Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
KONDAKTA wa daladala, Hamimu Seif (42) amepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kutishia kumuua kwa maneno, Rais Dk. John Magufuli.
Mshtakiwa huyo ambaye ni mkazi wa mtaa wa Ujiji, Mwananyamala, alipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi, Hellen Riwa na kusomewa shtaka na wakili wa serikali Mwandamizi, Kenneth Sekwao.
Sekwao alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Machi 10 mwaka huu katika baa ya Soweto iliyopo Makumbusho,Wilaya ya Kinondoni,Dar es Salaam.
Ilidaiwa kwamba mshitakiwa alitishia kumuua Rais Magufuli kwa kutamka maneno kuwa, ‘Kwa mambo anayoyafanya Rais Magufuli, nipo tayari kujilipua kwa kujitoa mhanga ili kumuangamiza’.
Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo na upande wa mashtaka ulisema upelelezi haujakamilika.
Hakimu Riwa alikubali kumpa dhamana mshtakiwa kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni mbili.
Mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti hayo na alirudishwa rumande hadi Aprili 21 mwaka huu kesi itakapotajwa.