25.3 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

MAASKOFU WANANE WAPINGA MRITHI WA MOKIWA KUSIMIKWA KESHO

Na MWANDISHI WETU

MAASKOFU wanane wa Kanisa la Anglikana nchini wamemwandikia waraka Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) Ernest Mangu, wakimwomba aingilie kati na kusitisha ibada iliyopangwa kufanywa kesho na Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dk. Jocob Chimeledya ya kumsimika mrithi wa Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam,  Askofu Dk. Valentino Mokiwa.

Hatua hiyo ya maaskofu hao imekuja wakati Kanisa hilo likiwa katikati ya mgogoro mkubwa unaotishia kulipasua msingi wake ukiwa ni uamuzi wa Askofu Chimeledya kumvua wadhifa wa uaskofu Dk. Mokiwa.

Katika waraka wao huo waliouandika Machi 8, mwaka huu baada ya kukutana maaskofu hao wameeleza kuwa wanaona hatua ya Askofu Chimeledya kufika katika Kanisa la Mtakatifu Albano kesho na kumsimika askofu mwingine anayemjua yeye kutaligawa zaidi kanisa na kuhatarisha usalama

Maaskofu  walioandika waraka huo ni pamoja na John  Lupaa wa Dayosisi ya Rift Valley (DRV), Eliasi Chakupewa wa Tabora, Boniface Kwangu wa Dayosisi  ya Viktoria Nyanza (DVN), Mathayo Kasagara wa Ziwa Rukwa (LR), Michael Afidh wa Zanzibar, Sadock Makaya wa Dayosisi ya Western Tanganyika (DWT), Maimbo  Mndolwa wa Tanga na Joseph  Mugomi wa Ruaha.

“Hivyo ili kudumisha amani na utulivu, Ibada hiyo isitishwe na dayosisi iendelee na majukumu yake hadi hapo Askofu atakapoitisha Nyumba ya Maaskofu (Baraza la Maaskofu) ambayo ndiyo yenye dhamana hiyo,” inaeleza sehemu ya waraka huo wenye kichwa cha habari ‘Mvutano wa kimadaraka katika Dayosisi ya Kanisa la Anglikana Dar es Salaam’. Unasomeka waraka huo ambao gazeti hili linao.

Pamoja na hayo, maaskofu hao wamepinga waraka ulioandikwa na Askofu Mkuu wa Anglikana, Chimeledya Februari 28, mwaka huu  kwenda kwa IGP Mangu, akiomba amzuie Askofu Valentino Leonard Mokiwa, asijishughulishe na uendeshaji wa Dayosisi hiyo kwamba ameamriwa kustaafu.

Katika hilo maaskofu hao wamesema uamuzi wa kumstaafisha Dk. Mokiwa haujathibitishwa na Nyumba ya Maaskofu (Baraza la Maaskofu).

“Na kwa kuwa tangu zuio hilo litoke waumini wa dayosisi hiyo wamekuwa wakisali kwa wasiwasi na kwa taarifa tulizozipokea kupitia vyombo vya habari zinaonyesha kuwa Askofu Mkuu amenuia kufika Kanisa Kuu la Mtakatifu Albano Jumapili Machi 12, kumsimika Kasisi kiongozi aliyemteua yeye,” unaeleza waraka huo.

Mbali na waraka huo kumpatia IGP, maaskofu hao pia wametuma nakala zake kwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Makamanda wa polisi wa mikoa ya kipolisi ya Ilala, Temeke, Kinondoni na Kigamboni.

Pamoja na hayo, maaskofu hao wametumia fursa ya kukutana kwao huko kuliomba kanisa kutafakari hali iliyonayo katika kipindi hiki.

MTANZANIA Jumamosi lilizungumza na Askofu Mugomi wa Ruaha ambaye alithibitisha waraka huo ni wao zaidi akisisitiza kuwa hawana lengo la kumtetea mtu isipokuwa kutaka utaratibu ufuatwe.

Alipoulizwa endapo IGP Mangu hatatoa ulinzi na hivyo kutoa fursa kwa Askofu Mkuu Chimeledya kumsimika Askofu mpya wa Dayosisi ya Dar es Salaam ni hatua zipi watachukua, Mugomi alisema:

“Kwanza Askofu Mkuu hatakiwi kumweka mtu, kuna mchakato, huo mchakato ndio unaobidi ufuatwe….na kuhusu ulinzi ni yeye ndiye aliyeanza kuomba sasa kwanini anaomba ulinzi ni kwa sababu mambo hayajakaa vizuri na sisi tunasema endapo IGP hatatoa ulinzi sisi hatuwezi kufanya jambo lolote la kupingana na Serikali.”

Wakati maaskofu hao wakitoa msimamo huo, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imeliandikia barua kanisa hilo ikimtaka Askofu Mokiwa kupeleka malalamiko yake katika ngazi za kanisa hilo.

Katika barua hiyo ya Machi 6, mwaka huu, kwenda kwa Askofu Mkuu Chemeledya yenye kichwa cha habari: “Yah: Kuamuru kujiuzulu na kustaafu Askofu Dk. Valentino Mokiwa wa Dayosisi ya Dar es Salaam’, inaeleza kuwa;

“Ofisi ya Katibu Mkuu imepokea barua yako na taarifa ya kina iliyoelezea historia na hatua ulizochukua kufikia kuamuru Askofu Dk. Mokiwa ajiuzulu. Ofisi ya Mhe. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi imepokea barua kutoka kwa Askofu Dk. Mokiwa akitoa malalamiko yake dhidi ya kuwepo kwa kundi la watu wanaochochea vurugu na kusababisha mgawanyiko ndani ya Dayosisi.

“Ni wazi kuwa Askofu Dk. Mokiwa hajaridhika na hali ya Dayosisi ilivyo. Kwa vile Kanisa la Anglikana na Dayosisi ya Dar es Salaam vyote vinaongozwa na Katiba tumemshauri Askofu Dk. Mokiwa kufikisha malalamiko yake kwenye ngazi zilizopo za kusikiliza malalamiko, rufaa ndani ya kanisa lenu,” inasomeka barua hiyo iliyoandikwa na kutiwa saini na M.L Komba kwa niaba ya Msajili wa vyama.

Tangu Askofu Mkuu Chimeledya atangaze kumwondoa Askofu Mokiwa, kumekuwa na matamko mbalimbali yanayopingana juu ya uamuzi huo kutoka kwa viongozi na waumini wa kanisa hilo na zaidi suala hilo likiwahi kufikishwa katika vyombo vya sheria hali inayoonyesha kuwapo kwa mpasuko. 

Wakati baadhi ya viongozi wakisisitiza kutomtambua Askofu Mokiwa wengine wamekuwa wakiibuka na kusisitiza kuwa Askofu Mkuu hana mamlaka ya kumwondoa katika wadhifa wake.

Msingi wa mgogoro huo ni agizo la  Askofu Mkuu Chimeledya kutaka Askofu Mokiwa ajiuzulu kutokana na tuhuma kumi zilizokuwa zinamkabili ambazo ni ukosefu wa maadili ikiwemo kufuja mali za kanisa na kuingia mikataba kiholela yenye viashiria vya rushwa katika maeneo ya Buza, ikiwemo pia kutoa daraja la Ushemasi, Upadre na Ukanon kwa katibu wa Dayosisi, Mkristo ambaye ametengana na mkewe na kuoa mke mwingine kiserikali kinyume na kanuni ya kanisa kuhusu ndoa.

Tuhuma hizo zilipata kujibiwa na Askofu Mokiwa mwenyewe akidai kuwa ni uzushi wenye lengo la kumchafua, lakini pia akidai zimezushwa kutokana na hofu ya uchaguzi wa Askofu Mkuu ndani ya kanisa hilo unaotarajiwa kufanyika mwakani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles