25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

AG Feleshi abariki Bodi ya Wanahabari, wadau wapongeza

*Asema Ofisi yake inaunga mkono hatua zinazochukuliwa

*Wadau wasema ni mwanzo mzuri

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Eliezer Feleshi amependekeza kuundwa kwa Bodi ya Wanahabari itakayosimamiwa na wanahabari wenyewe.

Amesema kuundwa kwa chombo hicho ndio kitachokuwa na wajibu wa kusimamia wanahabari na hata kuwashughulikia endapo watakwenda kinyume na maadili ya tasnia hiyo.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Eliezer Feleshi (wakwanza kushoto) alipokutana na Ujumbe wa TEF na MISA-TAN uliiongozwa na Mwenyekiti wa TEF, Dodatus Balile mapema leo ofisini kwake jijini Dodoma.

Jaja Feleshi ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Juni 13, 2022, ofisini kwake bungeni, jijini Dodoma alipokutana na wadau wa habari nchini.

“Sina tatizo, naona muwe na ‘regulator’, bodi yenu moja, ili mmoja wenu akienda kinyume na maadili (ya uandishi wa habari), mnamshughulikia nyinyi wenyewe,” amesema Jaji Feleshi.

Jaji Feleshi ametoa kauli hiyo baada ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF), Deodatus Balile, kumweleza kuwa, wanahabari wanapendekwa kuundwa kwa chombo kimoja kitakachosimamia wanahabari badala ya vyombo vinne kama inavyoelekezwa na Sheria ya sasa.

Pia, Balile amemweleza Jaji Feleshi kuwa, miongoni mwa mambo yanayotisha wanahabari katika sheria iliyopo sawa, anaweza kufungwa bila hata ya yeye (mwanahabari) kuitwa kusikiliza kesi yake.

“Niko na nyinyi na Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) katika hatua kuelekea mabadiliko ya sheria za habari. Sheria yoyote lazima ipitiwe vizuri na iwe na uhalali lakini pia iwe ya wananchi.

“Ofisi yangu ipo pamoja na hatua zinazochukuliwa na wanahabari katika kuyaendea mabadiliko yanayotakiwa,” amesema Jaji Feleshi.

Wadau wapongeza

Akizungumza na Mtanzania Digital kuhusua hatua hiyo, Balile amesema wamepokea mikono miwili kauli hiyo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali nakwamba lengo nikuona tasnia hiyo ikiwa na chombo kimoja kama ilivyo katika fani nyingine.

“Tumepokea kwa mikoano miwili kauli hii, kwani ndicho tunachokihimiza kwamba badala ya kuwa na vyombo vinne, tunahitaji tasnia ya habari iongozwe na chombo kimoja kama ilivyo kwa Wanasheria wana (TLS), kama ilivyo kwa Madaktari wana Baraza la Madaktari, Wauguzi na Wafamasia, kama ilivyo kwa Wakandarasi wana bodi ya Wakandarasi(CRB), kama ilivyo kwa Wagavi na Wahasibu wana (NBAA).

“Sasa sisi kuwa na vyombo vinne, Idara ya Habari(MAELEZO) hii tunaweza kusamehe ikaendelea kuwepo kwa ajili ya kazi za serikali, lakini Mfuko wa Mafunzo, Baraza la Ithibati na Baraza Huru la Habari hivi vyombo vitatu vinapaswa kuunganishwa kuwa chombo kimoja, hii itasaidia kwamba tuwe na dira.

“Kama ambavyo wanasheria wanapewa vitambulisho na TLS hata sisi hatutaki Idara ya Habari(MAELEZO) iendelee kutoa Press Card kwa waandishi wa habari bali zitolewe na hilo balaza huru litakalokuwa limeundwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Balile.

Katika hatua nyingine Balile amesema kuwa hiyo ni hatua njema kwani serikali imeonyesha nia njema ambayo awali haikuwepo.

“Tunashukuru serikali imeonyesha nia na hata hivi tunavyoendelea kuzungumza ni nia njema tunayoiona ambayo awali haikuwepo, Waziri(Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye) ameshaleta mapendekezo, tunasema tunashukuru kwa mapendekezo aliyoyaleta kuanzia kifungu cha 38 mpaka 67.

“Lakini tunamuomba na tunaiomba serikali kwamba waanzie kifungu cha 1 mpaka cha 67, tusibakize vifungu ili tukarekebisha nusu tukabaki tena kugombania nusu itakayokuwa imesalia,” amesema Balile.

Juni 10, mwaka huu akizungumza katika warsha ya kuwajengea uelewa wanahabari kuhusu mapendekezo ya Sheria ya Habari yaliyowasilishwa serikalini, Wakili James Marenga alisema kuwa moja ya mapendekezo waliyowasilisha ni pamoja na tasnia hiyo kuwa chombo chake kitakachoisimamia kama ilivyo kwenye fani nyingine ikiwamo ile ya sheria.

“Ikiwa Mwanasheria anahukumiwa na wanataaluma wenzake kwenye bodi yao, mwanahabari naye anapaswa kuhukumiwa kwenye bodi itakayoundwa na wao wenyewe na si bodi iundwe na serikali ama waziri,” alisema Marenga.

Mbali na Balile ujumbe huo pia uliambatana na Kaimu Mtendaji Mkuu wa TEF, Anita Mendoza, Makamu Mwenyekiti wa MISA- TAN, Wakili James Marenga na wadau wengine wa habari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles