23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

JPM yupo tayari kumpa kazi Lissu

 WAANDISHI WETU -DAR/MIKOANI

MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli amewataka wananchi wa Ikungi mkoani Singida kumshauri mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu asihangaike kugombea nafasi hiyo na kwamba atampa kazi serikalini.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana akiwa katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika Ikungi mkoani Singida.

“Ndugu zangu wa Ikungi hatuchagui sura bali tunachagua maendeleo, najua kuna mgombea anatoka hapa, mshaurini mwambie tutampa kura Magufuli yeye nitampa kikazi serikalini, si lazima wote tuwe rais.

“Mshaurini nitampa kazi serikalini ni mtoto wetu tunampenda wala hatuna tatizo, na mimi ndugu zangu sina tatizo na mtu yeyote, kwani kazi lazima uwe rais? Mwache Rais Magufuli sisi tutakupa kikazi utakachoweza kufanya kwa sababu sisi wote ni wamoja, akija mwambieni Magufuli atakupa kazi kwanini uhangaikie hii kazi ambayo hutashinda?” alisema Rais Magufuli.

KUZAA KWA MPANGO 

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alisema hakuna haja ya watu kuzaa kwa mpango kwa kuwa Serikali yake inatoa elimu bure. 

“Tunataka watoto wasome bure, ndio maana siku zote nilikuwa nasema zaeni, hakuna kuzaa kwa mpango, matiti ya kunyonyesha watoto tunayo, maziwa tunayo na wanaume wapo, wakina mama wapo na shule wanasoma bure, Serikali ipo,” alisema Rais Magufuli.

Vilevile aliwataka wakazi wa Ikungi na Watanzania kwa ujumla bila kujali tofauti za vyama vya siasa, kumpigia kura ili Serikali yake iendelee kutoa elimu bure.

“Asije akaja mwingine akageuza, badala ya kutoa elimu bure watoto wakaanza kudaiwa, tutakuwa tunarudi nyuma.

“Kwa nini turudi nyuma tulikotoka? Na ndio maana tunasema katika miaka mitano ijayo, tutatoa elimu bure, ndio maana tunaomba ndugu zangu mturudishe,” alisema Rais Magufuli.

MIRADI YA MAENDELEO SINGIDA 

Akihutubia katika viwanja vya Bombadier mjini Singida, Rais Magufuli alisema katika miaka mitano ya utawala wake Sh bilioni 470.4 zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Singida. 

Baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa hospitali na vituo vya afya uliookoa maisha ya kina mama 730 ambao walifanyiwa upasuaji, ujenzi wa barabara, madaraja, makaravati, kuweka taa za barabarani na mingine.

“Nitashangaa sana kama watu watakuja watapita kwenye barabara hizi leo, wapite wamtukane Magufuli, Singida mimi ninaijua na ninyi mnaijua.

“Barabara ya kutoka Singida hadi Mwanza ilikuwa ni ndoto, barabara ya Singida, Manyoni, Dodoma kilomita 45 haikuwepo. Barabara ya kutoka Mkiwa itaunganishwa na Mbeya nayo tutaichapa tu.

“Ndiyo maana nimekuja hapa kuomba kura ili tukatekeleze kazi iliyobaki, mtupe tena miaka mitano tukatekeleze yale tunayotaka kufanya… msije mkafanya majaribio ya miaka mitano, ni lazima mchague watu wenye upendo na ninyi,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema Sh bilioni 213 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa barabara, madaraja, makaravati na kwamba miongoni mwa barabara hizo ni ile ya Manyoni – Itigi – Chaya.

Aidha alisema barabara ya Chaya – Tabora kilomita 85 inaendelea kujengwa na hivi sasa zimebaki kilomita 20 ikamilike.

Dk. Magufuli alisema pia Sh bilioni 17 zimetumika Singida Mjini kwa ujenzi wa barabara ya Karume – Boma – Kinyeto – Misuna stendi – Majengo na kuweka taa za barabarani.

Alisema kuongoza nchi ni kazi kubwa na kuwataka Watanzania kutafakari mahali walipotoka, walipo na wanakoelekea kwa mustakabali wa taifa.

“Watu wanahitaji maisha yaliyo bora, kama ni huduma za afya wanazitaka, huduma za elimu wanazitaka, sisi tunataka maendeleo kwa Watanzania wote bila kubagua dini, vyama, ndiyo maana tunawaomba mtupe kura za kutosha.

“Tunataka taifa hili liendelee kwenda mbele, ninawaomba tena kwa mara nyingine niwe rais wenu,” alisema Dk. Magufuli.

KURA ZA WABUNGE, MADIWANI

Dk. Magufuli aliwaomba wananchi wa Mkoa wa Singida kuwachagua wagombea wote wa ubunge na udiwani ili ashirikiane nao kuwaletea maendeleo.

“Kufanya kwangu kazi nzuri kunategemea waheshimiwa wabunge mtakaowachagua, nataka niwaambie kwa ukweli msinichanganyie,” alisema Dk. Magufuli.

Awali, akizungumza katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Sokoni, Dk. Magufuli alisema miaka mitano iliyopita ilikuwa ni onja onja na kuahidi kuwa ijayo atachapa kazi isiyo na kifani huku akiwaomba wakazi wa Bahi kumpa kura za kutosha aweze kumalizia kazi aliyoianza.

Alisema ataendeleza jitihada za kuboresha elimu, vituo vya afya, kujenga shule, madarasa na huduma zote za kijamii kwa kukamilisha alipoishia. 

“Miaka mitano iliyopita nilipita Bahi nikawaomba kura kwa lengo moja tu la kuleta maendeleo katika nchi yetu, mikoa na wilaya zetu.

“Ninajua yako mengi ambayo yamefanyika na ninyi ndiyo mashahidi, ninajua yaliyofanyika mji wa Bahi haikuwa hivi, sasa hivi mji umepanuka unapendeza,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano ijayo ataendeleza jitihada kwa kukamilisha pale alipoishia.

“Tutaendelea kuboresha elimu, vituo vya afya, kujenga shule na madarasa na huduma zote za kijamii,” alisema Dk. Magufuli.

Aliahidi kumalizia kupeleka umeme katika vijiji 16, kufanya upembuzi yakinifu wa mradi wa maji Ibimwa na Bankolo ili kuchimba visima virefu.

“Miaka mitano iliyopita vijiji vinne tu vilikuwa na umeme, vilivyobaki vyote vitakuwa na umeme ndani ya miaka mitano,” alisema Dk. Magufuli. 

LISSU AAHIDI NEEMA MWANZA

Kwa upande wake, mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu ameahidi kuweka mazingira rafiki na sera wezeshi kwa wakulima wa mazao ya biashara ikiwemo zao la pamba kulipwa kwa wakati ili waweze kunufaika na kazi ya mikono yao.

Lissu aliyasema hayo jana wakati akiwa jijini Mwanza kuendelea na kampeni za kukinadi chama chake kuelekea uchaguzi mkuu wa kuchagua rais, wabunge na madiwani.

Alisema zao la pamba ambalo ni maarufu la biashara mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa sasa limeshuka thamani na kugeuka kuwa zao la mikopo kwani wakulima hawalipwi kwa wakati na siyo kumbilio la wanyonge tena.

Lissu alisema Chadema itahakikisha inarejesha thamani ya zao la pamba ili kuwanufaisha wananchi wa Kanda ya Ziwa.

 Alisema atahakikisha wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa wananufaika na uwepo wa Ziwa Victoria kwa kuwapa sera rafiki wavuvi badala ya kuchoma nyavu zao.

Lissu alisema miaka ya nyuma Mkoa wa Mwanza ulikuwa na viwanda tofauti vilivyokuwa vinaliingizia taifa kipato na kutoa ajira kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa, lakini hivi leo vimekufa.

Alitolea mfano viwanda vya nguo ambavyo siyo tu vilitoa ajira bali pia vilisaidia kuongeza thamani ya zao la pamba na kuwasaidia wakulima kujikwamua kiuchumi.

Lissu aliahidi kurejesha usimamizi wa viwanda na kuvifufua upya ili kuwapa fursa Watanzania ikiwemo wakazi wa Kanda ya Ziwa kufaidi fursa mbalimbali zitakazotokana na viwanda hivyo.

Aliwaahidi pia wafanyabishara kuifanya TRA kuwa mamlaka itakayosaidia kuendeleza uchumi wa nchi ili Serikali na wananchi wake wote wafaidike.

Pia alisema atahakikisha anaweka sera rafiki kwa benki zote nchini kufanya kazi ili ziwe na msaada kwa Watanzania wajasiliamali na kuziwezesha taasisi zote kukua zaidi.

Aidha Lissu aliahidi kujenga majengo ya biashara (mall) kwenye kila kituo cha mabasi ili wafanyabiashara wadogo na wakubwa wapate fursa ya kununua na kuuza bidhaa zao akitolea mfano mkoa wa mwanza ambao ni maarufu kwa mazao ya dagaa na samaki.

Lissu aliahidi kuwaongezea walimu mshahara kila mwaka ili waweze kuwa na maisha mazuri.

 HABARI HII IMEANDIKWA NA NORA DAMIAN (SINGIDA), FLORA MATIMO NA YOHANA SHIDA (MWANZA).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles