KILICHOMUUA DK. ANNA SENKORO

Dk. Anna Senkoro
Dk. Anna Senkoro
Dk. Anna Senkoro

LEONARD MANG’OHA NA ESTHER MNYIKA-DAR ES SALAAM


 

ALIYEKUWA mgombea urais kwa tiketi ya APPT Maendeleo katika Uchaguzi Mkuu wa 2005, Dk. Anna Senkoro, amefariki dunia kwa ugonjwa wa moyo.

Akizungumza kwa niaba ya familia, mkwe wa marehemu, Evance Mlay, aliliambia MTANZANIA kuwa Dk. Senkoro hadi anafikwa na umauti, alikuwa akisumbuliwa na tatizo la moyo kwa muda mrefu.

Alisema hali yake ilianza kubadilika Jumatatu iliyopita, wakampeleka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambako alipewa dawa na kurudi nyumbani.

“Leo asubuhi (jana) hali yake ilibadilika ndipo tulipompeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alipokewa katika kitengo cha ‘emergency’ (dharura) wakamfanyia vipimo, tukaambiwa amefariki,” alisema Mlay.

Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa MNH na taratibu za mazishi zinaendelea nyumbani kwa marehemu Tabata Segerea.

Dk. Senkoro aliyezaliwa Oktoba 18, 1964 ameacha watoto watatu na wajukuu wawili.

Siku chache baada ya Dk. Senkoro kugombea urais kwa tiketi ya APPT Maendeleo, alijiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kabla ya kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka juzi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here