23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Kenyatta ataja vipaumbele vita dhidi ya malaria

NAIROBI, KENYA

MWENYEKITI wa Umoja wa Marais wa Afrika wanaopambana na malaria (African Leaders Malaria Alliance – ALMA), Rais Uhuru Kenyatta, ametangaza vipaumbele vyake vinne vitakavyokuwa msingi wa juhudi za kutokomeza malaria kote Afrika ifikapo mwaka 2030.

Kenyatta ambaye aliteuliwa hivi karibuni katika mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika nchini Ethiopia, alisema vipaumbele hivyo vinavyotajwa kuleta mapinduzi makubwa, na kutafuta suluhu dhidi ya changamoto za mapambano ya kutokomeza malaria.

Alisema changamoto hizo zinajumuisha ushiriki hafifu wa wanawake, watoto na vijana, uhaba wa fedha toka sekta za ndani, za umma na binafsi pamoja na tishio la kudumaa kwa michango ya wahisani.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Nairobi, Rais Kenyatta alisema; “Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye vita hii ndani ya miaka kumi iliyopita, ili kuwa na Afrika tunayoitaka kama ilivyoelezwa kwenye mpango wa 2063 tusijisahau, badala yake tutafute na kupata rasilimali zaidi zitakazotusaidia kutokomeza malaria na kuokoa maisha.

“Na ndiyo maana tumeainisha maeneo ya vipaumbele yatakayokuwa msingi wa utendaji kazi wangu kama mwenyekiti wa ALMA ambayo ni matumizi ya dijitali na takwimu.”

Alizungumzia pia suala la uanzishwaji wa majukwaa ya kidijitali yanayofika katika mataifa mbalimbali ili kusaidia upatikanaji na uwazi wa takwimu za mapambano dhidi ya malaria.

“Hii itasaidia kwa kiwango kikubwa juhudi zetu hasa katika maeneo yaliyoathirika zaidi.

“Mbinu hii itasaidia pia kuwa na tafiti za ndani ya Afrika, hasa kwa kutumia taasisi za kitafiti zilizopo tayari ndani ya Afrika.

“Kwa kuimarisha upatikanaji wa takwimu, wananchi wote watakuwa na uelewa mzuri juu ya hatari zitokanazo na malaria na hivyo kuwawezesha kuchukua tahadhari mapema,” alisema Kenyatta.

Alisema kwa kushirikiana na viongozi vijana toka maeneo mbalimbali ya kiuongozi barani Afrika watajenga ‘Jeshi la Vijana’ dhidi ya malaria.

“Kikosi-kazi hiki cha mabalozi vijana kitaanzisha ushirikiano wa kisiasa, utafutaji wa fedha, ubunifu, utafiti na maendeleo na hata kuundwa kwa kada ya watu wanaopambana dhidi ya malaria,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles