24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kumpongeza Magufuli sio kosa, ni haki yake

MHINA SEMWENDA

KAMA kijana ninajiona nina deni kubwa sana kwa nchi yangu, mimi kama Mtanzania nimebahatika kushuhudia, ukuaji mkubwa wa nchi yetu katika awamu hii ya tano chini Rais Dk. John Magufuli.

Nashukuru sana Mungu amenijalia uhai wa kuweza kuona maendeleo haya. 

Miaka ya nyuma kabisa nikiwa chuo kikuu cha Dar es Salaam, niliwahi kutamani kumwona Magufuli akiwa Rais, sidhani kama wakati huo yeye binafsi alikuwa na malengo ya kuwa Rais, hamasa niliipata kutoka kwenye wimbo wa msanii Roma Mkatoliki enzi hizo sikuwahi kuhisi kama Magufuli angekuwa Rais ila niliishia tu kutamani.

Nashukuru ndoto yangu ilikuja kuwa kweli, na sasa yale niliyoyatamani ninayaona kwa macho yangu. Maeneo mengi ya nchi yetu sasa yanapitia katika mabadiliko makubwa ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja, vituo vya kufua umeme, ujenzi wa shule na hospitali pamoja na mengine mengi.

Kwa bahati mbaya, sijawahi kuwa mwanasiasa wala sijawahi kutamani kuwa mwanasiasa lakini ni ukweli usiopingika kwamba Rais Magufuli anafanya kazi nzuri.

Kwa dhati ya moyo wangu nampongeza Rais Magufuli, hakika naamini na bado naamini kabisa kwa tulikopitia watanzania na maendeleo yanayofanyika sasa. Sisi Watanzania tulipaswa kuwa wasemaji wakuu wa huyu mzee na kupongeza jitihada zake.

Lakini kwa siasa za Tanzania zilivyo, sasa Rais Magufuli anatumia nguvu kubwa kutueleza tena watanzania kile anachotufanyia nahisi labda kuna wakati anataka kukata tamaa na nahisi labda ndio namna siasa inavyomtaka afanye.

Kiubinadamu hata kama unamfanyia mtu jambo kubwa na hakuelewi unaamua kuachana naye na kuendelea na mambo yako. Ni sawa na mzazi anayepambana na mtoto ambaye hataki shule mwisho wa siku mzazi akikata tamaa akamuacha mtoto ndio huwa anaharibikiwa.

Mara nyingi ukimsikiliza Rais Magufuli anazungumza kuhusu Tanzania na maendeleo ya Tanzania kwa Watanzania wenyewe akiitakia mema Tanzania, sasa hata kama ni siasa ndio zilivyo ifike muda basi tumwelewe huyu mzee tumpe nafasi ya kuendelea kutufanyia kazi hii kubwa anayoifanya.

Ninachokiona mimi sio sawa Rais kutumia nguvu kubwa kutufanyia kazi halafu bado tena atumie nguvu kubwa kutueleza kazi anayofanya kwa sababu anayoyafanya yanaonekana.

Mimi kama kijana ninajiona nina deni kubwa kwa sababu sioni kama naitendea haki nchi yangu kwa kushindwa kusimama na kuisemea, tukiachana na itikadi za kisiasa.

Vijana tunapaswa kuwa mstari wa mbele kuyasema haya na kupongeza na kuwa mstari wa mbele, kuilinda nchi yetu na rasilimali zetu huku tukiwaacha wanasiasa waendelee na siasa zao.

Sio kweli kwamba kazi haifanyiki, inafanyika na tunaona sasa kwanini bado tena tunalaumu na kulalamika au wakati mwingine na kutukana kabisa.

Mimi sio mwanasiasa kama nilivyosema, lakini kila kijana au mtu akisimama na kusema au kutoa pongezi kwa Serikali hii utasikia au utaambiwa unahitaji kupewa ukuu wa wilaya au ukurugenzi, kitu ambacho sio sawa.

Lazima tujenge misingi ya kutofautisha uzalendo wa kusifia maendeleo na uzalendo wa kuipenda Tanzania na siasa au itikadi za chama kimoja au kingine.

Kupongeza au kusifia sio kosa au sio dhambi, ni utashi tu wa kibinadamu. Sasa kama itikadi za kisiasa ndio zinafanya tushindwe kuona yanayofanywa hata kama yanaonekana basi kuna shida kwenye siasa zetu.

Muda wote ninaposhuhudia siasa zetu nimejaribu kuwa muwazi ili nisiburuzwe na itikadi bali niwe katika mtazamo wa wazi.  

Kiubinadamu viongozi wanaweza kukosea wao sio malaika lakini sio baya moja lifute mazuri yote yaliyofanywa. Kila binadamu anafanya makosa hata mimi binafsi nimefanya makosa huko nyuma na bado nitafanya makosa.

Iweje kila linalofanywa kwa maendeleo ya nchi yetu lionekane baya kisiasa wakati kiuhalisia sisi ndio tunaonufaika nalo?

Nitatoa mfano midogo, ujenzi wa hospitali ni kwa manufaa yetu au wanasiasa? ujenzi wa barabara ni kwa manufaa yetu au, ujenzi wa madaraja ni kwa manufaa yetu au? Jibu ni ndio kwa sababu sisi ndio watumiaji wakuu wa miundombinu hiyo pamoja na mingine mingi.

Ubora wa barabara ni kwa manufaa yetu pamoja na mengine mengi, sasa sijui watanzania tunatakiwa tufanyiwe nini na viongozi wanaokuwa madarakani ili tuweze kuelewa na kuwapongeza huku tukiweka itikadi zetu za kisiasa pembeni.

Tukiachana na sifa za kisiasa au pongezi za kisiasa na wanasiasa, Watanzania tunapaswa kuwa wasemaji wakuu wa maendeleo yetu kwa nchi yetu.

Na sio kuwaacha wanasiasa kuwa wasemaji wa midomo yetu, kuona kwa macho yetu  na kuhisi hisia zetu, kwamba kila atakayesifia anataka madaraka au anataka kiki au anataka kujionesha hii sio sawa kabisa. 

Tujifunze kutengenisha siasa na maendeleo ya nchi yetu. Tuiangalie nchi yetu kwanza kisha siasa ndio zifuate. Siasa isiwe sehemu ya kukatisha tamaa, watendaji wa Serikali katika kutimiza majukumu yao au siasa isiwe sehemu ya kuwafanya watanzania wasiwe huru kusifia maendeleo wanayoyaona.

Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, Rais Magufuli anafanya kazi kubwa kwa nchi hii. Tumuunge mkono na tuwe sehemu ya kumpa moyo na faraja ili apate moyo wa kufanya makubwa kwa nchi yetu.

Kuna siku niliwahi kuwaza jambo moja. Hivi mtu anapokuwa kiongozi (Rais) na akafanya kazi yake vizuri ana lipi la kupoteza kati yetu sisi Watanzania au yeye kiongozi. 

Nitatoa mfano, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete au Rais wa awamu ya tatu, Benjami Mkapa na Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi wana lipi la kupoteza?

Baada ya kumaliza vipindi vyao na sasa wamepumzika. Hayo waliyoyafanya katika kipindi chao wasingeyafanya kwani wasingekuwa walivyo sasa?

Wamefanya yao mengi mazuri na mengine mabaya, lakini sasa wamepumzika wamemuachia kijiti Rais Magufuli ambaye naye itafika siku yake atapumzika.

Sasa kwanini kwa haya anayoyafanya kwetu sisi Watanzania tusimpongeze na kumpa moyo afanye zaidi maana mwisho wa siku, sisi ndio wanufaika wa haya yote.

Vijana bado tuna deni kubwa kuisimamia nchi yetu na kuuweka uzalendo wetu mbele na kuachwa kuongozwa na itikadi za kisiasa, hata tukasahau mambo ya msingi katika kuijenga nchi yetu.

Lazima tujenge utamaduni wa kujivunia vilivyo vya kwetu. Rais ni wetu tulimchagua wenyewe kwanini tusimuunge mkono na kumpa nguvu kuipeperusha bendera na nchi yetu vizuri?

Popote duniani, ukitamka Tanzania lazima Magufuli ndio aonekane nyuma ya bendera yetu sasa kwanini tusimuunge mkono na kumsaidia kuipaisha nchi yetu kimaendeleo.

Vijana tuna deni kubwa kwa nchi yetu tusipoliangalia hili sijui, watoto wetu siku zijazo watakuwa na hali gani.

Mimi binafsi nimejitoa kukupongeza na kukusifia na zaidi kukutia moyo. Pambana. Nchi yetu itafika tunakotaka. Mengineyo yatafuata baadaye.

Kwa sisi tusio wanasiasa hatufuati itikadi zetu, lakini tunamsemea mama Tanzania ambaye wewe leo ndio unamjenga na alama unazoweka zitabaki daima hata kama sio kwetu ni kwa watoto wetu na wajukuu zetu.

[email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles