22.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, July 23, 2024

Contact us: [email protected]

Kinondoni yapitisha bajeti ya bilioni 248/-

Boniface JacobNa Ruth Mnkeni, Dar es Salaam

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni imeidhinisha bajeti ya Sh 248,477,433,909 kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Akizungumza wakati wa kikao cha kupitisha bajeti hiyo cha Baraza la Madiwani, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob, alisema kati ya fedha hizo, Sh 64,285,690,000 ni makusanyo ya mapato ya vyanzo vyao vya ndani.

Jacob ambaye ni Diwani wa Kata ya Ubungo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema mapato kutokana na ruzuku kutoka Serikali Kuu ni Sh 182,771,743,909, mapato kutokana na michango ya nguvu ya wananchi ni Sh 1, 420,000,000 na mapato kutokana na fedha za mfuko wa barabara ni Sh 12,281,790,010.

Pia alisema bajeti ya mapato ya ndani imelenga kutatua changamoto zilizopo na imeongezeka kutoka Sh 56,550,927,000 hadi kufikia Sh 64,285,690,000 kutokana na vyanzo vya kodi ya majengo, mabango, huduma ya jiji, huduma za biashara na kodi za hoteli.

Katika hatua nyingine, alitaja maeneo yaliyopewa kipaumbele katika bajeti hiyo kuwa ni kuboresha na kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kuboresha miundombinu katika shule za msingi na sekondari, kuondoa tatizo la madawati na vifaa vya maabara, kuboresha sekta ya afya, kuboresha miundombinu ya barabara na kutoa huduma bora ya maji.

Alisema maeneo mengine ni kuimarisha kilimo mjini, kuboresha uhifadhi wa mazingira na ukusanyaji wa taka, kuboresha mazingira ya wafanyabiashara ndogo ndogo na kuimarisha ushirikishwaji wa jamii katika upangaji na utekelezaji na uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia mfumo wa wanawake na vijana.

“Katika sekta ya elimu manispaa imetenga zaidi ya shilingi bilioni 10 kwa kushirikiana na Serikali Kuu kutekeleza kwa vitendo sera ya elimu bure kwa kushughulikia changamoto mbalimbali kama upungufu wa madarasa, madawati, matundu ya vyoo, vifaa vya maabara na ukarabati miundombinu mibovu pamoja na kugharamia huduma za maji, umeme na ulinzi.

“Pia katika bajeti hii fedha hizi za sekta ya elimu zitanunua madawati 30,000 ili kuweza kuondokana na uhaba wa madawati kwa shule zetu za Kinondoni,” alisema Jacob.

Pia alisema ili kuhakikisha manispaa hiyo inakuwa safi wakati wote, jumla ya Sh 2,280,000,000 zimetengwa kwa ajili ya kununua malori 25 ya taka na kila kata itapewa gari moja.

“Pia shilingi milioni 400 zimetengwa kwa ajili ya kununua gari la majitaka na shilingi bilioni 1.2 zimetengwa kwa ajili ya kununua magari mawili ya kusaga taka (compactor) na zaidi ya Sh bilioni 3.6 zitatumika katika kuboresha huduma za usafishaji kwa shughuli mbalimbali,” alisema Jacob.

Akizungumzia uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, alisema manispaa inakusudia kuboresha mfumo wa ukopeshaji wa fedha za mfumo wa wanawake na vijana ili waweze kunufaika na fedha zinazotengwa kutokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya manispaa.

Alisema zaidi ya Sh bilioni 4.7 zimetengwa na kila kata itatumia Sh milioni 200 kwa maana Sh milioni 100 kwa vijana na Sh milioni 100 kwa wanawake.

Katika kuhakikisha barabara zinapitika wakati wote, alisema manispaa hiyo imetenga Sh 150,000,000 kwa ajili ya kununua kijiko na Sh 1,000,000,000 kwa ajili ya kununua greda ya matengenezo ya mara kwa mara ya barabara za kata na mitaa zilizopo katika hali mbaya kutokana na mvua zinazoendelea.

Pia alisema hadi kufikia Juni, mwaka huu wazee watakuwa wakitibiwa bure huku wananchi wa kawaida watakuwa wanalipia Sh 40,000 kwa mwaka ili waweze kutibiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles