23.1 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

Kampuni sita zimesaini kununua korosho-Waziri

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda amesema Serikali imesaini mikataba ya awali na makampuni sita ya kununua korosho.

Amesema Watanzania hawana desturi ya kula korosho ambazo zinaongeza heshima ya ndoa akitoa mfano mikoa ya kusini jinsi wanavyozaliana kwa wingi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana,  Kakunda alisema Serikali imeendelea kusaini mikataba ya awali na  makapuni ya ununuzi wa korosho ambayo hakuyataja majina.

“Tumeendelea kusaini mikataba mingine na makampuni mengine, mikataba ambayo tumeisaini ni ya awali.

“Mpaka sasa   tumesaini na makampuni sita nisingependa kuyataja kwa majina kwa sababu tunajua hali halisi ya makampuni ya korosho watu wanafuatiliana, wanaharibiana biashara pamoja na majina.

“Lakini kuna kampuni moja tuliikaribisha wiki iliyopita imekuja kukagua maghala ya korosho wamejiridhisha kwamba korosho yetu ni safi na haijaharibika na tumepeleka kwenda kuhakiki TBS na wameenda kufanya uhakiki katika nchi yao na wamejihakikishia kwamba ni nzuri na wanajiandaa kulipa.

“Hawa mabwana wakilipa tunawakabidhi korosho mara moja,”alisema Waziri Kakunda.

Akitoa ripoti ya maagizo aliyoagizwa na Rais Dk. John Magufuli wakati akiapishwa, Novemba 12 mwaka jana ya kusimamia ununuzi wa korosho, Kakunda alisema tangu   Novemba 13 mwaka jana hadi Mei 15 mwaka huu zimeweza kukusanywa tani  225,000.

“Kati ya hizo tani 2,200 zinaendelea kubanguliwa na viwanda  vya ndani kwa mikataba maalum. Maana yake zinabaki tani 228,000 katika maghala.

Alisema walipokea maombi ya kampuni 38 kwa ajili ya ununuzi wa korosho ambako maombi ya kampuni saba yalikuwa ya ndani na 27 kutoka nje ya nchi.

“Hayo makampuni yote yaliandika barua kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara ama kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mazao Mchanganyiko ambayo ipo chini ya Wizara ya Kilimo na kila aliyeleta barua aliitwa kwa ajili ya mazungumzo.

“Wale ambao wamefikia makubaliano ya bei walisaini mkataba wa awali,”alisema.

Kuhusiana na kampuni ya Indo Power Solution kuwa ni ya utapeli, Waziri Kakunda alidai taarifa hizo siyo za kweli.

“Kila tuliyekubaliana naye bei tulisaini naye mkataba, Kampuni ya kwanza kusaini mkataba ilikuwa Indo Power Solution ya   Kenya ambayo ilisaini mkataba tarehe 30 mwezi 11 mwaka 2018 yule Mkurugenzi wa Indo Power Solution alisaini na Mkurugenzi wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko mkoani Arusha na sisi tulikuwa mashahidi.

“Wizara yangu kupitia mimi ndiyo niliwaalika na Waziri wa Sheria na Katiba wakati huo alikuwa Profesa (Palamagamba) Kabudi na nilimwalika mahususi kwa sababu mkataba ule ulifanyiwa mapitio kwa kina na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambayo ipo chini yake.

“Nilimwalika Gavana wa Benki Kuu (BoT) ambaye malipo yote ya korosho yatapitia benki kuu kwa hiyo kumwalika ilikuwa ni sahihi na Naibu Waziri wa Kilimo Innocent  Bashungwa walikuwa kama sehemu ya wahudhuriaji.

 “Kilichonishangaza mimi wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara ni baadhi ya wabunge kupeleka lawama kwa Kabudi kwamba yeye ndiyo amemshauri Rais…nakanusha, Kabudi hakuhusika wala hatukuwa tumempelekea,”alisema.

Alisema sababu ya kusimamisha mkataba na Kampuni ya Indo Solution ni kutokana na kukiuka matakwa yaliyokuwepo kwenye mkataba.

“Indo Power Solution kwenye mkataba ule aliahidi kulipa tani 100,000 ndani ya siku 10, baada ya siku tano kupita akatoa taarifa  kwamba alikuwa anaomba aongezewe muda badala ya siku 10 iwe mwezi mmoja, tukampa.

“Baada ya mwezi mmoja akaomba tena aongezewe muda, sasa baada ya miezi miwili tarehe 30 ya mwezi wa tatu 2019 timu ya wataalamu ya ushauri ya Serikali ilipendekeza tusimamishe mkataba ule kwa sababu hauwezi kuwa na tija kwa sababu mnunuzi hakuweza kutimiza masharti.

“Na hilo siyo jambo la ajabu kama unashindwa masharti unaondolewa ile kampuni siyo ya utapeli ni kampuni halisi ambayo ipo mkienda Thika mtaikuta balozi wetu na wa Kenya  walithibitisha ni kampuni halali.

“Kushindwa kununia mzigo wa tani 100,000 siyo sababu kwa sababu  inafanya shuhuli zake kwa halali pale Kenya,”alisema.

Katika hatua nyingine, Kakunda alisema Watanzania wengi hawana desturi ya kula korosho.

“Watanzania wengi hawali korosho, ukiangalia manufaa ya korosho ni mengi, kwa sababu  unafikiri kwa nini kusini angalau wenzatu wanazaliana sana, korosho inaongeza rutuba kwa mwanaume.

“Tunazungumza ukweli ukimuuliza Dk. Ngugulile (Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wazee na Watoto) ambaye ni daktari wa binadamu atakwambia manufaa ya korosho ambayo ni kuongeza virutubisho kwa mwanaume kuweza kutotoa watoto wengi hiyo ni sifa mojawapo na kurudisha heshima ndani ya nyumba watu hawataki kula mpaka waandikiwe na daktari,”alisema Waziri Kakunda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,717FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles