25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 21, 2023

Contact us: [email protected]

Kuibuka kwa ‘Populism’ na mustakabali wa siasa za ulaya, Marekani

MWALIMU MATTEO MWITA

Kama umekuwa mfuatiliaji wa siasa za duniani, utakuwa umebaini wimbi la mabadiliko kwenye siasa. Wimbi hilo, limeletwa na kuibuka kwa watu fulani kwenye uongozi ambao hawakutegemewa kama wangeaminiwa na kupewa fursa za juu za kiuongozi.

Au kujizolea umaarufu kwa baadhi ya vyama katika baadhi ya nchi. Mtu kama Donald Trump kuchaguliwa kuwa rais wa taifa la Marekani, ambalo limejipambanua kuwa la kidemokrasia na kujali haki za binadamu kunatia mashaka.

Ila pia, kujizolea umaarufu kwa vyama kama UKIP cha Uingereza, AfD cha Ujerumani, National Rally cha Ufaransa n.k. kunazua wasiwasi ni wapi dunia inaelekea kisiasa.

Upepo huu wa kisiasa unatazamwa kwa pande mbili tafauti. Kuna baadhi wanaona kuwa unarudisha heshima ya baadhi ya mataifa, heshima iliyopotea hapo kabla, huku wengine wanaona ni kama kuipeleka dunia kwenye zama za giza. 

Ni nini hasa kinatokea?

Kumekuwa na kutoridha kwa baadhi ya watu kwa muda mrefu kuhusu baadhi ya mambo yanavyofanyika kwenye baadhi ya Serikali duniani. Kuna wananchi wameonesha kutoridhika na jinsi viongozi waliopewa dhamana ya kuwaongoza wanavyowaongoza.

Wengi wamekuwa wakisema, viongozi hawatekelezi ahadi zao na hali za uchumi kwa rai wa kawaida zinazidi kuwa ngumu. Hapo ndipo walipozuka viongozi wa kisiasa  wanaopinga mfumo uliopo madarakani. Mfumo huo wanazuoni wa maswala ya sayansi ya siasa wanauita “establishment”. Wakati harakati za kuupinga mfumo huo zinaitwa “populism”.  

 Populism na establishment ni nini?

Populism ni harakati za kisiasa ambazo zinajipambanua na watu. (harakati hizi zimekuwa zikijitanabaishi kuwa sehemu/sauti ya watu ambao wametengwa na mfumo). Na establishment ni kundi la watu wasomi wachache wanaoshikilia madaraka ya taifa fulani.

Mara nyingi, watu hawa wanakuwa ni wale wale wanaopata fursa ya kuongoza. Mathalani, unaweza kutabiri kiongozi atakayefuata kwenye chama flani, kwakuwa amekua kwenye mfumo wa siasa kwa muda mrefu.

Mfano dhahiri, ni pale Hillary Clinton alipopitishwa kupeperusha bendera ya Democratic, wengi walitegemea hilo kwakuwa alikuwa kwenye mfumo na amewahi kushika nyadhifa kadhaa wa kadhaa kwahiyo ni moja ya ‘elites.’

Kwa mujibu wa mwandishi Cas Mudde, aliyeandika “populism: A very short introduction” anasema kwenye muktadha wa siasa ‘populism’ ni wazo kuwa jamii imegawanyika katika makundi mawili. Yaani wale ambao ni waadilifu na mafisadi. kwa mana ya jumla nikuwa _‘populism’_ ni harakati za baadhi au kikundi cha watu wanaopinga mfumo wa kifisadi ambao umejengwa na _‘establishment’_

Kuibuka kwa harakati za ‘populism’

Kuibuka kwa ‘populism’ kunafungamanishwa na hali ya kisiasa na kiuchumi na swala hili linaweza kufananishwa kuibuka kwa makundi ya mrengo mkali miaka ya 1930. Kama ilivyokuwa kwa mwaka 1929, uchumi ulijokita kwenye baadhi ya vitu na ambao haukudhibitiwa ulipelekea mdororo wakiuchumi mwaka 2008.

Kusinyaa kwa uchumi na ukosefu wa ajira Ulaya magharibi ni mabaki ya mdondoko wa kiuchumi. Sarafu ya euro, kama thamani ya dhahabu ya miaka ya 1920 na 1930, imezifanya nchi masikini, maisha ya pande kitu kilichopelekea matatizo ya kiuchumi na kushindikana kuimarika hali ya uchumi hata baada ya kupunguza thamani ya fedha zao.

Wataalamu wa mambo ya uchumi wanasema, kwenye nchi nyingi za ukanda wa Euro, pato la taifa la kila mtu limekuwa kidogo sana ukilinganisha na mwaka 2007. Haishangazi ni kwanini ‘populist’ wanajipatia umaarufu.   

Utofauti mkubwa wa kipato kwa nchi za magharibi leo hii unafanishwa na ule mwa miaka 1920. Soko huria na ubunifu unaoletwa na teknolojia hudumaza vyama vya wafanyakazi.

Sera za kodi na kuhamishia viwanda nchi nyingine kama njia ya kukwepa utitiri wa kodi unasababisha watu wasio na ujuzi au wenye ujuzi mdogo kukosa kazi. Kwahiyo utafauti kati ya masikini na matajiri utaendelea kuongezeka.  

Ukiachilia hali ya kiuchumi, hali ya upigaji kura kwa nchi za magharibi imepungua kwa kiasi kikubwa kuanzia miaka ya 1970, hasa kwa vijana wa mijini, na waliobaki ndio wanaunga mkono “populism.”

Wapiga kura wameacha kujihusianisha na vyama vyao. Kitendo hicho kimesababisha ‘populists’ kuungwa mkono hata kama hawana muda mrefu kwenye siasa.  Nchini Marekani kwa mfano, maarifa kuhusu siasa yameongezeka kidogo sana kuanzia miaka ya 1950. Na utafiti wa hivi karibuni unaonesha kuwa wapiga kura wenye uelewa mdogo kuhusu siasa ndio waliosaidia ushindi wa Trump.

Uingereza utafiti baada ya kura ya kujitenga unaonesha kuwa wananchi hawakuwa na takwimu sahihi juu ya wahamiaji. Sasa hivi Facebook na Twitter ndio chanzo cha kwanza cha habari kwa watu wengi.

Hii inamaanisha kuwa maoni ya kisiasa yanatolewa kwa ufinyu, maoni haya yanakuwa ya upande moja, huku yakishabikiwa na maswahiba, familia au watu waliokuwa na mrengo sawa.

Hii athari yake ni kuibuka kwa habari zinazoegemea upande moja, habari ghushi na kupotea ule uandishi wa habari uliotukuka unaoangalia pande zote za habari. Kitendo cha watu kujikita zaidi kutazama filamu na matumizi ya michezo ya komputa kuna sababisha kufifia kwa fikra tunduizi, kitu kinachopelekea watu kutofikiri kwa kina na kuchukua maamuzi sahihi. 

Sababu tajwa hapo juu zilipelekea watu kufanya maamuzi waliyoyafanya kwenye kura za maoni za Uingereza kujitoa kwenye jumuiya ya Umoja wanchi za Ulaya na ushindi wa rais Trump Marekani. Kitu kilichowashtua wanazuoni na wafuatiliaji wa mambo ya siasa ulimwenguni.

Pamoja na wasiwasi na hofu ya baadhi yetu kuwa ‘populist’ wataingia madarakani Ulaya. Ila ukiangalia chaguzi zilizopita kwenye baadhi ya madarakani kwenye baadhi ya nchi za Ulaya, ukifanya uchunguzi utabaini kuwa itawachukua muda populist kuhodhi madaraka.

Ukiangalia, si kwa Geert Wilders wa Uholanzi au marine Le Pen wa Ufaransa walioweza kupata ushindi wa wakuvifanya vyama vyao kuunda serikali. Japo Ujerumani chama cha (AfD) kilifanikiwa kupata asilimia 13 ya kura na kupata wawakilishi kadhaa kwenye bunge la Bundestag. 

Baadhi ya wachambuzi wa maswala ya siasa wanasema ushindi huo sio wa kubeza. Dunia inabidi ichukulie ushindi huo kama kengele ya tahadhari. Wanasema, Le Pen kwenye uchaguzi uliopita aliweza kupata kura milioni 10.

Kwa Marekani Trump aliweza kushinda uchaguzi na mara baada ya kushinda, kuna mambo kadhaa yanayo leta shaka kwa utawala wa kisheria na kuheshimu haki za binadamu yameanza kujitokeza kama vile; vikundi vya baadhi ya weupe kuanza kujiona bora zaidi yaw engine, kuyazuia baadhi ya mataifa ya kiislamu kuingia Marekani, kuanzisha kampeni didhi ya wahamiaji na baadhi ya vyombo vya habari.

Nini Kifanyike kupunguza nguvu ya Populists?

Ili kuzua populism kunahitajika mabadiliko makubwa sana. demokrasia na kushamiri kwa muingiliano wa kivyama hakuwezi kuboreka au kuendelea kuepo kama uchumi sio mzuri na hakuna iwiyano sawa kati ya matajiri na maskini.

Serikali za Ulaya na Marekani inabidi zifanye juhudi za kuboresha uchumi kwenye nchi zao. Wawekeze kwenye elimu ya ufundi, elimu ya juu na kutengeneza fursa za ajira. 

Bila juhudi za mathubuti basi Ulaya na Marekani  zitarudi  kwenye zama za ufascist na hapatakuwa mahali salama tena  pa kuishi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles