ABUJA, NIGERIA
KIONGOZI wa kundi la Boko Haram nchini Nigeria, Aboubakar Shekau, amejeruhiwa vibaya kwenye shambulio la angani lililofanywa na jeshi la nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la Nigeria, makamanda wengine wakuu wa kundi hilo pia wameuawa wakitajwa kuwa ni pamoja na Abubakar Mubi, Malam Nuhu na Malam Hamman.
Jeshi la Anga la Nigeria limesema shambulio hilo lilitekelezwa Ijumaa iliyopita wakati viongozi hao wakishiriki sala ya Ijumaa katika Kijiji cha Taye, eneo la Gombale katika msitu wa Sambisa, jimbo la Borno.
“Kiongozi wao, anayefahamika kama, Abubakar Shekau, anaaminika kujeruhiwa vibaya begani,” jeshi limesema kupitia taarifa iliyotolewa na Naibu Mkuu wa Mawasiliano, Kanali Sani Kukasheka Usman.
Huko nyuma jeshi la Nigeria liliwahi kutoa ripoti za kifo cha Shekau, kabla ya mtu anayejieleza kuwa ni kiongozi huyo, kuonekana katika video akitoa taarifa.
Hakukuwa na taarifa ya haraka kutoka kundi hilo kukiri au kukana shambulio, ambalo limetokea huku kundi hilo likikabiliwa na mvutano wa kuwania madaraka baina ya Shekau na Abu Musab al-Barnawi anayeungwa mkono na kundi lijiitalo Dola la Kiislamu.