23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Ma-DC, Ma-RC waja na staili mpya

WAANDISHI WETU-NJOMBE/KATAVI/TABORA

NI staili mpya ya uongozi. Ndivyo unaweza kusema baada ya wateule wa Rais Dk. John Magufuli, kuibuka na staili ya aina yake katika kuongoza katika maeneo yao.

Katika staili hiyo, Mkuu wa Wilaya ya  ya Ludewa mkoani Njombe, Andrea Tsere, ameagiza watu wote wanaoishi bila ya kufunga ndoa wapelekwe mahabusu.

Hatua ya kutangaza uamuzi huo unatokana na kile alichokiita sababu ya tabia ya kuoana baada ya miaka mitatu wanaachana na kusababisha kukithiri kwa wimbi la watoto wa mitaani.

Wakati Tsere akiyasema hayo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera, ameibuka na mpya ambapo amewataka waganga wa jadi kutumia utaalamu wao kuwaloga watu  waende  wakapige kura  na kuchagua viongozi wazuri  kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, mwaka huu.

Kwa upande mwingine, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, ameibuka na mpya baada ya kumwaga machozi kanisani wakati wakiombea kukomeshwa kwa mauaji ya watu mkoani kwake jambo ambalo limezua mjadala mitandaoni baada ya video yake kusambaa kwa kasi.

DC Tsere na wasiooa

Katika agizo kuhusu wasiooa, Tsere alitoa agizo wakati akizungumza katika kongamano  la wanaume lililoandaliwa na umoja wa makanisa wilayani Ludewa mkoani Njombe, lililokuwa na lengo la kupinga mila potofu lililofanyika  Kata ya Mavanga mwishoni mwa wiki.

Alisema watu wamekua wakiishi na kuzaa na kwa sababu hajawafunga ndoa, wamekuwa wakiachana bila ya utaratibu wowote.

“Sasa ili tupunguze habari ya watoto wa mitaani watu wasiofunga ndoa wafunge ndoa na anayebisha apelekwe mahabusu. Kwa sababu waliamua kutafutana na kukaa kama mtu na mke, ni vyema kuhalalisha ili liwe kwa mujibu wa sheria.
“Kwa ambaye hataki baadae anataka kusababisha watoto wa mtaani, unatuletea sisi Serikali matatizo, mahabusu mtakwenda kwa sababu nyie pia ni wahalifu,” alisema.

“Hii tabia ya vijana kuoana baada ya miaka mitatu kuachana imekua sugu, mbaya zaidi wanasababisha wanaume kwa sababu malalamiko mengi katika ofisi yangu, ni mwanamke ameachwa  na mwanaume.

“Unakuta amemzalisha watoto wawili au watatu sana sana wawili au watatu hawazidi hapo ameshapata mwanamke mwengine yule kesi kila siku jioni.

 “Na mwingine anasema ukitaka kujua kama mimi sina habari na wewe ananunua kufuli jipya anafunga mlangoni alafu yeye anamtoa nje,” aliongeza.

Alisema kama mwaaume ana uwezo wa kuoa mke wa pili ni vyema aoe na kuwatunza wote na si kuanza kujenga uadui na yule wa kwanza wakati alishampa ahadi nyingi.

“Leo hii umezaa naye mtoto wa kwanza, mtoto wa pili unamuacha, sasa ukimuacha bahati mbaya ndugu zako wanakuunga mkono mwanamke anakua ana haki kwa kweli utakwenda mahabusu tu,’’ alisema Tsere.

Kwa upande wa Paroko wa Parokia ya Mavanga, Padre Method Msanga, alisema lengo la kuandaa kungamano hilo ni kuwakutanisha wanaume kwa lengo la kuwaimarisha kiimani pamoja na kuwaelimisha madhara ya mila potofu.

“Sisi kama makanisa tutaendelea kuwashika vijana, wanawake na wanaume ili kuwakomboa wale wote wanaoteseka na mila potofu na kushindwa kupiga hatua kimwili na kiroho,’’ alisema Msanga.

Naye Mchungaji wa Kanisa la Anglikana, Faraja Mapunda,  alisema changamoto wanazokutana nazo wanaume ni kwa sababu hawashiriki kanisani, badala yake wanaendekeza mila potofu  

RC Homera na waganga S/Mitaa

Katika tukio jingine, Mkuu wa  Mkoa wa  Katavi, Juma  Homera  amewataka waganga wa  jadi kutumia utalaamu wao kuwaloga watu  waende  wakapige kura  na kuchagua viongozi wazuri  kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji.

Homera  alitoa kauli hiyo, wakati wa  kikao chake  na   waganga wa jadi  wa   Mkoa wa  Katavi mjini Mpanda .

Alisema waganga wa  tiba za  asili  wamekuwa wakiwahudumia watu wenye imani  tofauti na watu wamekuwa wakiwaamini  kwa tiba zao.

Aliwataka watumie utalaamu wao kuwaloga watu ili wakapige kura kwa wingi na kuwachagua  viongozi wazuri kwenye uchaguzi ujao.

Aliwaonya kuacha tabia ya kutumia nyara za Serikali kwenye shughuli zao na kutumiwa na majangili na majambazi .

Alisema kumekuwapo na tabia ya  waganga wa jadi  kuwadanganya majangili na majambazi kuwa wakipewa  tiba inayotokana na nyara za Serikali kama vile nyayo ya fisi, jangili akiingia ndani ya hifadhi na kuua wanyama  askari hawezi kumuona au kukamatwa kitu ambacho sio kweli.

Alisema  kuanzia sasa katika  mkoa huo,  waganga wote wa asili wanatakiwa watambuliwe na wajulikane  wanatibu nini  na wanafanyia kazi zao wapi.

“Tumepanga  kufanya  msako  wa kuwasa wale wote wanaofanya shughuli bila kuwa na kibali,” alisema.

Kamanda wa Polisi wa  Mkoa wa  Katavi, Benjamini  Kuzaga, alisema hawatosita kuwakamata waganga  wa jadi  ambao watakutwa  wakiwa na nyara za Serikali pasipo kuwa na kibali cha kumiliki.

Aliwatahadharisha kuacha kupiga ramli chonganishi  kwani zimekuwa zikisababisha  kutokaea kwa mauaji kwenye baadhi ya maeneo ya mkoa huo .

Mwenyekiti wa  Waganga wa  Jadi wa   Mkoa wa Katavi,  Siasa Kashindye alisema mpaka sasa wana waganga wa jadi zaidi ya 2,000 ila wengi wao hawajasajiliwa.

RC Mwanri aangua kilio

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri  aliangua kilio kuombea mauaji yanayoendelea katika mkoa huo, alipokwenda katika Kanisa la Pool of Siloam mkoani humo mwishoni mwa wiki.      

Mwanri aliwaangukia wachungaji na waumini wa Kanisa hilo na kupiga magoti, huku akiomba mauaji yakomeshwe na watu wamrudie Mungu.

“Hii Tabora inahitaji maombi na numekuja kuhudhurisha kilio, kama Mungu alifika mahali akaihurumia Ninawi kiasi hicho, jee Mungu huyo huyo hataihurumia Tabora hapa mauaji yakaondoka katika mkoa huu, watu wakaacha kuuana kama wanavyouana na Kanisa la Bwana likafanya kazi hii ya kuomba na shetani akaondoka mahala hapa.

“Na madhabahu hizo zikaondoka kabisa mkajua zimeondoka na neno la Mungu likahubiriwa mahali hapa, na watu wakatii sauti ya Mungu katika mkoa huu,” alisema.

Habari hii imeandaliwa na Elizabeth Kilindi (Njombe), Walter Mguluchuma (Katavi)na nyongeza Andrew Msechu (Dar)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles