24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Pinda akana kulialia

Waziri Mkuu Mizengo Pinda
Waziri Mkuu Mizengo Pinda

Na Walter Mguluchuma, Katavi
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amesema yeye si kiongozi wa kulialia jambo ambalo linamfanya ashindwe kutoa maamuzi mbalimbali ya Serikali kama watu wengi wanavyodai.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Shule ya Msingi Kashaulili mjini Mpanda, Pinda alisema kumekuwapo na watu wengi wanaobeza uwezo wake wa kiutendaji.
“Kumekuwa na baadhi ya watu ambao wamekuwa wakibeza mimi sifai kuwa kiongozi kwa vile nashindwa kutoa uamuzi mbalimbali katika mambo yanayohusu Serikali na ninapokuwa bungeni eti nalia,” alisema Pinda.
Alisema uvumi huo hauna ukweli wowote juu ya utendaji wake wa shughuli za Serikali, kwani amekuwa akitoa uamuzi pale ambapo anahitajika kufanya hivyo.
“Nataka wananchi wa Tanzania wanielewe, nimekuwa nikitoa uamuzi mwingi wa bila kutangaza kwenye vyombo vya habari, huwa sipendi kufanya hivyo kwa sababu si kila jambo lazima litangazwe,” alisema.
Alisema kama angekuwa hana uamuzi, nchi isingepiga hatua yoyote ya maendeleo na kuwa na heshima kubwa ndani na nje.
“Nimekuwa nikiwaita na kuwakemea baadhi ya mawaziri pale ninapoona mambo hayaendi sawa sawa, hata kwenye wizara zao wanazofanya mara nyingine nimekuwa nikishauriana nao,” alisema.
Pinda alisema pia wako baadhi ya watu wanamzushia kuwa ana mali nyingi wakati sio kweli, kwani nyumba yake iliyopo Mtaa wa Makanyagio mjini Mpanda na makazi yake ya Kibaoni ni ya kawaida tu.
Januari 2009, Waziri Mkuu Pinda alitoa machozi bungeni wakati akijibu swali la aliyekuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Hamad Rashid Mohamed, aliyemtaka aeleze sababu zilizomfanya atoe kauli ya watu wanaowaua maalbino nao pia wauawe alipokuwa ziarani katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Kutokana na kauli hiyo, kambi ya upinzani ilitoa tamko mbele ya waandishi wa habari ikimtaka Pinda aachie ngazi kwa madai kwamba anapingana na utawala bora wa kisheria.
“Kwa mtu ambaye hajapata nafasi ya kukutana nao (albino) na wakamweleza wanayoyapata…(sauti yake ikabadilika ghafla na kutokwa na machozi), wauaji hawa hawawezi kuvumiliwa. Katika mazingira kama haya, Watanzania hatutakuwa tayari kuwavumilia wauaji hao,” alisema Pinda kwa sauti ya huruma bungeni wakati akielezea adha wanazozipata albino.
Mwaka 2013, Pinda alisema uwaziri mkuu ni mzigo kama msalaba na ikiwa ataondolewa, atafurahi kwa kuwa atapumzika.
Alitoa kauli hiyo bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Kassim Mohamed (CUF), katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo.
“Rais akiniambia nimeshindwa majukumu nitaondoka, huku nikiwa na kicheko, hata ninyi wabunge mna nafasi ya kuniondoa, mnaweza kufanya hivyo mkiona inafaa kwani nitafurahi na kupumzika,” alisema.
Rukia katika swali lake, alimtaka Pinda kutoa ufafanuzi kuhusu kauli za wabunge wa CCM kuwa yeye ndiye mzigo.
Pinda alisema licha ya jitihada anazofanya kutekeleza wajibu wake kwa kusimamia wizara 20, anashangaa kuhukumiwa kwa upungufu unaotokea katika wizara moja au mbili.
Alisema anasimamia wizara kama 20 na zote zinafanya kazi vizuri, lakini kama kuna wizara moja au mbili hazijafanya vizuri sana, hiyo haitoshi kudai atimuliwe kazi.
Pinda alisema uzuri wa nafasi ya uwaziri mkuu, mtu haombi, bali anateuliwa na rais kwa majaaliwa ya Mwenyezi Mungu, hivyo isipompendeza, ni kazi rahisi kwa rais ambaye atamwambia kuwa ameshindwa jukumu lake na kumwondoa.
“Bunge pia mnaweza kumwondoa Waziri Mkuu kwa uwezo wenu, hivyo dada Rukia kama unafikiri hilo na wabunge wote wakaona sawa, nipo tayari, tena nitafurahi kweli kweli angalau nimeutua msalaba huu, mana’ke hii kazi ni ngumu,” alisema.
Katika swali la msingi, Mbunge huyo alitaka kujua kauli ya Waziri Mkuu iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kuwa kuna baadhi ya mawaziri ni mizigo alipokuwa katika ziara yake mkoani Mbeya.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema hata yeye alisikia kauli hiyo kwenye vyombo vya habari akasema ni vema kumsubiri Kinana arudi kutoka katika ziara na kumsikiliza alichosema alikuwa na nia gani, ndipo wataona namna ya kwenda mbele zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles