23.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa: Sijakata tamaa

mbili*Asema ameshindwa pambano si vita

*Ajipanga upya agoma kueleza mikakati yake

*Ukawa wataka ZEC imtangaze Maalim Seif Z’bar

Na Fredy Azzah, Dar es Salaam

WAZIRI mkuu wa zamani na aliyekuwa mgombea urais kupitia Chadema, Edward Lowassa, amesema ataendelea kupambana katika siasa na kwamba yawezekana ameshindwa katika pambano lakini si vita.

Lowassa aliyasema hayo jana katika mkutano na waandishi wa habari, baada ya kuulizwa nini hatima yake ya kisiasa baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, ambapo Rais Dk. John Magufuli aliibuka mshindi.

Akijibu swali hilo, Lowassa alisema. “Nitaendelea kuwa active (imara) kwenye siasa, I might lost the battle but not the war  ‘yawezekana nimeshindwa pambano lakini si vita,” alisema Lowassa.

Lowassa ambaye katika uchaguzi huo alikuwa mshindi wa pili kwa kupata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 nyuma ya Rais Magufuli aliyeshinda kwa kura 8,882,935  sawa na asilimia 58.46.

Kutokana na hali hiyo alisema ataendelea kuipinga Serikali hadi pale watakapoelewana.

Bila kusema ni mbinu gani atatumia kutimiza azma hiyo, alisema kila kitu kitaonekana muda utakapofika kwani hawezi kutoa silaha zake zote kabla ya vita.

Pia waandishi walipotaka kujua endapo wabunge wanaotokana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) watahudhuria siku Dk. Magufuli atakapohutubia Bunge, alisema. ‘tutavuka daraka tukilifikia’ akimaanisha kuwa kitu kitakachofanywa na wabunge wa Ukawa kitaonekana siku hiyo.

Alisema Ukawa, utaendelea kuwataka Watanzania wakatae matokeo batili ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania bara na kuendelea kuwa watulivu.

Alisema umoja huo una ushahidi wa kutosha kuonyesha jinsi matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano yalivyochakachuliwa na kiasi cha kura zilizoibwa.

“Wakati mwafaka tutaweka bayana ushahidi huo ili Watanzania wajue kwa nini Ukawa inasema kwa dhati kuwa haitambui matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi na kwa nini haitashirikiana na Serikali ya sasa ambayo ni batili kisheria.

“Kama sheria ingeturuhusu tungekuwa mahakamani kupinga uamuzi wa Tume ya Uchaguzi. Uamuzi huo umetekelezwa tu kwa sababu ya fitna ya sheria mbovu zilizotungwa kuhakikisha CCM inabaki madarakani milele. Hii lazma tuendelee kuikataa na kuipinga kwa nguvu zetu zote.
“…Ukawa itaendeleza harakati za kisiasa katika nyanja mbalimbali ili kutekeleza azma ya kuleta mabadiliko ya kweli nchini,” alisema Lowassa wakati akisoma tamko la umoja huo.

Alisema umoja huo utaendelea pia kudai Katiba ya wananchi itakayohakikisha kuwa Tanzania inakuwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Serikali inayowajibika kwa umma.

“Ni wazi kuwa uchaguzi mwingine katika mazingira ya sasa na chini ya Katiba ya sasa hauwezi kuzaa matunda tofauti. Bila Katiba mpya ya wananchi, Tanzania haitakuwa na demokrasia na itaendelea kuwa nchi inayotawaliwa kwa mizengwe na udikteta wa CCM,” alisema.

Mustakabili wa Zanzibar

Lowassa pia alizungumzia hali ya mambo visiwani Zanzibar hasa baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi.

Suala hilo ndilo lilikuwa ajenda kubwa ya mkutano huo na waandishi wa habari,  ambapo Lowassa alisema. “Wakuu wa Ukawa kwa kauli moja walikariri tamko lao la kumuunga mkono  kwa dhati Maalim Seif Sharif Hamad kwa ushindi wake dhahiri na kuitaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar imtangaze kuwa Rais wa Zanzibar mara moja,” alisema.

Alisema katika mkutano wa viongozi hao uliofanyika Novemba 9, mwaka huu jijini Dar es Salaam, walilaani vikali uamuzi wa ZEC kufuta uchaguzi halali na kuonya mbinu mpya za kutaka uchaguzi urudiwe hazikubaliki na zitahatarisha amani na utulivu wa Zanzibar.

“Viongozi wa Ukawa walimpongeza Maalim Seif na viongozi wote wa CUF Zanzibar kwa busara na ustahimilivu wao mkubwa na jitihada zao zinazoendelea kulinda amani,”alisema Lowassa.

Alisema kinyume na Tanzania bara, uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa wa wazi na wa amani kwani vyama vyote vya siasa na hata wawakilishi wa kimataifa walikiri hivyo mpaka pale ilipobainika CCM inashindwa.

“Wakuu wa Ukawa walikataa dhana kuwa uchaguzi ule ule unaodaiwa kufutwa kwa kuwa ulikuwa na mizengwe, ulizaa matokeo halali kwa wabunge Bunge la Jamhuri ya Muungano na urais wa jamhuri, lakini batili kwa wajumbe la Baraza la Wawakilishi na Rais wa Zanzibar. Dhana hii haina mantiki yoyote bali ni ubabe wa kisiasa tu.

“Haiwezekani chungu kimoja kikapika halali na haramu kwa pamoja.  Kwa kigezo cha ZEC kuwa uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa batili basi matokeo yake yote ikiwa ni pamoja na yale ya Rais wa Jamhuri ya Muungano pia ni batili.

“Hii ina maana kuwa hata ushindi unaodaiwa na Dk. Magufuli, mbali ya kuwa ni matokeo haramu ya wizi kwa kura za Tanzania bara, pia ni batili kisheria kwani hana ridhaa ya watu wa pande zote mbili za Muungano,” alisema Lowassa.

Hali ya nchi

Akizungumzia hali ya nchi, Lowassa alisema viongozi wa Ukawa walikubaliana kwa kubaini kuwa hali si shwari nchini licha ya ukimya wa wananchi.

“Wananchi wanaelewa fika kuwa CCM na Serikali yake wamepora ushindi wao na sasa inaendelea kushinikiza kwa vitisho vya majeshi yenye silaha yanayoranda mitaani ili matokeo ya wizi huo wa waziwazi yakubalike,” alisema.

Alisema  CCM na Serikali yake wanajua haikubaliki na hata ifanye vipi haiwezi kushinikiza nafsi za Watanzania.
“Kama CCM inadai kuwa imeshinda kwa nini ihitaji majeshi, magari ya washawasha na silaha za vita ili wakubalike?

“CCM ilitayarisha mkakati wa kuhujumu uchaguzi na ndiyo maana ikanunua magari, na vifaa vya vita kwa mabilioni ya fedha ili kuutisha umma wakati wananchi wanakufa kwa kukosa dawa hospitalini.

“Kama CCM inadai imeshinda kwa nini wana hofu kubwa mpaka kuhujumu uhuru wa vyombo vya habari, kupiga marufuku mikutano ya kisiasa na kutunyima viongozi wa Ukawa hata fursa ya kuwashukuru Wananchi kwa kutuunga mkono katika safari yetu ya kuleta mabadiliko? hii ni aibu kwa Taifa letu,” alisema Lowassa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles