28.6 C
Dar es Salaam
Saturday, January 28, 2023

Contact us: [email protected]

LEMA: HATUTAMUOGOPA MAGUFULI

ELIYA MBONEA NA JANETH MUSHI

-ARUSHA

MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), amewataka wananchi wa Jimbo hilo kuacha woga na waamshe mori ya kupigania haki ikiwamo kuirejesha Arusha ya Mwaka 2010.

Lema aliyasema hayo jana wakati akiwahutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Ngarenaro mjini hapa

Katika mkutano wake huo wa kwanza tangu alipotoka mahabusu ya Gereza la Kisongo alikokaa kwa miezi minne kutokana na kukosa dhamana ya kesi ya uchochezi inayomkabili, Lema alisema, umefika wakati wa kupigania haki pale inapovunjwa na viongozi akiwamo Rais John Magufuli.

“Hatutaogopa kumkosoa Rais Magufuli pale atakapokuwa amevunja Katiba ya nchi, tutasema kweli na tutapigania haki hiyo,” alisema Lema na kuongeza:

“Wananchi wa Arusha mmekuwa waoga amsheni mori ya kupigania haki. Nawaambieni hivi hakuna mtu aliyetupa nchi vizuri na kirahisi kama Rais Magufuli.

“Nawaambieni kila aliyetakiwa kukemea uovu na hakufanya hivyo ipo siku uovu huo utamrudia. Leo hii huko tunakoelekea hata hao watachoka na watarudi kuimba wimbo tunaoimba sisi,” alisema Lema.

 

Akielezea kuhusu kukaa kwake mahabusu miezi minne Lema aliyekuwa akishangiliwa kila alipozungumza alisema, wito wa uongozi na kuwatumia wananchi ndio uliomsukuma kukaa magereza.

“Nimekosa dhamana kwasababu ya wito, nisingekuwa na wito wa kuwatumikia wananchi nisingikwenda magereza. Mimi sijaingia kwenye uongozi kwa ajili ya kutafuta fedha,” alisema Lema.


MAISHA YA MAHABUSU


Akizungumzia maisha yake ya mahabusu ambako alipata cheo cha kuwa Mnyampara, alisema mahabusu si kubaya japokuwa roho inaendelea kumuuma kwa wale aliowaacha wakikabiliwa na mateso makubwa.

“Jumatano iliyopita nilirudi Magereza kutafuta ndoo yangu niliyokuwa nakalia nilienda kuichukua na kuiweka chumbani kwangu. Mke wangu aliniuliza nikamjibu kuwa wapo watu wengi walioonewa hivyo kila ninapokuwa nikiomba naiangalia ndoo ile na kuwaombea waliopo magereza.”

"Nimekaa mahabusu miezi minne sina kosa kabisa,nilichukuliwa Dodoma na Polisi usiku nikapelekwa Kondoa, katikati ya njia nikaomba kujisaidia haja ndogo polisi wakanizunguka na silaha za SMG 5 niliwauliza mnanitafuta mimi ama kuna mwingine mnamtafuta niliwaambia kama kuna kitu nimeshau kwenye maisha yangu ni hofu na woga,"

 “Tuliingia Arusha Saa 12 asubuhi nikasikia Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) akipigiwa simu na kutoa maelekezo mtu yeyote asinione, nimeanza kukaa mahabusu tangu Mwaka 2004. Lakini nikafikiria nimefanya nini, kuona maono ndiyo yananitesa mimi hivi, neno la Mungu?”, alihoji Lema.


Alisema alipokuwa mahabusu alikuwa akisali na kumuuliza Mungu mbona anateswa wakati yeye ndiye alimpa kauli hiyo,Mungu akamjibu hateseki na akitoka awasamehe na wasubiri kisasi cha Mungu hivyo anasubiri kisasi cha Mungu na anatarajia kumuona Mungu.

KATIBA

Akielezea kuhusu suala la Katiba, Lema alisema Rais Dk. Magufuli akiwa anaapa aliishika pamoja na Biblia akiapa kuilinda na kuitumikia lakini hivi sasa haisimamii.


Huku akinukuu maandiko ya Biblia kutoka Kitabu cha Isaya 30:9-10; “Kwa maana watu hawa ni waasi,watoto wasemao uongo,watoto wasiotaka kuisikia sheria ya bwana,wawa ambiao waonaji,msione na manabii msitoe unabii wa mambo ya haki,tuambieni maneno laini,hubirini maneno yadanganyayo".


Alisema yeye amevaa kombati hivyo aliyosema aliona maono na badala yake watu wengine walidhani amevuta bangi. Hata hivyo kwa vile alitamka neno la Mungu na kisha kuwekwa ndani aliahidi kuendelea kujitetea kwa neno la Mungu na kuthibitisha maono yake.


POLISI

Lema aliwataka polisi kuzingataia sheria na kuacha  kuonea watu kwani wanaishi mitaani hivyo wananchi wakiamua kulipiza kisasi itakuwa jambo lisilopendeza.

Alisema anaomba Mungu hilo lisitokee  lakini ipo siku wananchi  hao watachoka na uonevu huo.

"Polisi mnaona sifa mlisema kazi ya Jamhuri ni kuona watu wanateseka ndiyo maana mnanitesa mimi,polisi hii dhuluma mnayofanya ya kudhalilisha watu, Afrika Kusini ilikuwa na polisi wabaya kuliko ninyi,hao watu mnaozuia wasifanye mkutano iko siku watakusanyika kwa njia nyingine ndiyo sababu vyama vya upinzani vikikomaa vinasaidia amani katika nchi na siyo balaa,"alisema Lema

Kuhusu mhimili wa Mahakama, Lema alishangaa mahakama za chini kutokuwa na nguvu hadi Majaji wa Mahakama ya Rufaa kuhoji kutokupewa kwake dhamana.

Pamoja na hilo alidai kuwa Rais alimteua Kaimu Jaji Mkuu ili Mahakama icheze wimbo wa serikali.

"Kama binadamu hata yeye angependa kuwa Jaji Mkuu siyo Kaimu, maana yake ni kwamba kitendo cha kumkaimisha wakati aliyekuwepo ameshastaafu maana yake ni moja Mahakama icheze wimbo wa serikali,Mahakama mnisikilize watu hawa wakikosa imani nyie watamaliza kesi zao mitaani na wakimaliza mitaani amani ya Taifa itapotea,"alisema Lema

Alisema mahakama ni  chombo muhimu kilichobaki cha kupambana na ustawi  wa amani nchini hivyo ikisimama imara Taifa litapata haki kwani Mahakama ya Tanzania huwezi kuijua mpaka utakapokuwa jela.

"Askari mmoja alisema Jamhuri imefurahi kumtesa Lema,haya mateso ni baraka,Mungu awabariki wale wote walioshiriki mpango wa  kumuweka magerereza na kuwa wamemtengeneza kuwa mbunge shupavu,wamemtengenezea thawabu ya kuwatetea wafungwa na mahabusu,"

"Wananchi wa Arusha naomba msaamaha kwa ajili ya Bunge,tumetunga sheria mbaya kuhusu maisha yenu,nilishasema kuna saa tukisha tunatunga sheria tunahisi tunatungia nyani na si watu.

“Kule ndani kuna Wakili maarufu, Median Mwale ambaye Mwaka 2010 alinifuata nijitoe nimuachie Dk. Batilda Buriani agombee kupitia CCM na anirudishie gharama zangu,

“Leo hii Wakili yule ana miaka sita mahabusu kwa kesi ya utakatishaji fedha haramu, lakini aliyebaka kosa lake lina dhamana, hizo sheria tumetunga wabunge," alisema Lema

Alisema amekutana na wafungwa wengi hivyo akienda bungeni watapeleka marekebisho ya sheria ya adhabu  kwa kuwa kazi ya serikali na magereza ni kurekebisha na magereza kumejaa watu wengi wakiwemo watoto wadogo wengine wakiwa na  umri wa miaka 14 hivyo wakiendelea kukaa kule watalawitiwa na kufanyiwa ukatili.

Aliwataka wananchi kujenga utamaduni wa kuheshimu waliowachagua (mbunge,madiwani, wenyeviti wa mitaa),wakisikia mtu amemsema kiongozi vibaya waondoke kwenye mikutano husika.

Katika mkutano huo Lema alitumia fursa hiyo pia kumshukuru na kumpongeza mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo kwa kazi nzuri ya kugawa pikipiki kipindi alichokuwa mahabusu


WAJIBU WA MAASKOFU/MASHEIKH


Lema alisema viongozi hao wa kiroho wana wajibu wa kutafuta haki na kwa Taifa hili; "Nilipokuwa magereza nilimtumia askofu wangu ujumbe kuwa nimepata maono nimeona watumishi wa Mungu,Masheikh,wachungaji, wainjilisti na maaskofu wakichomwa moto kwenye kiama nikamuuliza Mungu mbona  nawajua,Yesu akanijibu hao wana dhambi moja ya uoga.


"Hivi maaskofu na msheikh hamuoni watu wanaonewa,hamuoni Katiba inavunjwa? kanisa na msikiti likisimama imara likatoa kauli madhubuti nchi hii itabadilika hakuna kiongozi asiye na dini,watumishi wa Mungu mmepoteza mamlaka yenu mnashindwa kukemea,wananchi wanaonewa wanapiga watu bila sababu,mmefuatilia kesi yangu sheria imevunjwa lakini mmeshindwa kutoa kauli.

"Nilishasema mtu akiona uonevu unafanyika halafu asitoe kauli uonevu huo utamkuta kwa njia moja ama nyingine,warembo,matajiri, wachungaji wanatufuata kwa kuchoshwa na uovu wa CCM.

Katika hilo alimsifu Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Josephat Gwajima akisema ndiye kiongozi wa kiroho aliyebaki wengine wote wameogopa.

Kwa upande wake Msanii wa Filamu Wema Sepetu aliyeonekana kuwateka wananchi katika mkutano huo alisema amewasamehe wote waliomfanyia uovu.

“Nina amani na nafsi ya moyo kuwa mwanachama wa Chadema kwa kweli najivunia. Ninamshukuru Mungu kwa kuwatia moyo na ujasiri viongozi na wanachama wa Chadema ili waweze kuleta mabadiliko ya kweli,” alisema Wema ambaye gari lake lilizongwa na wananchi alipokuwa akiondoka uwanjani hapo.

Naye Mke wa Lema, Neema Lema aliyepewa nafasi ya kusalimia wananchi hao aliwashukuru kwa moyo wao wa kuendelea kumuamini mbunge na kumuombea alipokuwa mahabusu ya Gereza la Kisongo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles