24.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 27, 2021

Katoliki wafanya mabadiliko maeneo nane kukabili corona

MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

BARAZA la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini (TEC) limefanya mabadiliko katika maeneo nane ya jinsi ya kutekeleza majukumu yake ya kiroho ikiwamo kuendesha ibada,ikiwa ni njia ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona kwa waumini wake.

Uamuzi huo wa Kanisa Katoliki umekuja  katika wakati ambao idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona imepanda kwa kasi na kufikia 94 kati yao 62 wakiwa wamebainika ndani ya wiki moja.

Mbali na hatua ilizochukua mwanzo kama kuweka utaratibu kwa waumini wake kunawa mikono na kuweka umbali kati ya mtu na mtu wakati wa ibada, kanisa hilo sasa limekwenda mbali na kutangaza kuzuia mikusanyiko ya waimba kwanya na wale wanaofanya mafundisho ya sakramenti mbalimbali.

Pamoja na hayo pia limetoa mwongozo kwa makasisi wake wanaoendesha ibada kwa kujikinga kwa dawa, hali kadhalika vifaa wanavyotumia kama microphone, kupunguza muda wa ibada, na zaidi limesitisha sherehe za ndoa.

Taarifa iliyotolewa juzi na kusainiwa na Katibu Mkuu wa TEC, Padri Charles Kitima, na kabla ya hapo mahojiano yaliyofanyika kati yake na gazeti dada la hili la MTANZANIA, TEC imefikia uamuzi huo  kutokana na kile ilichosema kuwa maambukizi mengi ya virusi vya corona yanaonekana pia kutoka kwenye misongamano ya watu wengi.

KWAYA/MAFUNDISHO

Kuhusu kwanya TEC imetangaza kusitisha mazoezi ya yanayofanyika kwenye mikusanyiko  pamoja na uimbaji wa kwenye ibada.

Kwa  mujibu wa taarifa hiyo ya TEC, vilevile imesitisha mafundisho ya dini kwa watoto na makundi mengine kwa njia ya mikusanyiko.

“Mafundisho yanaweza kufanywa kwa njia nyingine mfano kuelekeza watoto wajisomee Katekisimu ama njia nyingine za mitandao”.

Pamoja na hilo, TEC pia imewataka wanaoidhinisha ibada waangalie suala la muda, kwamba ibada zisiwe ndefu.

“Tunaomba waidhinishaji wa ibada na huduma mbalimbali za kikatoliki wazingatie masharti ya umbali kati ya mtu na mtu, matumizi ya microphone, kunawa mikono kabla ya kuingia kanisani pia kunyunyiza dawa vifaa vya ibada.

“Na yule anayetoa huduma ajikinge kwa umakini na kuongozwa na ueledi husika kiafya kadri ya majukumu yake mfano kuwahudumia wagonjwa , kuendesha ibada ya mazishi nakadhalika,” inasomeka taarifa hiyo.

Pia TEC imewataka maketekista  wanaokaa na wahitaji wa huduma za kiroho waeleweshwe na kupewa vifaa kujikinga, kufanya usafi na unyunyizaji dawa.

HATUJAZUIA NDOA,TUMESITISHA SHEREHE

Kanisa hilo pia limesema halijasitisha ndoa, bali kilichozuiliwa ni sherehe zinazoambatana na tukio hilo ili kuepuka kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Limewashauri waumini wake kama kuna uwezekano wasogeze mbele matukio mbalimbali hadi janga hilo liishe ili waje kufanya pamoja na sherehe.

Akizungumza na gazeti dada la hili la MTANZANIA Juzi Katibu Mkuu  huyo wa TEC, Padri Kitima, alisema sakramenti zitaendelea kutolewa kwa kuzingatia maelekezo ya kitaalamu.

“Kuna sakramenti nyingine kama mtu amekaribia kufa huwezi kumnyima ubatizo, huwezi kumnyima kupokea sakramenti ya ndoa, lazima itatolewa, unakuta (mtu) ni mgonjwa na padri ameelekezwa namna ya kutoa (sakramenti) kulingana na mazingira asiambukizwe na asiambukize wengine,” alisema Padri Kitima.

Alisema kuna mazoea ya watu kuingiza shamra shamra ambayo ni hulka ya binadamu, lakini akasisitiza kuwa zinahatarisha zaidi kazi ya kuzuia maambukizi.

“Kama unadhani lazima mtoto wako apate ubatizo, kipaimara hakuna shida, masharti ndiyo hayo, au nyie wachumba wawili mnasema tulishapanga kufunga ndoa mwezi wa nne, mje kanisani mtafunga mko wawili na wasimamizi kwa umbali wa mita moja moja, lakini hakuna sherehe,” alisema Padri Kitima.

Alisisitiza katika kupambana na janga la corona, waumini wote wazingatie Serikali inaagiza nini katika kufanya shughuli za kikatoliki.

“Katika vita hivi tunaongozwa na sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali, maelekezo ya Wizara ya Afya na mengine yanayotolewa na waziri mkuu, hivyo kikanisa huo ndio utaratibu tunaoufuata.

“Serikali imesema zingatia umbali wa mtu na mtu katika kutoa huduma yoyote zingatia umbali, kuna ‘physical’ na ‘social distance’, kuna huduma zingine ambazo tumezizoea na tuna desturi zetu kama kanisa.

“Sakramenti inaleta furaha, amani, mshikamano wa kijamii, inaunganisha familia, koo, huwezi kusema wasije watu wengine katika saktramenti kama hii… tafsiri iliyotolewa haikuwa sahihi,” alisema Padri Kitima.

WATOTO

Alisema pamoja na uhitaji wa kutoa mafundisho ya kidini kwa watoto, ni vyema wazazi na walezi wakazingatia kutowakusanya pamoja.

“Kwa mfano nimemsikia waziri mkuu ameongea tusikusanye watoto kanisani ili kuwapa mafundisho ya dini, maparoko wameshatoa taratibu mbalimbali, wazazi fundisheni watoto na fanyeni sala na watoto kwenye familia mkiwa mmekaa mbalimbali.

“Watoto ni wengi na huwezi ‘kuwa–control’, mwingine ana umri mdogo haelewi ni kwanini asikaribie kwa mkubwa wake, kwa dada yake au kwa kaka yake na ukimzuia anaanza kulia.

“Kwahiyo unapokwenda kanisani umekaa naye karibu, ukikohoa unamwambukiza, sasa isiwe sababu ya wewe kwenda kusali ukamwambukiza mtoto wako,” alisema Padri Kitima.

Alisema pia hivi sasa maaskofu wanatakafari zaidi kuhusu kuboresha mazingira mengine ya sala ili kuhakikisha ibada zilizo na umuhimu mkubwa katika kupambana na corona zinawekewa taratibu mbalimbali.

“Mfano kama ibada ilikuwa inachukua masaa mawili na nusu kwanini tusiifanye iwe ya saa moja, kadiri unapowaweka watu muda mfupi unapunguza hatari ya maambukizi,” alisema Padri Kitima.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,310FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles