25.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 12, 2024

Contact us: [email protected]

KIM NANA KUWAPIKU ZARI, MOBETTO KWA DIAMOND?

Na JOSEPH SHALUWA


NENDA Kamwambie ndiyo wimbo uliomtambulisha kwenye game la muziki wa Bongo Fleva, msanii Nasibu Abdul ‘Diamond Plantumz’. Mbagala ukafuatia na kuzidi kumpaisha. Hapo hakulaza damu, akaongeza juhudi.

Mara paaap! Akaondoka na tuzo tatu za Kili mwaka 2010. Hiyo ikawa moto wa kifuu. Tangu hapo Diamond hajawahi kufanya makosa kwenye kazi yake ya muziki. Mpaka sasa ana utitiri wa tuzo kutoka ndani na nje ya nchi.

Amefanya kolabo na wasanii wengi wenye uwezo wa ndani na nje ya nchi, huku akitumbuiza kwenye shoo kubwa za nje ya nchi na matamasha makubwa. Amefanya kolabo kibao na wasanii wa Nigeria, akaona haitoshi akaingia Marekani.

Muziki wake unazidi kupaa siku hadi, huku mafanikio yake yakiwa siyo ya kutafuta. Alizaliwa Tandale, akahamia Sinza na sasa anaishi Madale, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, akivuta hewa safi katika hekalu lake.

Ndani ya hekalu lake la kifahari, yupo mtoto mzuri anayekwenda kwa jina la Kim Nana. Hilo ni jina la mjini. Wazazi wake kule Moshi walimpa jina la Lilian Kessy. Mrembo huyo ni video vixen ambaye ameanza kuwa juu  kwa sasa.

Pekupeku za mtaani zinaeleza kuwa, kwa sasa Diamond hapindui kwa mrembo huyo na kwamba muda wowote, watu watafinya mpunga kwani ndoa ipo njiani. Siyo hivyo tu, msichana huyo tayari ameshabadili dini na kumfuata Diamond.

 

KIM NANA KUWAPINDUA ZARI, MOBETTO?

Ishu inayogonga vichwa vya wengi kwenye anga la burudani ni je, mrembo huyo atafanikiwa kuwaondoa warembo, Zarina Hassan ‘Zari The Boss Lady’ na Hamisa Mobetto na kufunga ndoa na staa huyo?

Kwa muda mrefu kumekuwa na mvutano kati ya Zari na Hamisa, juu ya nani hasa angeingia ndani ya mjengo, lakini mwisho wa yote ikatokea Zari kumwagana na Diamond na kutimkia nyumbani kwake Afrika Kusini.

Je, Kim ana jipya lipi litakalomfanya Diamond awapotezee moja kwa moja wazazi wenzake Zari na Hamisa? Hayo ndiyo maswali wanayojiuliza wananzengo wengi kwenye mitandao ya kijamii.

Tukumbuke kuwa licha ya Mond kuwa na listi ndefu ya wadada walioingia kwenye uhusiano naye, Zari na Hamisa walipewa nafasi kubwa zaidi hasa baada ya kufanikiwa kuzaa nao.

Zari amezaa watoto wawili na Diamond – Tiffah na Nillan, huku Hamisa akizaa naye mtoto mmoja anayetajwa kwa jina la Dylan.

 

MASTAA WALIOTOKA NA DIAMOND

Mbali na Zari na Hamisa, wapo mastaa wengine ambao waliwahi kutoka na Diamond. Tuachane na wale ambao hakudumu nao muda mrefu, tuzungumzie wale ambao uhusiano wao ulikuwa moto kiasi cha ndoa kunukia.

Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu ndiye staa ambaye alikuwa na uhusiano ulioiva na Diamond na kudumu kwa muda mrefu. Uhusiano wao una historia ndefu; Diamond mwenyewe anakiri kufundishwa lugha ya Kiingereza na Wema.

Uhusiano wao ulikuwa kivutio kwa mashabiki wao, nyota zao kwa pamoja zikazidi kung’ara huku wengi wakiamini mastaa hao wangeingia kwenye ndoa, lakini baada ya muda uhusiano wao ulivunjika.

Hata alipoingia mtangazaji mahiri, Penniel Mungilwa ‘Penny’ naye alipewa nafasi kubwa zaidi na penzi lao likawa moto, lakini mwisho wake wakamwagana.

 

DIAMOND MWENYE SURA TATU

Diamond ni staa mwenye sura tatu. Ni mwenye kipaji na asiye na mchezo na kazi kabisa. Ni mpambanaji mwenye kutafiti, kujua na kuwapa mashabiki wanachokitaka. Ni staa wa Bongo Fleva mwenye mafanikio makubwa.

Katika kipindi cha miaka nane tangu atoke kimuziki, amekuwa mwenye mafanikio makubwa, anajitahidi kulinda hadhi ya muziki wake. Anamiliki nyumba kadhaa, viwanja, mashamba na kampuni za muziki na habari.

Sura ya pili ya Diamond ni kulipa fadhila. Anajua kurudisha kwa jamii. Amesaidia wengi wenye uhitaji. Mara kadhaa amejitolea kuwasaidia wasanii wenzake, wanawake na watoto.

Hivi ninavyoandika makala haya, msanii Hawa Said ‘Hawa wa Nitarejea’ yupo nchini India akiendelea na matibabu kwa gharama zake. Yupo vizuri sana kwenye eneo hilo.

Sura ya tatu ni ‘Sukari wa Warembo’. Haonyeshi msimamo kwenye mambo ya uhusiano. Wapo wanaosema kuwa huenda Diamond amechagua aina hiyo ya maisha ili awe anazungumzwa sana na mashabiki.

Katika sura zote tatu, hii ya mwisho haipo sawa. Diamond anapaswa kuangalia namna ya kufanya ili kujisafisha katika eneo hilo. Kitu pekee anachotakiwa kufanya ni kuchukua uamuzi wa kuoa.

Heshima yake kimuziki na kusaidia jamii, inaweza kupanda maradufu akichukua uamuzi wa kuoa. Pengine huu ni wakati wake sahihi zaidi kumuoa Kim Nana ikiwa wameridhiana na amemuona anafaa kuwa malkia katika hekalu lake Madale!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles