25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 21, 2023

Contact us: [email protected]

Mfanyabiashara aliyetekwa Dar alivyookotwa Mombasa

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

MFANYABIASHARA, Raphael Ongangi aliyedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana, amepatikana Mombasa nchini Kenya akiwa ametupwa karibu na nyumba ya shangazi yake aliyetambulika kwa jina la Doroth Osoro.

Taarifa za kupatikana Ongangi ambaye ni raia wa Kenya, zilithibitishwa jana mchana na mkewe, Veronica Kundya na baadaye Jeshi la Polisi Wilaya ya Kinondoni.

Ongangi alidaiwa kutekwa na watu wasiojulikana Juni 24, mwaka huu eneo la Oysterbay, Dar es Salaam akiwa na mkewe, Veronica.

Katika utekaji huo, walizuiwa na watu hao huku wakitoa bastola na kuwachukua wote wawili kabla ya kumwachia mkewe na baadaye wakaondoka na Ongangi.

Taarifa za kupatikana kwa mfanyabiashara huyo, zilianza kusambaa kwenye mitando ya kijamii jana mchana.

Akizungumza na MTANZANIA, Veronica alisema ni kweli mumewe amepatikana Mombasa nchini Kenya na tayari amezungumza naye kwa simu.

“Ni kweli mume wangu kapatikana na nimezungumza naye mwenyewe, yupo Mombasa, tumezungumza kwa kifupi ni mzima wa afya, nashukuru sana, sina taarifa nyingine zaidi ya hiyo. Zaidi namshukuru sana Mungu kupatikana kwa mume wangu akiwa hai.

“Kwa sasa siwezi kuzungumza mengi, zaidi namshukuru Mungu, pia nawashukuru Watanzania kwa kumwombea mume wangu apatikane na wengine kuwa karibu nami katika kipindi hiki kigumu,” alisema Veronica.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Kinondoni, Mussa Saibu, alisema ni kweli amepata taarifa za kupatikana kwa mfanyabiashara huyo kutoka kwa Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.

“Ni kweli nami nimeambiwa na Zitto muda mfupi uliopita na wanasema katupwa huko Mombasa karibu na nyumba ya shangazi yake anayeitwa Doroth Osoro, ameachwa hapo.

“Sasa ndio tutajua kama alitekwa au hakutekwa baada ya kumhoji na kama hajui chochote basi atakuwa hakutekwa,” alisema Kamanda Saibu.

Alipotafutwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola kama ana taarifa za kupatikana kwa mfanyabiashara huyo, alisema hana taarifa na kwamba yuko safarini.

“Sina taarifa hizo, kwa sasa nipo safarini, ngoja kwanza niwasiliane na Jeshi la Polisi halafu nitarudi kwako,” alisema Lugola.

Ongangi amepatikana ikiwa imepita siku moja tu tangu Zitto alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo lililomkuta rafiki yake huyo wa karibu ambaye miaka ya nyuma alikuwa msaidizi wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles