23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Kutekwa kwa Mo Kazi bado nzito

Na WAANDISHI WETU


ZIKIWA zimepita siku tano tangu kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji ‘Mo’, Jeshi la Polisi limesema kazi ya kumsaka mfanyabisharahuyo imekuwa ngumu.

Limesema  linaendela na msako usiku na mchana  kuangalia njia ya kumpata mfanyabishara huyo ambaye hadi sasa  hajapatikana.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi Kanda Malumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema   kazi imeendelea kufanyika usiku na mchana lakini bado hawajafanikiwa kumpata.

“Kwa kweli bado tunaendelea na oparesheni, kazi hii ni ngumu, bado tuko kazini usiku na mchana, hatujapata ahueni hadi sasa,” alisema.

Mambosasa alisema polisi wanaendelea na kazi katika maeneo yote ambayo kwa utaalamu wanaona yanaweza kuwapa mwanga kuhusu kutekwa kwake   kuhakikisha wanampata mfanyabiashara huyo.

Dewji maarufu kama Mo, alitekwa nyara Alhamisi Oktoba 11   saa 11 alfajiri alipowasili katika kituo cha mazoezi ya viungo cha Hoteli ya Colloseum,   Masaki,   Dar es Salaam.

Taarifa za awali za Jeshi la Polisi zilieleza kuwa mashuhuda walisema watu  wawili miongoni mwa  waliomteka nyara wanaweza kuwa raia wa kigeni kwa kuwa walikuwa kama wazungu.

Kutokana na msako unaoendelea jana jioni polisi walivamia katika Msikiti wa Shia uliopo Kisutu ambako pia anasali baba wa mfanyabiashara huyo, Gullam Dewji,   kusawaka baadhi ya watu wanaohusishwa na tukio hilo kwa namna moja au nyingine.

Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, Kamanda Mambosasa alisema hana taarifa lakini huenda ni sehemu ya askari wake waliopo kazini wakiendelea na uchunguzi.

Hata hivyo alieleza kuongezeka   idadi ya watu waliokamatwa.

Alisema  usiku wa kuamkia jana walikamatwa watu wengine sita na kufanya idadi ya waliokamatwa kufikia 26 hadi sasa.

“Hadi sasa idadi ya tuliowahoji kuhusiana na kutekwa kwa mfanyabishara Mohamed Dewji imefika 26,” alisema.

Nyumbani kwa Mo

Timu ya MTANZANIA ilifika nyumbani kwa Baba mzazi wa MO, Gullamhusein Dewji kwa ajili ya kupata taarifa kuhusu kinachoendela na kukuta ulinzi wa Kampuni G1 ukiwa umeimarishwa.

Mmoja wa walinzi hao alisema shughuli zote na vikao kuhusu suala hilo vinaendelea nyumbani kwa Mo Mtaa wa Laiboni, ambako ndiko ndugu wote walipokusanyika.

Hata hivyo  ilielezwa kwamba katika eneo hilo hatakiwi mtu yeyote asiye mwanafamilia au ambaye taarifa zake au jina lake halijawasilishwa kwa walinzi.

Lakini mmoja wa walinzi hao alilieleza MTANZANIA kuwa ndani ya nyumba hiyo hakukuwa na mtu yeyote zaidi yao, kauli iliyobainika baadaye kuwa haikuwa  ya kweli.

MTANZANIA haikuweza  kumpata msemaji wa familia wala kuingia ndani kwa Mo kutokana na walinzi kukataa kutoa ushirikiano.

Walinzi hao walisema wamepewa maagizo ya kutoruhusu waandishi wa habari katika nyumba hiyo.

“Tangu juzi tumepewa maagizo maalumu kwamba waandishi wa habari hamruhusiwi kabisa kuingia ndani,” alisema mmoja wa walinzi hao.

Hata hivyo, chanzo kimoja ambacho kilijitambulisha kuwa ni jirani wa Mo na kuomba kutotajwa jina   gazetini, kililidokeza gazeti hili kwamba si tu waandishi pekee ambao hawaruhusiwi kuingia ndani ya nyumba hiyo.

Chanzo hicho kilieleza kuwa hata baadhi ya ndugu zake wa damu nao wamezuiwa kuingia.

“Nimeona kuna orodha maalumu ya watu wanaotakiwa kuingia ndani, wengi ni jamii ya kihindi lakini si ndugu wote wanaruhusiwa kuingia.

“Kuna baadhi ya viongozi wa juu wa Serikali pia wanaruhusiwa kuingia lakini nao si wote, kwa mfano wanasheria wapo ambao wameruhusiwa kuingia, lakini pamoja na kuwapo kwenye orodha, muhusika akifika lazima pia apige simu ndani kuthibitisha kuwa ndiye na amefika.

“Lakini hata hao viongozi wa Serikali pia,wakifika wengine kama hawapo kwenye orodha hawaruhusiwi, inabidi yafanyike mawasiliano na walioko ndani ndipo ama aingie au la,” kilieleza chanzo hicho.

Chanzo hicho kilieleza kuwa kwa taarifa zilizopo ni kwamba hata vikao vingi vinaonekana havifanyiki hapo nyumbani.

Chanzo hicho kilisema    kwa maelezo yaliyopo vikao vingi kwa sasa vinafanyika kwenye msikiti wao maeneo ya mjini, ambao baada ya kufuatilia ilibainika kuwa ni msikiti wa Jamatini uliopo Mtaa wa India na Azikiwe.

Kiliongeza kuwa kwa jinsi ulinzi ulivyoimarishwa nyumbani hapo hata walinzi waliopangiwa kulinda ndani, wanalinda ndani tu  na waliopangiwa kulinda nje hao wanalinda nje tu.

MTANZANIA pia lilifika katika eneo la Klabu ya Yatch ambako Jeshi la Polisi lilibainisha kama eneo ambalo litaongezewa ulinzi madhubuti.

Hata hivyo, mmoja wa walinzi katika eneo hilo aliwazuia waandishi langoni,  hakuwaruhusu kuingia ndani ya klabu hiyo.

“Leo si siku ya kazi na hapa wanaoruhusiwa kuingia ndani ni wanachama wetu ambao wana kadi zao maalumu, siwazuii kwa nia mbaya, ikizingatiwa mmekuja kwa nia njema ya kupata taarifa  lakini inabidi nifuate utaratibu, lazima niwasiliane na kiongozi wetu,” alisema na kwenda ndani.

Baada ya dakika kadhaa, mlinzi huyo alirejea langoni  akiwa amefuatana na Meneja wa Klabu hiyo, Brian Fernandes ambaye alisema kutokana na hali ilivyo ndani ya klabu hiyo asingeruhusu  waandishi kuingia.

“Kwa leo (jana), kwa kuwa si siku ya kazi na kuna wateja wetu wengi wakiwa mabalozi huko ndani, hatuwezi kuwaruhusu kuingia.

“Lakini ni kweli eneo hili na ufukwe mzima kuanzia kule Slip Way ulinzi umeimarishwa na Jeshi la Polisi.

“Tunawapa ushirikiano wa kutosha  kwa sababu wote lengo letu ni kuona mwenzetu Mo anapatikana.

“Katika eneo letu tuna kamera zinazonasa matukio yanayoendelea, wamekagua na wanaendelea kukagua kila kinachoendelea,” alisisitiza.

MTANZANIA lilifika pia katika Hoteli ya Slip Way ambako, tofauti na ilivyokuwa Klabu ya Yatch, waandishi waliweza  kuingia ndani.

Akizungumza, Mkuu wa ulinzi katika eneo hilo, Kanali Kasele Charles alithibitisha kuwa katika eneo hilo pia ulinzi ulikuwa umeimarishwa na polisi.

“Tumepokea askari wa Jeshi la Polisi, ulinzi umeimarishwa katika eneo lote.

“Pamoja na hayo, sisi tulijiwekea utaratibu kwamba katika eneo la kule chini (ufukweni) tunafunga saa 12:00 jioni na kufungua saa 12:00 asubuhi.

“Yaani ikifika saa 12:00 jioni haturuhusu mtu yeyote kuonekana eneo lile kwa sababu katika muda huo maji yanakuwa yameanza kurudi.

“Sasa kwa mfano kama mtu anakuwa amekunywa na kulewa, inakuwa si salama kwake, kwa sababu  anaweza kuzama kwenye maji, ikawa taabu kwetu.

“Ikifika saa 12:00 asubuhi tunaanza kuwaruhusu watu kuingia, MO alikuwa anakuja kwenye hoteli yetu pia, hapa kwetu watu kama wale tuna maeneo maalum kwa ajili yao, kupaki gari zao na kufanya shughuli zao.

KAULI YA LUGOLA

Juzi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,  Kangi Lugola alisema Jeshi la Polisi haliwezi kuomba msaada vyombo vya kimataifa vya uchunguzi kwa kuwa bado halijashindwa.

Kangi alitoa kauli hiyo Dar es Salaam baada ya kuulizwa na gazeti hili alipomaliza mkutano wake na waandishi wa habari aliouitisha kutoa tathmini ya matukio ya utekaji na upoteaji wa watu nchini.

Gazeti hili lilitaka kufahamu iwapo Serikali ipo tayari kuruhusu vyombo vya kimataifa kusaidia uchunguzi wa tukio la kutekwa Mo kwa kuwa   siku tatu zimekwisha kupita bila mafanikio yoyote.

Akijibu swali hilo Kangi alisema; “Hatuwezi kuruhusu vyombo vya kimataifa kufanya kazi ya uchunguzi wa tukio hilo kwa sasa kwa kuwa Jeshi la Polisi bado halijashindwa kumpata Mo, tunamtafuta na atapatikana pamoja na waliomteka, tumejipanga vizuri,” alisema Lugola.

HABARI IMEANDALIWA ANDREW MSECHU, VERONICA ROMWALD NA LEONARD MANG’OHA

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles