25.1 C
Dar es Salaam
Saturday, December 9, 2023

Contact us: [email protected]

Maafisa Ugani Maswa wakabidhiwa pikipiki

Na Samwel Mwanga, Maswa

MAAFISA Ugani 17 katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu wamekabidhiwa pikipiki kwa ajili ya kuwasaidia kuinua Sekta ya Kilimo sambamba kuongeza mapato katika Halmashauri ya wilaya hiyo.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Juni 13, 2022 na Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Paul Maige kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Maswa wakati wa kukabidhi pikipiki hizo kwenye viwanja vya halmashauri ya wilaya ya Maswa.

Maafisa ugani hao wameaswa kutumia pikipiki hizo kwa uadilifu mkubwa kwani sekta hiyo ndiyo msingi mkubwa ambao utatutoa kwenye uchumi tegemezi na kuupaisha juu kwani Watanzania walio wengi wamejikita kwenye kilimo.

“Mie najua ninyi ni waadilifu hivyo ni vizuri mkafanye kazi kwa bidii mara baada ya kupata hizi pikipiki na sekta ya kilimo ndiyo msingi mkubwa wa uchumi wa nchi yetu na sasa tumetoka kwenye uchumi tegemezi na tunaelekea uchumi wa juu hivyo mkasimamie kilimo ambacho Watanzania walio wengi wanajishughulisha nacho,”amesema Maige.

Pia ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu kwa kuwezesha kupatikana kwa pikipiki hizo kupitia wizara ya kilimo.

Nae Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Vivian Christian amesema kuwa ni vizuri pikipiki hizo zikatumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo huku akitaka kuwepo na mkataba ili kuwabana watakaotumia kinyume na ilivyokusudiwa.

“Hatutarajii hizi pikipiki zigeuzwe kufanywa bodaboda za kusafirisha abiria au tuzikute mkifanyia starehe kwenye maeneo ya starehe zifanye kazi za kiserikali na tutaweka mkataba kati ya halmashauri na ninyi ili ukikiuka tunakunyanganya,”amesema Christian.

Awali, Afisa Kilimo,Umwagiliaji na Ushirika wilayani humo, Robert Urasa amesema kwamba kwa sasa Maafisa Ugani na Ushirika ambao kwa ujumla yao wako 45 wilayani humo kila mmoja ana pikioiki.

Amesema kuwa awali walipokea pikipiki 28 kutoka Wizara ya kilimo kupitia Bodi ya Pamba na sasa wamepokea pikipiki 17 kutoka Wizara ya Kilimo hivyo Maafisa ugani watawafikia wakulima na kuwapatia Elimu na Ushauri.

Urasa amesema katika kufanya hivyo tija ya uzalishaji wa mazao ya biashara na chakula itaongezeka pia watasaidia kuhamasisha katika masuala ya kilimo na mifugo,masuala ya ushirika hasa katika Vyama vya Ushirika vya Msingi(Amcos)katika maeneo ya vijijini na kwenye Kata.

Aidha, amesema kuwa pikipiki hizo zitasaidia kwa Maafisa ugani kufuatilia na kutoa takwimu sahihi za ununuzi wa zao la pamba katika maeneo yao ukizingatia hiki ni kipindi cha musimu wa uuzaji wa zao hilo kwani halmashauri hiyo inategemea mapato ya ndani kupitia ushuru wa zao hilo.

Maafisa ugani  hao waliokabidhiwa pikipiki hizo waliishukuru serikali kuwapatia vyombo vya usafiri na kuhaidi  kuweza kuwafikia wakulima mara kwa mara jambo litachangia sekta ya kilimo kwa kiwango cha juu  kuinua kipato cha Taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles