23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Kilichosaidia udumavu kwa watoto kupungua

Na AVELINE KITOMARY

UDUMAVU ni tatizo linalotokana na utapiamlo unaosababishwa na ukosefu wa lishe bora, ambapo huwakumba watoto wadogo.

Mtoto akidumaa hupata athari zisizoweza kurekebishika, hudumu katika maisha yake yote. Hali ya udumavu husababisha kupungua kwa kasi ya maendeleo ya ukuaji wa akili na hivyo kuwafanya watoto wapate matokeo mabaya darasani.

Udumavu pia husababisha kupungua kwa kasi ya ukuaji kimwili, kupungua kwa uwezo wa kufanya kazi ambapo matokeo yake huwa ni kupunguza mapato kiuchumi.

Watoto hao wana uwezekano wa kuwa na uzito uliozidi au kiribatumbo, kuugua magonjwa ya moyo, kiharusi, shinikizo kubwa la damu na kisukari wakati wanapofikia umri wa utu uzima.

Ili watoto wawe na afya bora wanatakiwa kupata lishebora kuanzia tumboni, kunyonyeshwa ipasavyo na baadaye kula mlo kamili.

Wataalamu wanasema baada ya mtoto kuzaliwa anatakiwa kunyonya maziwa ya mama pekee hadi atakapofikisha umri wa miezi sita na baadaye taratibu kuanza kulishwa vyakula vingine.

HALI YA UDUMAVU NCHINI

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dk. Germana Leyna, anasema sasa hivi kiwango cha udumavu kwa watoto wa umri wa chini ya miaka mitano kimepungua.

Kwa mujibu wa Dk. Leyna, tathmini ya mwaka 2018 inaonesha kuwa kiwango cha udumavu kimeshuka kutoka asilimia 34 hadi asilimia 31.7.

“Kwetu sisi ni mafanikio, japo hatujaweza kufikia malengo ya kidunia ya udumavu chini ya asilimia 20 ya watoto hao.

“Pia tumuweza kupambana na utapiamlo na kupunguza kiwango cha ukondefu kwa watoto kutoka asilimia 4.5 mwaka 2015/2016 hadi kufikia asilimia 3.5 mwaka 2018. Kiwango hiki kimeendana na malengo ya afua ambayo ni asilimia tano.

“Tumeweza kushusha na kupunguza kiwango cha wanawake wenye upungufu wa damu, awali mwaka 2015 /2016 waliokuwa na tatizo hilo walikuwa ni asilimia 45 lakini mwaka 2018/2019 ni asilimia 29,” anasema Dk. Lyna.

“Huwa tunafanya tafiti ili zitusaidie kugundua ukubwa wa tatizo. Baadhi ya tafiti hizo ni pamoja na ile ya lishe kitaifa (TNNS 2018) iliyoangalia mtawanyiko wa wazal- ishaji chumvi na ile ya kuangalia upungufu wa vitamin A na madini ya chuma katika kaya.

“Matokeo ya tafiti hizi yameendelea kusambazwa kwa wadau ili kusaidia kuboresha afua za lishe nchini,” anaeleza Dk. Leyna.

UNYONYESHAJI WAONGEZEKA
Mwanzoni elimu ya unyonyeshaji kwa muda wa miezi sita ilikuwa haitiliwi mkazo lakini kadri wataalamu wa lishe wanavyoelimisha jamii ndiyo unyonyeshaji kwa hatua ya miezi sita ya mwanzo unavyongezeka.

Kiwango cha unyonyeshaji kwa muda wa kipindi hiko umekuwa na nafasi kubwa zaidi katika kupunguza udumavu.

Dk. Leyna anasema kiwango cha unyonyeshaji kimeongezeka kutoka asilimia 41 ya mwaka 2014 na kufikia asilimia 58 kwa mwaka 2019.

Mkurugenzi wa TFCN, Dk. Germana Leyna akionyesha mkoba wa siku 1000

“Baada ya miezi sita mtoto anatakiwa ale chakula chenye mchanganyiko wa makundi mawili, mwaka 2014 asilimia 20 ya watoto kati ya umri wa miezi sita hadi 23 waliweza kulishwa ipasavyo kwa idadi ya milo inayotakiwa na chakula mchanganyiko hadi mwaka 2019 walifikia asilimia 30.

“Tunapima kiwango cha unyonyeshaji wa kwa kipindi cha miezi sita baada ya mtoto kuzaliwa kwa kutumia teknolojia ya atomic ambayo mtoto akipewa chakula kingine hata maji kipimo hicho kinaonesha.

“Katika kupima tunachukua mate ya mama na ya mtoto, tunamnywesha mama aina ya madini ili mtoto apate kupitia maziwa ya mama. Kama mtoto anameshawahi kunyweshwa kitu kingine inajulikana.

Tulifanya upimaji kwa kina mama 132 katika mikoa ya Iringa na Njombe, kila sehemu tulichukua sampuli 33 za mama na mtoto katika kila wilaya.

KUONGEZA VIRUTUBISHI VIWANDANI
Hatua ya uongezwaji wa virutubishi kwenye chakula imekuwa ikisaidia zaidi kupunguza kiwango cha udumavu, hii ni baada ya madini muhimu kupatikana katika vyakula hivyo.

Katika hili, kitengo cha maabara ya kupima vyakula imekuwa na uwezo mkubwa wa kubaini kiwango cha virutubishi na madini katika vyakula na mwili wa binadamu, madini yanayopimwa ni pamoja na copper, iron na madini tembo.

Mkuu wa Idara ya Microbiolojia katika maabara hiyo, Abdurahman Azizi, anasema kuna njia mbili za kuongeza kiwango cha virutubishi mwilini .

Anazitaja: “Njia ya kwanza tuna- fanya kibiologia, hii ni ya kuonge- zwa virutubishi moja kwa moja kwenye vyakula viwandani pale kinapotengenezwa. Tumekuwa tukifanya hivi kwenye viwanda vikubwa, lakini hivi karibuni tutafika kwenye viwanda vidogovidogo au hata vyama vya ushirika.

“Virutubisho tunavyoongeza ni vitamini A kwenye mafuta ya kula, Vitamini A ,B12, zink, folic acid na madini ya chuma kwenye unga wa ngano na mahindi. Hii inafanyika kwenye viwanda vikubwa, kwa upande wa viwanda vidogo tunaongeza kwenye unga wa ngano.

“Njia nyingine ni kulima vyakula vyenye virutubishi, tunahama- sisha kilimo cha vyakula kama viazi lishe, mahindi lishe na maharagwe. Mfano, viazi na mahindi vinaongeza vitamini A na maharagwe yana madini ya chuma, hivi ni vyakula ambavyo tunahamasisha wakulima kulima na kutumia.”

Licha ya njia hizo, anasema pia wanahakikisha madini joto yanaongezwa kwenye chumvi ambapo hii hufanyika kwa kushirikiana na wauzaji wadogo hivyo, asilimia 61 ya kaya hutumia chumvi yenye madini joto huku mpango ukiwa ni kufikia asilimia 90.

Ofisa utafiti wa biochemistry, Francis Milinga, anasema uboreshwaji wa maabara umesaidia kutoa uhalisia wa upimaji wa sampuli za aina mbalimbali ikiwamo upimaji wa virutubisho kwenye damu.

“Tumenunua vifaa mbalimbali vya kupima virutubisho kwenye vyakula vya kiwandani, upimaji wa virutubishi kwenye damu, kupima kiwango cha mafuta kwenye mwili na kiwango cha unyonyeshaji wa maziwa ya mama.

“Pia tumefanya utafiti wa madini joto mwilini hasa tumengalia viwanda vidogo vidogo, tafiti ya mwisho inangalia upungufu wa virutubisho ngazi ya kaya mkoani Morogoro kwa kushirikiana na Shirika la Udhibiti wa Magonjwa (CDC), ambapo sasa tuko hatua ya mwishoni.

“Tunaangali folic acid kwa wanawake walioko katika umri
wa kuzaa miaka 18 hadi 49 kwa sababu wanawake waliko katika umri wa kuzaa wanaweza kuathiri mtoto atakayezaliwa iwapo mwanamke atabeba ujauzito huku akiwa na upungufu wa folic acid. Madhara yake ni pamoja na mtoto kuzaliwa akiwa na mgongo wazi na kichwa kikubwa,” anabainisha Milinga.

Anaeleza kuwa lengo hasa la mradi huo ni kuhakikisha wanawake wanapata madini ya folic acid na kuongeza virutubishi katika vyakula mbalimbali kama vilivyotajwa hapo juu.

MPANGO JUMUISHI

TFCN pia imeanzisha mpango wa lishe jumuishi utakaohusisha sekta mbalimbali ili kusaidia upatikanaji wa lishe bora nchi nzima.

“Tumeanzisha mpango jumuishi wa kitaifa wa lishe unaoainisha ma- jukumu ya kila sekta. Mwaka 2016 tuliona ni muhimu kushirikiana na sekta zinazogusa moja kwa moja lishe, tumeungana na Wizara ya Elimu, Wizara ya Viwanda, kilimo, mifugo fedha na ofisi ya Tamisemi, haya ni mafanikio makubwa.

“Pia tunahamasisha kila halmashauri kuongeza bajeti ya lishe kutoka Sh 500 hadi Sh 1,000 kwa kila mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano,” anafafanua.

Dk. Leyna anasema pia wameanzisha kampeni ya Mkoba wa siku 1,000 itakayosaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza kiwango cha udumavu kwa watoto kuanzia wakiwa tumboni hadi wanapofikisha umri wa miaka miwili,” anasema Dk. Leyna.

Kwa mujibu wa Dk. Leyna, Mkoba huo utahusisha utoaji wa elimu ya lishe katika kaya zote nchini.

“Mkoba huu unajiendesha wenyewe kwa kuchangisha fedha za kutengeneza mikoba kwaajili ya kupeleka elimu kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa watoto tangu wakiwa tumboni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles