23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Kenyatta amtumia JPM ujumbe akisikitishwa na kauli ya Jaguar

Mwandishi wetu – dar es salaam

RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta, amemtumia ujumbe maalumu Rais Dk. John Magufuli, unaoelezea msimamo wa Serikali yake kuhusu kukerwa na matamshi yaliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Starehe, Charles Njagua Kanyi, maarufu Jaguar.

 Ujumbe huo wa maandishi, uliwasilishwa jana na Balozi wa Kenya nchini, Dany Kazungu na kupokewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Magogoni Dar es Salaam. 

Akipokea taarifa hiyo, Majaliwa alisema Watanzania wamefurahishwa na hatua zilizochukulia na Serikali ya Kenya dhidi ya mbunge huyo, zinazodhihirisha kwamba matamshi hayo hayakuwa msimamo wa Serikali ya Kenya wala wananchi wake, bali ni msimamo wake binafsi.

Majaliwa alisema siku zote Watanzania na Wakenya wamekuwa huru kuishi na kufanya kazi au biashara katika nchi za Afrika ya Mashariki, na pale yalipotokea matatizo au kutokukubaliana, Serikali husika zilikaa mezani na kumaliza tofauti hizo.

“Uhusiano kati ya Kenya na Tanzania ni wa karibu mno na wa kidugu, kwani kuna baadhi ya makabila yapo katika nchi mbili hizi kama vile Wamasai na Wakurya na Wajaluo, hivyo ushirikiano katika masuala mbalimbali yakiwemo ya  kabiashara na ya kijamii haukwepeki,” alisema.

Majaliwa alitoa wito kwa viongozi na wananchi wa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kujiepusha na kauli zenye viashiria vya kujenga chuki, uhasama na migongano miongoni mwa wananchi, kwani kauli hizo zisipodhibitiwa mapema, zinaweza kusabisha hofu.

Alitumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania kuendelea kuishi kwa amani na upendo na ndugu zao wa Kenya na wageni wote kutoka nchi za Afrika Mashariki. 

“Mambo yetu yote katika nchi za Afrika Mashariki, hasa ya biashara na ya kiuchumi, kwa ujumla yataenda vizuri endapo tutalinda na kudumisha amani, bila amani tutaogopana na tutashindwa kabisa kushirikiana,” alisema Majaliwa.

Balozi Kazungu alimshukuru Majaliwa kwa kauli yake aliyoitoa bungeni jijini Dodoma, iliyowataka Watanzania kuwa watulivu na wayachukulie matamshi ya mbunge huyo kuwa ni msimamo wake binafsi na si wa Serikali ya Kenya.

Alisema msimamo wa Rais Kenyatta siku zote umekuwa ni kuwapokea na kuwakubali ndugu zao wote wanaotoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki walioamua kuishi au kufanya biashara nchini Kenya.

Mwanzoni mwa wiki iliyopita, Njagua ambaye pia ni mwanamuziki, alitoa matamshi ya kichochezi, akiwataka raia wa kigeni kutoka mataifa mbalimbali wanaofanya shughuli za kibiashara nchini Kenya, wakiwemo Watanzania, waondoke ndani ya saa 24 vinginevyo watawapiga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles