23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 27, 2023

Contact us: [email protected]

Serikali kupitia upya mashamba yaliyofutwa

Munir Shemweta-KILOSA

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi,  amesema wizara   itapitia upya mashamba yote yaliyofutwa na Rais katika Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.

Lukuvi  alikuwa akizungumza   na wananchi wa Kata  ya Chanzulu, Wilaya ya Kilosa   alipokwenda kutatua mgogoro wa ardhi katika wilaya hiyo ikiwa ni jitihada za wizara kumaliza migogoro ya ardhi nchini.

Alisema katika maeneo mbalimbali yapo mashamba yaliyofutwa na Rais lakini hayajawekewa utaratibu  wa kuyatumia na hivyo kutoa fursa kwa wajanja wachache kujigawiwa na mengine kuyauza kwa wananchi bila kufuata utaratibu.

Alisema katika kuhakikisha mashamba yote yaliyofutwa na Rais katika Wilaya ya Kilosa na kuzua mgogoro baina ya wananchi na wamiliki,  wizara  imeamua kupeleka timu kutoka wizarani kwa ajili ya kuyafanyia uhakiki mashamba yote yaliyofutwa katika wilaya hiyo.

Kwa mujibu  wa Lukuvi, timu hiyo inajumuisha Kamishna wa Ardhii,  Mary Makondo, Kaimu Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Samweli Katambi, Mthamini Mkuu wa Serikali Evalyne Mugasha, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Kati Ezekiel Kitlya na wataalamu kutoka Idara za Mipango Miji wizarani.

Alisema  uamuzi wa kwenda na timu kutoka wizarani unalenga kumaliza  migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo hasa baada ya kubaini ofisi za wilaya na Mkoa wa Morogoro kushindwa  kutatua mgogoro huku viongozi wa wake wakituhumiwa.

Waziri   alitaja kazi kubwa itakayofanya timu hiyo kuwa ni kupitia  mashamba 15 yaliyofutwa na rais  na kufufua mipaka ya mashamba hayo na kazi hiyo itafanywa kwa na ushirikiano wa ngazi za wilaya.

“Tutayapitia mashamba yote yaliyofutwa na rais na kujua kilichomo ndani yake na timu ya uhakiki niliyokuja nayo itanilitea mapendekezo ya namna ya kutumia mashamba na mengine watapewa wanaostahili na si kila mtu atapewa,” alisema Lukuvi

Huku akishangiliwa na wananchi wa Chadulu, Lukuvi alisema wale wote waliojimilikisha mashamba yaliyofutwa na  Rais watanyang’anywa na kupatiwa wanaostahili na mengine yatatolewa kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa ajili ya kupatiwa wawekezaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,729FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles