omar Ali Shehe, alisema kinachofanyika si uchaguzi bali ni ‘utaratibu wa kibabe kwenye kile kinachoitwa demokrasia ya vyama vingi’.

Taarifa hizo za CUF zilisema mawakala sita wa chama hicho na wengine wa vyama vya upinzani, walitolewa nje ya vituo bila sababu za msingi.

CCM

Kwa upande wake Naibu Katibu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema chama chao hakihusiki na udanganyifu wowote katika uchaguzi huo.

Alisema mwenendo mzima wa upigaji kura umekuwa huru na wa haki na ndio maana wananchi wanapiga kura bila tatizo .

“Chama chetu kimekua na utaratibu wa kujenga wanachama wake imani na ndiyo maana tunaendelea kuaminiwa kila siku,” alisemai Vuai.

Kauli ya NEC

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Hamid Mahmoud Hamid, alisema hakuna mawakala waliotolewa nje ya vituo vya kupigia kura na kwamba taarifa hizo zinazosambazwa ni uzushi.

“Kama kuna mawakala wametolewa nje basi itakua wana makosa na ndio maana huenda ikawa wametolewa. Wapo baadhi ya mawakala nimepewa taarifa walikua wanazungumza na simu kwenye vituo kitu ambacho hawakutakiwa kufanya hivyo,’’ alisema Hamid.

Habari hii imeandaliwa na Na Muhammd Khamis (UoI) Zanzibar , ELIYA MBONEA, Arusha na Nora Damian, Dar

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles