25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Kondomu pakiti 17,000 zaondolewa sokoni

Na AVELINE KITOMARY-MOROGORO 

KATIKA kuhakikisha udhibiti wa vifaa bandia sokoni unafanikiwa, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imesema kwa mwaka wa fedha 2019/2020 iliondoa sokoni paketi 17,076 za kondomu kwa kushindwa kukidhi vigezo vinavyotakiwa.

Hayo yalisemwa jana mkoani  Morogoro na Kaimu Mkurugenzi wa Dawa na Vifaa Tiba, Akida Khea wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari katika kikao kazi cha uhamasishaji wa waandishi wa habari kuhusu usimamizi wa Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba sura 219.

Khea alisema bidhaa hizo zilizoondolewa ni zile feki ambazo hazikidhi matakwa ya viwango, zinazoweza kuwa na madhara na nyingine ni zile ambazo zilikuwa zikiuzwa kwa kutumia jina la mtu mwingine.

“Kwanza kabla ya kondomu kuingia sokoni huwa tunapima ubora wake, kama kiwango cha mafuta, ustahimili wa matumizi na urefu wake, hivyo endapo tukipima na tukakuta haina vigezo tunaizuia kuingia sokoni.

“Pia licha ya hiyo, huwa tunafanya ukaguzi katika maduka mbalimbali hapa nchini kwa kuangalia ubora wa bidhaa zilizopo na kama muda wa matumizi ya bidhaa hizo hazijaisha, hivyo tuko makini katika udhibiti wa usalama wa ubora wa bidhaa,” alieleza Khea.

Alisema kondomu zilizoondolewa sokoni ni takribani aina tano ambazo ni Life Guard, Ultimate, Maximum Classic, Prudence na Chishango.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa TMDA, Adam Fimbo, alisema mamlaka hiyo inafanya kazi za udhibiti ili kuhakikisha afya ya wananchi inakuwa salama.

“TMDA inafanya ukaguzi mara kwa mara ili kuhakikisha hamna bidhaa bandia sokoni na kama zikipatikana hatua za kisheria zinachukuliwa kwa watu wanaokiuka taratibu zilizowekwa,” alifafanua Fimbo.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano, Serikali imejenga viwanda 16 kwa ajili ya dawa na vifaa tiba ili kuhakikisha vinapatikana nchini.

“Tumepunguza masharti ili kuruhusu viwanda kujengwa, hiki ni kitu kikubwa kwani Serikali inaendelea kuhamasisha uchumi wa viwanda, hili ni jambo kubwa kwetu,” alisema Fimbo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles