25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa pasua kichwa

Lazaro-Nyalandu1Na Absalom Kibanda, Dar es salaam

SASA ni bayana kwamba tumeingia kwa kishindo mwaka wa Uchaguzi Mkuu ambao Watanzania tunaratajia kupata safu mpya ya viongozi wa kisiasa na wa kiserikali watakaoliongoza taifa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Kauli za kushtusha, kushangaza, za maana na za kipuuzi zimeanza kusikika kutoka katika kila kona ya taifa hili zote zikigusia kwa namna moja au nyingine kile ambacho kinaweza kikabadili mwelekeo wa siasa za Tanzania kwa miaka mingi ijayo.bTumewasikia maaskofu, manabii,
wachungaji na mapadri wakiusemea mwaka huu. Tumewaona na kuwasikia viongozi wakuu na wajuu kimamlaka, wanasiasa, wanajimu na vigogo wastaafu wakiuzungumzia mwaka huu kwa muktadha ule ule wa uchaguzi mkuu.
Wote hao kwa staili na kwa namna tofauti, wametoa kauli nzito na wakati mwingine nyepesi na za hovyo kueleza kile ambacho kwa maono na maoni yao, wanakiona kuwa ndichokitakachotokea mwaka huu. Kwa bahati njema au mbaya, nyakati nyingine kauli hizo za kinabii, kishabiki, kinajimu au kichambuzi zimebeba jumbe zinazofikirisha, kufurahisha, kuchekesha na si ajabu kuudhi, kufedhehesha na kukasirisha. Niliseme hili mapema kabisa
na pasipo kumung’unya maneno kwamba, nikiwa mdadisi mkubwa wa masuala ya siasa na uongozi wa taifa hili, mimi ni mmoja wa watu ambao wameguswa kwa namna na kwa njia tofauti na kauli hizo.
Nikiwa mmoja wa Watanzania mwenye maono, matamanio na pengine malengo na makusudi mema kwa taifa langu nimeona nitakuwa sijaitendea haki nafsi yangu iwapo nitaamua kukaa kimya pasipo kueleza lolote na kisha nikasubiri hadi mambo yaharibike kabisa ndipo niwe na la kusema.
Nitakuwa nikiukatili utashi wangu kifikra iwapo nitakaa kimya na ama
kuzipuuza, kuzilaani au kuzibariki kauli kama zile zilizotolewa na akina
Lazaro Nyalandu na baba yake wakiroho, Mtume na Nabii Josephat Mwingira usiku wa kuamkia mwaka mpya. Kwamba Nyalandu, Waziri wa
Maliasili na Utalii, amefikia hatua na kupata jeuri ya kutoa mwaliko mahususi kwa kwaya ya Kanisa la Efatha eti kwenda Ikulu Novemba
mwaka huu na kutumbuiza siku atakayokuwa akiapishwa kuwa Rais wa tano wa Tanzania si kauli ya kuachwa hivi hivi pasipo kuipigia mstari mwekundu.
Si hilo tu, nitakuwa na roho ya Tomaso, yule mwanafunzi wa Yesu aliyekosa imani kwamba Kristo alikuwa ameshinda mauti kaburini na kufufuka, iwapo nitajifanya kutohoji mantiki ya kiroho na kisiasa ya kauli ya Mtume na Nabii Mwingira aliyemtangazia ukuu Nyalandu ‘live’ usiku ule ule wa mapatano yao.
Katika mazingira ambayo taarifa zinasema maono ya Mtume Mwingira yanapingana na ya wachungaji wake watatu ambao wao kila mmoja kwa
wakati wake wanadai kuonyeshwa jina la mwanasiasa mwingine tofauti na
Nyalandu kushinda urais wa Tanzania, mara moja naona halitakuwa jambo sahihi kunyamaza pasipo kuzitafakari na kuzichanganua kama si kuzijaribu roho zilizobeba unabii wa namna hiyo. Kama hiyo haitoshi, nitakuwa mtu wa hovyo iwapo nitafumbia jicho na kujifanya kutoijali kauli ya askofu mmoja wa kule Mbeya aliyewataka wanasiasa kuacha kujisumbua na urais wa mwaka huu wakati maono aliyonayo yanaonyesha tayari jina la mtu atakayerithi mikoba ya Rais Jakaya Kikwete.
Katika hili la askofu wa Mbeya, najiona nikiwiwa kuwakumbusha Watanzania wenzangu waliomsikia askofu huyo au wakasimuliwa taarifa na habari zake kurejea kauli zilizotolewa na maaskofu wa namna hiyo hiyo mwaka 2005 walipojiingiza katika siasa hata kututamkia kwamba mgombea fulani eti ni chaguo la Mungu. Kwa lengo hilo hilo la kuweka kumbukumbu sawa pasipo kubishana na maono hayo ya kitume na kichungaji, mguso ninaoupata katika hayo si kuwatilia shaka watumishi wa
kiroho wa aina ya Mwingira na askofu yule wa Mbeya bali kuuliza sababu zinazomfanya Mungu akaendelea kuruhusu balaa la kiuongozi katika taifa letu.
Ninalazimika kulihoji hili wakati nami nikimpigia magoti Mungu ninayemuabudu kuisadia Tanzania impate rais mwenye roho ya Farao wa
Misri wa zama za Mussa au Herode na Pilato wa enzi za Yesu ambao wote pia naamini walikuwa chaguo la Mungu ambalo kusudi lake lilikuwa ni
kuwafundisha watu fulani fulani kwa njia ya viboko. Sidhani wala sitaki kuamini kwamba, Watanzania tumefikia hatua ya kuwa na roho za uasi na maovu kwa kiwango cha kumfanya Mungu atuzire hata akaruhusu tumpate rais na viongozi wengine ili tuendelee kuteseka, kuishi kwa mashaka, tabu na umasikini.
Naandika haya huku kumbukumbu zangu zikiyatafakari maneno makali ya Nabii Mwingira siku ile ile alipomtia wakfu wa ukuu’ Nyalandu na kutamka kwamba matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu yatahitimisha zama za utawala wa mapepo na majini kwa taifa. Hili nawaachia Watanzania kulipima wao wenyewe.
Katika misingi hiyo hiyo, nitakuwa sijatenda haki iwapo nitakaa kimya na kujifanya kutozisikia kauli kama zile za kinajimu na kitabiri za akina Hassan Hussein Yahya na Sheikh Sharif ambao nao kwa njia tofauti wametabiri kuhusu urais na uongozi ujao wa Tanzania baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu. Kwa uzito mkubwa zaidi, nafsi yangu itanisuta iwapo nitajifanya kusahau ukubwa wa majeraha na ulemavu nilioupata takriban miaka miwili iliyopita kwa sababu hizi hizi za siasa
za wakubwa, iwapo nitalifumba jicho langu na kuiacha kauli nzito ya Waziri
Mkuu, Mizengo Kayanza Peter Pinda kuhusu safari yake ya kusaka urais wa
2015 ikipita pasipo kuichambua. Lakini pengine nitakuwa mpuuzi
kweli kweli iwapo nitajifanya hamnazo na kujifikisha katika hatua ya ama kuzishabikia au kuzipuuza propaganda za urais wa baada ya Kikwete zilizofinyangwa kwa ufundi mkubwa na kwa malengo mahususi na bingwa wa siasa za kikachero, Bernard Kamilius Membe.
Katika hili la Membe mwenye hulka ya kusuta wengine alionao katika boti aliyoipanda ‘CCM’ yako mengi yanayofikirisha, kuvutia, kushangaza, kustaajabisha na kupuuzwa ambayo yumkini yanahitaji kurasa kadhaa
kuyachambua. Moja rahisi kabisa ni kwamba, hata baada ya kuonywa na chama chake na kuwa kifungoni, Membe amejikuta akirejea kanisani na kuzungumzia siasa na baya zaidi na tena mbele ya makasisi akatoa hukumu kwa wengine, akajitangazia haki, akajikuza mwenyewe na kujisifia kwa usafi kwa staili ile ile waliyofanya mafarisayo zama za Yesu.
Sina hakika Philip Mangula na Abdulrahman Kinana wataliangaliaje hili la Membe mwezi ujao, wakati wakichambua na kupitia adhabu ambazo CCM ilizitoa kwa vinara sita wa urais waliotuhumiwa pamoja na mambo mengine kwa makosa ya kuanza harakati za urais mapema huku baadhi yao wakihusishwa kujijenga kwa kutumia nyumba za Ibada. Katika hili Membe kama ilivyo kwa Pinda ana bahati moja kubwa kwamba, haangaliwi kwa jicho la husuda na chuki na vigogo wanaokiongoza chama hicho kama ilivyo kwa mtu ambaye yeye (Membe) anamuona kuwa adui na mshindani wake mkubwa, Edward Lowassa.
Ninahitaji muda, fursa na nafasi ya kutosha kulijadili kwa kituo hili na hivyo naamini wasomaji na Watanzania wenzangu watanipa fursa kuendelea na mada hii wiki ijayo na kuingia kwa undani kulisemea hili.
Kwa mwelekeo huo huo, ninahisi nitakuwa nimejidhulumu fursa ya kutafakari kwa kina hali ya hewa kisiasa iwapo nitaziweka kapuni kauli
nzito kama zile zilizotolewa za Mzee wetu, Cleopa David Msuya na kabla
yake, Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Mzee Philip Mangula ambao
wote kila mmoja kwa wakati wake amezungumzia safari hiyo hiyo ya urais
wa mwaka huu 2015. Nitakuwa sijatenda haki kwangu na kwa wengi wengine iwapo, mada hii nitaihitimisha huko tuendako pasipo kudurusu fikra za ujana na zenye matarajio makubwa zilizobebwa na kauli za juzi na zile za awali za mwanasiasa kijana, mbunifu na mwenye mshawasha mkubwa wa urais na uongozi, Januari Makamba. Rejeo na mapitio ya kauli zote hizo ambazo nakusudia kuziweka katika chekeche la mchujo ninaokusudia kuubebesha maono na maoni yangu halisi, sambamba na matamanio mema kwa taifa langu, yanaweza yakachukua muda kidogo kuyahitimisha na pengine hata nikalazimika kuifanya mada hii ikaendelea katika matoleo mawili au matatu ya gazeti hili la RAI.
Nikirejea kauli za Mtume Mwingira, moja kwa moja najikuta nikiingia
katika maandiko matakatifu ambako naamini mtumishi huyo wa Mungu
anao ufahamu mkubwa usioweza ukatiliwa shaka na mtu wa kariba yangu niliye nje na kando ya mimbari na madhabahu. Kauli ya Mtume Mwingira
kwamba Nyalandu anatabiriwa ukuu, imenifikirisha sana kwa kiwango cha
kunichukua hadi kwa Mtume Paulo wa ndani ya Biblia ambaye mapenzi yangu makubwa kwake yalijengwa na namna alivyofundisha katika msingi wa kubainisha tofauti kati ya maoni yake binafsi na maagizo ya Mungu.
Kwa maoni yangu Mtume Paulo alikuwa mwerevu kila alipokuwa akihubiri na kusema maoni yake kuwaeleza waliokuwa wakimsikiliza akisema hapo nasema mimi si Bwana (Mungu) na katika sehemu nyingine akasema ‘hapo asema Bwana (Mungu).
Nilitarajia kumsikia Mwingira akitoa ufafanuzi wa maono yake juu ya ukuu wa Nyalandu kwa waumini na wasikilizaji wake, iwapo kile alichomtamkia kilikuwa kikitoka kwake au alikuwa akikisema Mungu kwa kinywa chake (yeye Mtume Mwingira). Kwamba Nyalandu ambaye sasa ni Waziri wa Maliasili na Utalii kwa maono au maoni ya Mwingira atapata ukuu sawa sawa na matamanio aliyonayo au zilivyo ndoto zake? Basi hili ni suala la kusubiri wakati utakapofika.
Unabii huo wa Mwingira ukichanganya na ujasiri wa Nyalandu mwenyewe aliyefikia hatua ya kutoa mwaliko kwa kwaya ya kanisa hilo siku ya kuapishwa kwake kuwa Rais wa Tanzania Novemba mwaka huu hata kabla mchujo wa wagombea urais haujaanza achilia mbali kufanyika, ni moja ya mambo ya kustaajabisha na kushangaza.
Nilipolisikia hili likitoka kinywani kwa Nyalandu, nililazimika kujiuliza mara mbili mbili iwapo Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ulikuwa umetuandalia muujiza wa urais unaomhusu mwanasiasa huyo mchanga na
mwenye rekodi ya kutiliwa shaka. Silioni hili likitokea japo kwa Oktoba/ Novemba mwaka huu. Wakati nikistaajabishwa na yale ya Mtume na Nabii Mwingira na Nyalandu kwa mfano wa kujiona nikiota ndoto ya alinacha, siku moja au mbili tena baadaye nikakutana na kauli ya kutia shaka kutoka kwa Waziri Mkuu, Pinda.
Nikiwa mdadisi wa masuala ya siasa, mwandishi wa habari wa umri wa kati
na mfuatiliaji wa karibu wa masuala ya siasa, wanasiasa na wapambe wao kazi ya kuyapima maneno ya Pinda, ukweli na uhalisia wake naiachia Kamati za Maadili za Chama Cha Mapinduzi (CCM), hekima ya Rais Kikwete, wana CCM wenzake na taasisi za dola. Nalisema hili kwa uwazi kabisa kwamba, timu ya wapambe wanaotamba kumuunga mkono Pinda ambao baadhi yao baaada ya kuwasikia kwa muda mrefu juzi tu hapa walionyeshwa katika mkanda moja mfupi wa video unaosambazwa
mitandaoni ukionyesha wakiwa na waziri mkuu inaundwa na watu wenye
rekodi ya matumizi makubwa ya fedha. Wakati Pinda akitoa kauli hiyo, kwa maoni yangu alipaswa kuwakana pia vijana na makada wengine wa CCM wanaopita mikoani na wilayani wakishawishi wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na wale wa Mkutano Mkuu wa chama hicho kumuunga mkono wakitumia fedha kama wanavyofanya kwa wagombea takriban wote wa chama hicho.
Sitaki kuamini kabisa kwamba, Pinda kama ilivyo kwa vinara wa urais wa CCM halijui hili au amefikia hatua ya kusahau kabisa kuwa wanachama
wenzake wengine sita wako katika uangalizi kwa makosa hayo hayo. Lakini huenda katika hili inawezekana yakawa ni makosa kumsema Pinda wakati tukijua fika kwamba uongozi wa juu wa CCM ndiyo uliokuwa na wajibu wa kulichunguza na kulitolea kauli na uamuzi.
Badala yake Makamu Mwenyekiti wa Taifa, Mangula na Kamati zake za maadili katika hili wanaonekana kumgwaya Pinda kama wanavyowafumbia macho wengine kadhaa na wao kuelekeza macho yao yote kwa mtu mmoja tu anayeitwa Lowassa. Tuombe uzima na kukutana
wiki ijayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles