LOWASSA AKIPIGWA NYUMBANI TUTAMPOTEZA

0
1038

Na CHARLES MULLINDA


KWA mara nyingine tena, Edward Lowassa na jeshi lake la upinzani, yuko vitani akipigana na Jeshi la Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwania umiliki wa Jimbo la Monduli, mkoani Arusha.

Katika vita hii, Lowassa, mwanasiasa mwenye ushawishi, mvuto na nguvu za kisiasa analiongoza jeshi lake kupigana na jeshi la mahasimu wake katika uwanja mdogo wa vita ulio nyumbani kwao Monduli. Ameapa kupigana kufa au kupona kutetea ngome yake ya mwisho isitekwe na wapiganaji wa CCM.

Ninaamini Lowassa hakupenda wala hakuwa na dhamira ya kupigana vita hii bali amelazimika kwa sababu ana wajibu wa kuipigania ngome yake kuu ya kisiasa, Monduli.

Ila, ningepata wasaa wa kumshauri kabla hajaingia vitani ningemwambia akimbie, aiache Monduli itwaliwe kwa amani na adui zake ili baadaye akiwa amejiimarisha vizuri arejee vitani kuikomboa.

Ningemshauri hivyo kwa sababu ni wazi hajaimarika kiasi cha kutosha kurudi vitani baada ya kujeruhiwa vibaya katika vita vya 2015 na kama atapigwa, akipigwa katika vita hii, akipigiwa nyumbani kwake Monduli, utakuwa ndiyo mwisho wake, atapotea.

Hatakuwa na uwezo wa kuikomboa tena Monduli na nadhani ndiyo maana ameapa kupigana kufa au kupona, ameapa kufia Monduli. Anajua hii ndiyo vita yake ya mwisho hivyo ni ama apotee kabisa au aendelee kuwapo.

Hata hivyo kiapo cha Lowassa ni cha kishujaa. Kwa mpiganaji yeyote wa aina yake anayejua umuhimu wa kuilinda ngome yake ya mwisho isiangukie mikononi mwa adui ni lazima aape kufa kishujaa.

Wapiganaji wake – watiifu na wasaliti – walioko uwanja wa vita Monduli wamejawa mori ya mapambano kwa tamko lake kuwa hatishwi na wingi wa wapiganaji 16 hodari wa CCM waliopelekwa kupambana naye.

Kwamba hata kama adui yake CCM ataongeza idadi ya wapiganaji hadi kufikia 100, hawatafua dafu mbele yake. Wasahau kuiteka ngome yake ya Monduli. Hili nalo ni tamko la mpiganaji shupavu.

Katika vita hii ya uchaguzi mdogo wa Mbunge wa Monduli, Lowassa ni lazima ashinde ingawa dalili hizo hazipo. Nasisitiza akishindwa, akipigiwa nyumbani, adui zake wataiteka Monduli na kusimika utawala wao. Watawateka wafuasi, mashabiki na ndugu zake. Lowassa atakuwa ameteketezwa. Tutampoteza.

Lowassa analazimika kushinda vita hii kwa sababu anapigana akiwa na kumbukumbu ya kupigwa vibaya katika vita ya kihistoria ya mwaka 2015 iliyopiganwa kwa siku 64 baina ya majeshi yake ya muungano wa upinzani dhidi ya wapiganaji wenye ujuzi na uzoefu wa vita vya kisiasa vya hovyo na kistaarabu wa CCM. Ni matarajio ya wengi kuwa hatorudia makosa yaliyomgharimu katika vita hiyo.

Tathmini niliyoitoa mwaka 2016 kuhusu mwenendo wa vita ya uchaguzi mkuu wa mwishoni mwa 2015 baada ya majeshi ya Rais Pombe Magufuli kuyaangamiza ya Lowassa, nilieleza jinsi ilivyokuwa ngumu na ilivyogharimu uhai wa wanajeshi wa vyama hivyo viwili na raia na jinsi wapiganaji wa pande hizo mbili walivyotumia silaha za kisasa na za kale kushambuliana na kujihami.

Nilieleza kinaga ubaga jinsi silaha nzito nzito zilizotengenezwa kienyeji za aina ya matusi, kashfa, kuchafuana, kuibiana mbinu za kampeni, kumwagiana tindikali, kuzidisha muda wa kufanya kampeni, uwezo wa ushawishi wa kisiasa na kujenga hoja na hata kuwindana kwa lengo la kunyamazishana milele zilivyovurumishwa na majeshi ya pande zote mbili.

Silaha hizo bado zipo na zinaendelea kutumika vitani Monduli.

Makosa yaliyofanywa na Lowassa mwenyewe katika vita ile ndiyo yaliyowawezesha wapiganaji wa CCM kuwachakaza wapinzani wao ndani na nje ya uwanja wa vita.

Lowassa aliponzwa na brigedi yake ya propaganda iliyokuwa na wanahabari wasomi ambao hawakuelemika. Aliponzwa na utitiri wa wapiganaji waliokuwa na uchu wa madaraka kuliko tamaa ya utumishi, uzalendo na maendeleo ya taifa.

Alikosea kuvaa ngozi ya kondoo wakati kiuhalisia alikuwa chui aliyejichanganya katika kundi la kondoo huku kondoo wakijua yeye ni chui anayewawinda hivyo wakakaa naye kwa tahadhari na hata alipotaka kuanza kuwaangamiza mmoja baada ya mwingine hakufanikiwa, walikwepa mashambulizi yake.

Ndiyo maana halikuwa jambo la ajabu jina lake lilipokatwa mapema miongoni mwa wagombea urais ndani ya CCM na baadhi ya wafuasi wake kumkimbia wakaenda kujiunga na adui, wakapambana naye majukwaani na kufanikisha ushindi wa wale aliokuwa akipambana nao.

Wakatawazwa kuwa viongozi wa kisiasa katika maeneo mbalimbali nchini na ni hao hao ambao sasa wanapambana naye wakikisaidia CCM kuiteka ngome yake muhimu ya Monduli.

Kosa jingine alilolifanya Lowassa katika vita ile ni kujiunga na jeshi la upinzani lisilokuwa na wapiganaji watiifu kwa makamanda wao. Jeshi lenye makamanda wanaohubiri wasichokiamini na kutenda wasiyopenda kutendewa hivyo haikuwa ajabu kwa wananchi kukataa kutawaliwa na jeshi lisilokuwa na mwelekeo.

Jeshi la Lowasssa katika vita ya 2015 lilikuwa na wapiganaji mabingwa wa kueneza sumu lakini wasiokuwa na uwezo wa kupambana katika medani za vita. Kwa kiwango chake lilifanikiwa kupenyeza sumu hiyo kwa baadhi ya wapiga kura lakini lilishindwa kuilainisha mioyo ya wengi wanaoamini katika Tanzania kwanza.

Kwa mpiganaji wa aina ya Lowassa, haina shaka alijifunza mengi katika vita ile na hasa jinsi wapiganaji wake waliopata vilema vitani walivyomkimbia na wanavyoendelea kumkimbia kwenda kujisalimisha kwa wapinzani wake na kuwa viongozi wa kuimba pambio la ‘Hapa kazi tu’

Sitarajii kuwa Lowassa atakuwa ameingia katika vita ya kuipigania kambi yake ya Monduli bila kujua kuwa wimbi la wapiganaji wake ndumilakuwili waliolemaa vitani kuendelea kumkimbia ni kubwa. Ninaamini anajua kwamba hata hao alionao sasa vitani Monduli wapo walio mbioni kumsaliti hivyo hapaswi kumwamini yeyote miongoni mwao.

Nina hakika Lowassa anapigana vita hii kuitetea ngome ya Monduli akiwa na kumbukumbu sahihi kuhusu jinsi wana mtandao wenzake walivyomtelekeza hata kulazimika kuondoka katika wadhifa wa uwaziri mkuu. Anajua kwanini aliachwa akaangamia peke yake.

Kwa tunaojua undani wa anguko lake kutoka katika uwaziri mkuu, tunaamini kila risasi anayoitupa kuelekea kwa adui zake itakuwa inamkumbusha jinsi alivyoshtakiwa mbele ya baraza la watunga sheria mwaka 2008, akasulubiwa bila huruma kisha washirika wake waliogeuka kuwa watesi wake wakampa uhuru wa kuchagua aina ya kifo cha kisiasa alichokitaka.

Anapopigana sasa atakuwa anakumbuka jinsi alivyojaribu kupambana bila mafanikio akiwa ndani ya CCM kuwania kuteuliwa kuwa mgombea urais kupitia chama hicho, lakini, licha ya kujiamini yeye mwenyewe na pia kuaminishwa na washirika wake kuwa yeye ndiye na asiyemtaka aondoke, bila kutarajia mambo yaligeuka, aliondoka yeye.

Hivyo kila anavyosonga mbele au kurudi nyuma katika mapambano ya kuipigania Monduli atakuwa anajua hatma yake ni ipi na sisi tunaoutazama mpambano baina yake na mahasimu wake tuna kila sababu ya kujiandaa kumpokea katika hali atakayokuwa nayo baada ya kumalizika kwa vita.

Kwa sababu mwenendo wa vita hii umeishatoa mwelekeo wa matokeo yatakavyokuwa; kwamba historia kwa mara nyingine ni lazima itajirudia, kama taifa moja la watu wastaarabu tujiandae kisaikolojia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here