23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wanajeshi wa Marekani waanza kuondoka Afghanistan

WASHINGTON, MAREKANI

MAOFISA wa Marekani wamesema mamia ya wanajeshi wa Marekani wameanza kuondoka nchini Afghanistan kama ilivyokuwa imepangwa awali.

Uondoaji askari wa Marekani unakuja wakati ambapo viongozi hasimu wa Afghanistan waliapishwa Jumatatu katika hafla mbili tofauti kama marais wa nchi, na hivyo kuibua wasiwasi kwa Marekani wa jinsi ya kuendelea na utekelezaji wa makubaliano ya kukomesha vita vilivyodumu kwa miaka 18.

Mvutano baina ya Rais Ashraf Ghani ambaye alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa Septemba mwaka jana na hasimu wake Abdullah Abdullah ambaye alielezea udanganyifu katika uchaguzi, unahatarisha kutumbukia tena katika machafuko.

Mvutano huo wa kisiasa umeyatia shakani mazungumzo ya ndani na kundi la Taliban ingawa Rais Ghani jana alisema ameanza kuunda timu ya majadiliano.

“Jukumu letu ni kuhakikisha amani na kumaliza miaka 40 ya vita. Nitahakikisha amani inarejea na ujasiri wa watu na mfumo wa Jamhuri,” alisema Rais Ghani wakati akiapishwa.

Msemaji wa Jeshi la Marekani nchini Afghanistan, Sonny Legget, alisema kwenye taarifa yake kwamba jeshi limeanza ‘kutimiza sharti la kupunguza wanajeshi hadi 8,600 ndani ya siku 135’.

Kati ya wanajeshi 13,000 wa Marekani walioko Afghanistan, 8,000 wanajihusisha na mafunzo na kuvishauri vikosi vya Afghanistan, wakati wengine 5,000 wakishiriki kwenye operesheni ya kupambana na ugaidi na kulisaidia jeshi la nchi hiyo pindi wanapohitajika.

Ghani alikuwa akijivuta kuwaachia wafungwa karibu 5,000 wa Taliban, kitu kilichokubaliwa kwenye mkataba wa amani wa Taliban na Washington.

Lakini jana Ghani aliahidi atatangaza amri ya kuachiliwa wafungwa, baada ya Marekani na maofisa kadhaa wa kigeni kuunga mkono juhudi hizo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo alipongeza hatua hiyo ya Ghani ingawa ‘alipinga vikali’ kuanzishwa kwa Serikali mbili mjini Kabul.

Pompeo alionya matumizi yoyote ya nguvu kusuluhisha tofauti za kisiasa.

Kundi la Taliban tayari limeyatuma magari yatakayowabeba wafungwa wanaotarajiwa kuachiwa, na pia wako tayari kuheshimu makubaliano kwa kuwaachia maofisa 1,000 wa Serikali waliokuwa wanawashikilia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles