23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

LIPUMBA: HERI JECHA KULIKO MAALIM SEIF

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM


MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba amesema ni afadhali ya Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha aliyefuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kuliko Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad aliyemuita sultan ambaye alichukua madaraka ya kujaribu kumwondoa katika wadhifa wake akashindwa.

Mwanasiasa huyo, alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja,baada ya Maalim Seif kusema bora CCM adui kuliko kukaa na Profesa Lipumba msaliti.

Profesa Lipumba ambaye pia ni msomi aliyebobea katika uchumi, aliingia katika mgogoro na CUF mwaka jana,baada ya kuandika barua ya kubatilisha uamuzi wake wa kujivua uenyekiti kwa kile alichodai nafsi yake inamsuta.

Agosti 2015, miezi michache kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu, Profesa Lipumba aliandika barua ya kujiuzulu na baadaye akaenda nje ya nchi kwa mapumziko kabla ya kurejea katikati ya mwaka jana.

Mgogoro mkubwa uliibuka siku ulipofanyika mkutano mkuu ambapo haukukubali arejee katika nafasi yake na badala yake ukakubaliana na barua yake ya kujivua uenyekiti.

Hata hivyo alipata nguvu, baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa kumtambua kuwa mwenyekiti halali wa chama hicho.

Mwanasiasa huyo mkongwe alihojiwa jana na kipindi cha 360 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Clouds cha mjini Dar es Salaam.

 “Kwa aibu iliyofanyika katika Mkutano Mkuu uliofanyika pale Blue Pearl, hata wajumbe wakaimba bora Jecha kuliko Seif, kwamba bora Jecha ambaye angalau kafuta uchaguzi ukafanyika, lakini Maalim yeye katangaza matokeo bila kura kupigwa …ilikuwa ni aibu na vurugu ikawa kubwa,”alisema.

Kutokana hilo, mtangazaji alimuliza ilikuwaje alikwenda kwenye mkutano ambao hakualikwa, alisema aliitwa na wajumbe wa mkutano mkuu baada ya kuona kinachofanyika sicho.

 “Mkutano mkuu uliitishwa,nilipokea simu kama 12 ya wajumbe wakitaka niende, huku wakieleza kuwa barua yangu, inasomwa tunaomba uje kama ndiyo uliyoiandika wewe, baadaye nilivyoona simu imezidi nikaenda na dereva wangu.

“Kufika pale, blue gard wa chama (kikosi cha ulinzi), wakanipokea nikakaa kukawa na mjadala kuwa  wajumbe wanataka mwenyekiti aje atoe maelezo, lakini Julius Mtatiro akakataa akasema Katiba hairuhusu, wakaahirisha hadi saa 12 jioni wakasema ajenda hii imefutwa sasa tunapiga kura wajumbe wakasimama lazima mwenyekiti atoe maelezo,”alisema Lipumba.

Maalim anawatisha wabunge

Alipoulizwa kuwa haoni amepoteza mvuto kwa sasa kwa sababu  kati ya wabunge 42 , wanaomuunga mkono ni wawili tu, Profesa alisema: “Tatizo la Maalim anatumia ubabe katika kuwadhibiti wabunge, wale waliokuwa na msimamo alichukua utaratibu wafukuzwe chama na wengine wameingia woga ukileta mgogoro anakushughulikia.

“Kwa mfano kabla Abdalah Mtolea (Mbunge wa Temeke), alikuja nyumbani kwangu akasema tunahitaji nikafungue kesi mkutano usifanyike sasa leo wanaona  sijui ameaminishwa kuwa ukicheza na huyu bwana utapotea ambapo huyu mwingine ni demokrasia muda wowote anaweza kukusamehe,” alisema.

Pamoja na mambo mengine, pia aliulizwa  kumekuwa na taarifa kuwa anatumiwa na CCM, madai ambayo Profesa Lipumba aliyakanusha.

“Mimi situmiwi na CCM na ndio tabia yake Maalim anapokosana na mtu anaanza kusema unatumiwa na CCM hata wakati ule wa Hamad Rashid alisema hivyo,” alisema.

Alisema hakuna mwanasiasa yeyote Tanzania Bara ambaye alipigania haki za Wanzanzibari na hata baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 kama yeye na  alivunjika mkono kwa sababu ya kuhamasisha maandamano ya CUF.

 “Kama kuna mwanasiasa Tanzania Bara ambaye amepigania haki za Wazanzibari, ni Profesa Lipumba. Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 wakati yale maandamano yanafanyika Maalim alikuwa nje ya nchi lakini mimi niliyaongoza,”alisema.

Ashangaa Maalim kumsamehe Sumaye

Profesa Lipumba, alisema Maalim Seif ana matatizo kwa kumsamehe Frederick Sumaye ambaye wakati wa maandamano ya baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 alikuwa Waziri Mkuu.

“Katika maandamano yale, watu zaidi ya 60 walipoteza maisha halafu leo Maalim anasema amemsamehe Sumaye…ana matatizo,”alisema.

Alisema msuguano wao ulianza wakati wa mchakato wa Katiba Mpya ambapo Maalim Seif alitaka wabadilishe msimamo wao wa serikali tatu, akitaka wawe na muungano wa mkataba.

“Alitaka tubadilishe msimamo wetu wa serikali tatu ili tuwe na muungano wa mkataba na miaka yote CUF imesimamia serikali tatu. Nikapeleka mapendekezo ya CUF wakaniambia mbona katibu wako ameleta muungano wa mkataba.

“Wakanihoji sasa waamue lipi ndiyo nikawaambia wasome katiba yetu, kiongozi mkuu wa chama ni mwenyekiti na kama ameleta katibu, basi ni msimamo wake binafsi,”alisema.

Kiini cha mgogoro

Akizungumzia kuhusu kiini cha mgogoro wao, alisema Maalim Seif angekuwa anaheshimu katiba ya CUF kusingekuwa na matatizo yoyote.

Alisema tatizo kubwa Maalim Seif, anataka kila kitu aamue yeye na ndio sultani wa chama kwa sababu hataki kufuata katiba.

Alipotakiwa kutoa mifano ya usultani wa Maalim Seif, alisema ni wakati alipotengua barua yake ya kujiuzulu, lakini katibu mkuu huyo akalazimisha mkutano mkuu ufanyike.

Akaulizwa ni wapi Katiba ya CUF inaposema ukijiuzulu unatengua, alisema:” Katiba ya CUF haijakataza kutengua kujiuzulu. Na si mimi tu niliyefanya hivyo, hata Ahmed Mazrui  (Naibu Katibu Mkuu) alikosana na Ismail Jusa, akaandika barua ya kujiuluzu baadaye akatengua akarudi kwenye nafasi yake,”alisema.

Mtangazaji pia alimwuliza kuwa hakuna sehemu ndani ya katiba yao kwamba baada ya kujiuzulu asubiri baada ya muda fulani, alisema kwa mujibu wa katiba, kujiuzulu hakutakamilika mpaka mamlaka iliyomchagua ikubali kujiuzulu kwake.

Sababu za kujiuzulu

Alisema alijiuzulu baada ya kukosekana umoja kwa sababu awali walikuwa wamekubaliana na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willbroad Slaa awe mgombea urais wa Ukawa, lakini baadaye wakamleta Edward Lowassa.

“Katibu mkuu aliitisha kikao baada ya kushauriana na Freeman Mbowe (mwenyekiti), nimejikuta nikawa na wakati mgumu kulinda masilahi ya chama na wananchi kwa ujumla ukosefu wa umoja ulitumiwa na Chadema kutugawa na kudhalilisha viongozi wa CUF Bara, kwamba hatuna fedha za kuweka mgombea urais wa bara na kwamba taarifa hizi wamepewa na Maalim Seif.

“Baadaye nikamwandikia barua Maalim kuwa nimesikitika na kuhuzunishwa na hali ya kutowapo na hali ya mashauriano. Pamoja na kung’atuka kwangu awe karibu na wakurugenzi wa chama kuhakikisha tunashinda majimbo tutakayoachiwa ndani ya Ukawa,”alisema.

Kutokana na hilo, akaulizwa mpaka ametaka kurudi kwani kuna badiliko gani lililotokea sasa, Profesa Lipumba alisema: “Nilikuwa sina nia ya kurudi, uchaguzi ulipofanyika, hali ya Zanzibar matokeo yakafutwa tukawa tena hakuna lolote linalozungumzwa kuhusu uchaguzi huo.

“Nikampigia simu Maalim, nikamwambia mbona kwa kawaida baada ya uchaguzi  CUF inakuwa iko moja na sisi huku bara tunakuwa tunazungumzia, nikamwambia suala la Zanzibar lizungumzwe akasema sawa atawapanga wakurugenzi.

“Sasa kuhusu kurudi, wajumbe wa Baraza Kuu kutoka Zanzibar na Bara, wajumbe wa mkutano mkuu na wanachama wengine walikuwa wakiniomba nirudi,” alisema.

Aliulizwa kuwa sifa ya kiongozi ni msimamo na wakati anajiuzulu aliombwa lakini alisimamia msimamo wake na kwanini leo hakusimama kwenye msimamo uleule ili kuweka sawa heshima yake, alisema msimamo wake ulikuwa wazi kwa kukosekana ushirikiano.

“Sisi ambao tulikuwa tunaamini katika haki sawa kwa wote na rushwa ni adui sasa nikajikuta katika wakati mgumu kumnadi Lowassa, ukawa ni mzigo mzito hata mnyamwezi hauwezi,”alisema.

Mtangazaji akamwuliza: Unataka watu wakuelewe wakati ulipojitoa aliwaumiza wenzako? Alisema “Sio mimi wanachama wananifuata wanasema hali si nzuri,” alisema.

Alipoulizwa kuwa uhai na mustakabali wa chama ukitegemea yeye aondoke ndani ya chama atakuwa tayari, alisema suala hilo liko kwenye katiba.

Kuhusu kuitwa Ikulu

Alisema baada ya Uchaguzi Mkuu kuisha, aliitwa Ikulu na Rais Dk. John Magufuli kama mwanachama wa kawaida.

“Kikubwa alichoniambia Rais Magufuli alinieleza  kuhusu suala Zanzibar kuwa chochote watakachoamua Wazanzibari ataunga mkono, baadaye ndio nikamweleza Maalim,”alisema.

Baadaye mtangazaji aliendelea kumwuliza kuwa anaamini katika haki sawa kwa wote?

Lipumba: Naam

Swali: Sasa kwanini wewe na Dk. Slaa mkawaacha watu jangwani wakati wa vita?

Lipumba: Hakuna kwa sababu Chadema walitusaliti kwa utaratibu wa kumleta Lowassa.

Swali: Umeshawahi kwenda hija?

Lipumba: Naam, nimekwenda mara mbili

Swali: Sasa ikawaje ukaenda kuvunja ofisi ya chama?

Lipumba: Hapana sikwenda kuvunja. Tulifika ofisini na walinzi wa chama tukakuta geti limefungwa tunagonga haifunguliwi kumbe wamebadilisha walinzi wamewaleta wa kampuni ya ulinzi wana silaha. Baadaye mmoja wa wale walinzi niliokuwanao akapanda juu akafungua geti.

Swali: Nani aliyekukabidhi ofisi siku hiyo?

Lipumba: Hakuna aliyekuja kunikabidhi kwa sababu naibu katibu mkuu alikuwapo.

Swali: Ulifanya nini

Lipumba:  Niliwakaribisha wanachama na kuwaeleza tujenge umoja na tuweke mkakati mpya

Swali: Unamtambua Maalim Seif kama nani

Lipumba: Namtambua kama Katibu wa chama lakini haji ofisini nimemwandikia barua aje ofisini nimpangie kazi

Swali: Ulishawahi kukaa tawi lolote la serikali kwa siri

Lipumba: Hapana

Swali: Inapokuwa CUF ya Maalim wana vikao kunatokea vurugu, lakini kwako hakuna

Lipumba: Mimi sijui wala sielezi watu wakavamie.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles