22.7 C
Dar es Salaam
Sunday, June 4, 2023

Contact us: [email protected]

Kuzuia wapinzani hakutatatua matatizo ya serikali 

manguKWA mara nyingine tena yombo vya dola, hasa Jeshi la Polisi, vimeingia katika mgogoro na vyama vya upinzani nchini. Jeshi la Polisi si tu kuwa limetangaza kupiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa, bali pia limetumia nguvu pale ambapo vyama hivyo vilikaidi agizo hilo na kutaka kufanya mikutano yao kwa sababu wanaamini kuwa wana haki ya kuifanya.

Jeshi la Polisi lilianza kuzuia mkutano wa kuchambua bajeti uliokuwa umeandaliwa na ACT-Wazalendo jijini Dar es Salaam. Likatoa askari wa kutosha kuhakikisha kuwa wanazuia mkutano huo ambao haukuwa wa hadhara, haufanyiki.

Siku chache baadaye, nguvu zikatumika kuzuia mkutano wa hadhara wa Chadema uliokuwa umepangwa kufanyika Kahama. Tukashuhudia mabomu ya machozi yakipigwa kuwatawanya watu ambao walikuwa wamekwenda kuhudhuria mkutano huo ambao ulikuwa wa amani. Baadaye Jeshi la Polisi likatoa tangazo la kuzuia mikutano yote ya vyama vya siasa. Kwanza, watu wengi walisikitishwa na hatua hii kwa sababu mikutano ya hadhara ni moja ya nyenzo zilizowekwa kisheria kwa ajili ya kuviwezesha vyama vya siasa kufanya kazi zake vema.

Kwa maana hiyo, kuzuia mikutano ya hadhara inaonekana kuwa ni moja ya njia za kuminya nafasi za vyama vya siasa kufanya kazi zao. Lakini hapa vinavyoumia zaidi ni vyama vya upinzani kwa sababu chama tawala kinaweza kuwatumia viongozi wake serikalini kama vile mawaziri kufanya mikutano na wakaruhusiwa kwa kigezo tu kuwa iliyokatazwa ni mikutano ya vyama vya siasa.

Lakini, wakati tukidhani kuwa iliyozuiwa ni mikutano ya hadhara tu, sasa tumeshuhudia hatua nyingine za kushangaza sana kwani hata mikutano ya ndani nayo inapigwa marufuku. Tumeshuhudia mahafali ya wanafunzi katika mikoa kadhaa ikizuiwa na polisi kisa tu kutoombwa kwa kibali cha kufanyika kwa shughuli hizo.

Kama kigezo ambacho Jeshi la Polisi wanataka tukiamini ni kuwepo kwa taarifa za kiitelijensia zinazoonyesha kuwepo kwa uwezekano wa uvunjifu wa amani, inashindikana vipi kuzitumia taarifa hizo kuhakikisha kuwa unawekwa ulinzi wa kutosha kuhakikisha kuwa fujo hizo hazitokei. Hakuwezi kuwepo na kisingizio kuwa hakuna askari wa kutosha au vifaa kwa sababu tumeshuhudia askari wa kutosha na vifaa vikiwepo katika harakati za kuzuia mikutano hiyo.

Na inakuwaje vigumu kwa Jeshi la Polisi lililojidhatiti na vifaa vya kisasa kushindwa kuzuia fujo katika mkutano na shughuli za ndani kama mahafali?

Ni jambo la kushangaza sana kuwa Jeshi la Polisi ambalo hivi sasa linajinasibu kuwa na vifaa vya kisasa vya kukusanya taarifa za kiintelijensia linaweza kutumia njia na mbinu za kizamani za kuzuia mikutano ya hadhara eti kwa sababu kuna hofu ya kuzuka kwa vurugu.

Lakini pale mikutano ya hadhara iliporuhusiwa, hatukushuhudia fujo wala vurugu isipokuwa katika matukio machache ambayo kimsingi Jeshi la Polisi liliingilia kati shughuli za kisiasa.

Kama kweli mikutano ya vyama vya siasa ingekuwa ni vyungu vya kupika vurugu ni dhahiri kuwa nchi hii isingetulia wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana. Kwa muda wa miezi kama miwili ambayo wanasiasa, wakubwa kwa wadogo, kutoka vyama mbalimbali, walizunguka nchi nzima kufanya kampeni kupitia mikutano ya hadhara na ya ndani, hatukushuhudia vurugu licha ya kuwepo hali iliyodhihirisha kuwa Jeshi la Polisi halikuwa na askari wa kutosha kuweza kuhakikisha ulinzi wa kutosha katika mikutano hiyo.

Kama kweli vyama vingekuwa vina nia ya kufanya vurugu, huo ndio ulikuwa wakati mzuri kufanya hivyo kwa sababu Jeshi la Polisi lilihemewa. Lakini hatukushuhudia vurugu zozote.

Kutokana na hali hiyo, ni vigumu sana kutoamini hizi tuhuma kuwa serikali inalitumia Jeshi la Polisi kwa ajili ya kukisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM) dhidi ya mashambulizi kutoka kwa vyama vya upinzani. Inakuwa vigumu kutoamini tuhuma kuwa kinachofanyika ni njama za serikali kutumia vyombo vyake vya mabavu kudhibiti upinzani nchini.

Vinginevyo, hivi mtu unawezaje kuelewa kirahisi mathalani ni vipi mkutano wa ndani wa ACT-Wazalendo kuchambua bajeti ungesababisha vurugu. Au unawezaje kuamini taarifa za kiintelijensia kuwa mahafali ya wanafunzi yanaweza kuwa chanzo cha vurugu.

Hata kama shughuli hizo zinaweza kuwa chanzo cha vurugu, Jeshi la Polisi linashindwaje kudhibiti wafuasi wa vyama vya siasa ambao wako ndani ya chumba!

Hiki kinachofanywa na Jeshi la Polisi ni kibaya sana. Inavyoonekana nguvu nyingi zinatumika kuwatisha wananchi kuwa kuunga mkono vyama vya upinzani ni kujitakia matatizo na vyombo vya mabavu vya serikali. Lakini vitisho kama hivyo haviwezi kufanya kazi vizuri katika Tanzania ya leo kwa sababu watu, si tu wanazifahamu haki zao, bali pia wanafahamu jinsi ya kuziomba au kuzidai pale inapobidi.

Inapofikia hatua vyama vinalazimika kwenda mahakamani kama ilivyofanya Chadema ili kudai haki ambayo ipo kisheria, Jeshi la Polisi lifahamu kuwa linakaribia kuwafikisha watu kwenye ukingo wa uvumilivu. Tulishuhudia Chadema ikienda mahakamani kudai haki ya kumzika kiongozi wake. Ni jambo la aibu sana kwa nchi inayodai kuwa ni ya kidemokrasia, iliyoamua kufuata mfumo wa vyama vingi, halafu chama kinalazimika kutafuta haki ya jambo dogo kama hili mahakamani.

Leo hii hii inafahamika kuwa kufanya mikutano ya hadhara ni haki ya kila chama cha siasa. Lakini kutokana na ubabe, vyama vinalazimika kwenda mahakamani kudai kitu ambacho kipo dhahiri.

Huko ndiko kuwafikisha watu kwenye ukingo wa uvumilivu. Itafika mahali watajiona kuwa ni hamnazo kwa kuendelea kutumia rasilimali zao kudai haki ambayo imeshatolewa bure. Licha ya kugharimu fedha na rasilimali nyingine, lakini kesi hizi zinagharimu muda mwingi ambao ungeweza kutumika kuleta maendeleo kwa vyama hivi na taasisi nyingine.

Pamoja na kuwa ni kazi ya Mahakama kutafsiri sheria, lakini tunapozilazimisha Mahakama kutafsiri sheria ambazo zipo dhahiri, ni kuzidharau. Pia tunazipotezea muda Mahakama hizo kuendesha mashauri mengine muhimu zaidi. Kwa upande mwingine, wapo ambao wanaweza kuona Mahakama zinatumika katika michezo ya kisiasa. Haifai kufikia hatua hiyo.

Ni kweli kuwa serikali ina matatizo mengi inayokabiliana nayo, lakini sidhani kama vyama vya upinzani ni moja ya matatizo hayo. Kinachotakiwa ni kuhakikisha kuwa vyama hivyo vinapewa uhuru na haki zao walizopewa kisheria na hiyo itaipa serikali nafasi kubwa ya kutatua matatizo yake. Kama serikali ikiendelea kuhangaika na vyama vya siasa, kamwe haitapata nafasi ya kutosha kutatua matatizo inayokabiliana nayo kwa sababu vyama hivi vipo na vitaendelea na shughuli zake hata kama Jeshi la Polisi litaongeza udhibiti wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,280FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles