24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

KARIBU SAGCOT SULUHISHO KWA WAKULIMA WETU

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

SAGCOT ni kifupi cha maneno yenye maana ya Southern Agricultural Growth Corridor Growth of Tanzania, tafsiri yake ni Mpango wa Kuboresha Kilimo Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini,  ambao ilianzishwa miaka mitatu iliyopita, lengo kubwa likiwa ni kusaidia uwekezaji mkubwa na mdogo katika kilimo kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Kwa muda mrefu wakulima wengine nchini wamekuwa wakilalamikia hatua ya ukosefu wa wataalamu ambao wanaweza kupandisha mazao yao na hata kuimarisha uzalishaji kwa wingi.

Na ili tuweze kufikia huko, ni lazima kuwepo na makakati madhubuti  ikiwemo kwa wakulima kupatiwa mbegu bora  pamoja mbolea ambayo itafanikisha kupata mazao yaliyo bora, ili kuwawezesha kupata masoko ya  uhakika  nje ya nchi .

Katika  hili Serikali ina wajibu wa kuhakikisha kuwa wakulima waliopo vijijini wanapewa kipaumbele kwa kupatiwa mbegu bora pamoja na mbolea kwa wakulima hao, ili waweze kuzalisha mazao kama mpunga, viazi na mahindi   kwa kiwango kikubwa.

Kutokana na mpango kabambe wa SAGCOT, Serikali ya Uholanzi imeingiza nchini aina 14 ya mbegu za viazi kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kuboresha maisha ya wakulima kupitia mradi wa kuboresha zao la viazi nchini.

Kwa mujibu wa Mshauri wa Kilimo wa Ubalozi kwa nchi za Kenya na Tanzania, Bert Rikken, nchi yake imeona Tanzania ina nafasi kubwa ya kuongoza uzalishaji wa viazi kutokana na ukubwa wa ardhi na hali ya hewa.

Wameamua kuingiza mbegu hizo ili kuongeza uzalishaji kwa sababu wakulima wanazalisha chini ya tani nane hadi 10 kwa hekta, hivyo ujio wa mbegu hizi utasaidia kuongeza uzalishaji na kufikia tani 40 kwa hekta.

“Mbegu hizi ni nzuri kwa matumizi mengi, viazi vyake vina ladha nzuri na vinaweza kutumika kutengeneza chips au bidhaa nyingine zitokanazo na viazi ambazo zinaweza kusafirishwa nje ya nchi. Mradi huu ulianza kwa kutiliana saini mawaziri wa kilimo kutoka Tanzania na Uholanzi mwaka 2016, ili kuruhusu mbegu kuingia nchini ili kupata ithibati,” anasema Rikken.

Mradi huo wa miaka mitatu utakaogharimu kiasi cha Euro 388,000 sawa na Sh milioni 700, utahakikisha Tanzania inapata mbegu mpya za zao hilo na kutoa mafunzo kwa taasisi zinazojihusisha na kilimo nchini ili kuongeza uzalishaji.

Kutokana na mkakati huo kabambe, Kaimu Mthibiti Mkuu wa Mbegu kutoka Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI), Dk. George Swella, anaeleza kuwa kazi yao kubwa ni kuhakikisha mradi unafanikiwa kwa kusimamia mchakato wa kupima mbegu zilizoingizwa nchini kutoka Uholanzi ili kujua kama zinaendana na mazingira ya Tanzania.

Akieleza faida za ujio wa mbegu hizo, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Twahir Nzallawahe, alisema kwa sasa Tanzania imekuwa na matumizi makubwa ya viazi hasa kwa chips, hivyo haja ya kuongeza uzalishaji ni wazo mwafaka kwa kipindi hiki.

Anasema viazi mviringo ni zao muhimu kwa uchumi na mustakabali wa usalama wa chakula nchini, mchango wa viazi mviringo kwa Watanzania wa Nyanda za Juu Kusini na Kaskazini ni mkubwa hasa katika mnyororo wa kuongeza thamani kwa sababu mahitaji ya zao hili ni makubwa kutokana na ongezeko la walaji wa chips mayai na chips kuku.

Kwa upande wake, Naibu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mpango wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Jennifer Baarn, aliwahakikishia wajumbe ushirikiano wa kutosha kuhakikisha mradi unafanikiwa.

Kwa muda mrefu wakulima wa viazi nchini wamekuwa wakitegemea mbegu zilizoandaliwa kienyeji hadi ilipofika mwaka 2013, Serikali ya Finland ilipofanikiwa kuingiza aina nne ya mbegu ambazo ni Asante, Sherehekea, Tengeru na Meru.

Kwa hakika ujio wa SAGCOT unafungua neema kwa wakulima wadogo, kati na hata wakubwa ambapo kila mmoja atanufaika kwa uzalishaji ulio bora na wengi kuzingatia tija kwa watu wote.

Karibu SAGCOT ufungue milango kwa wakulima wa Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles