22.6 C
Dar es Salaam
Saturday, May 21, 2022

JPM: Kazi ilikuwa ngumu

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

RAIS Dk. John Magufuli ameelezea ugumu waliopitia kuwapata wagombea wa ubunge akisema iliwalizimu kutumia taarifa nyingi kuwajadili kwa muda mrefu ili wale watakaopitishwa wawe wenye uwezo.

Pia alisema alipitia majina ya wagombea wote 10,367   waliochukua fomu na walioteuliwa ni wale wenye uwezo wa kuongoza, wazalendo, wenye kujitoa kwenye chama, wanaofahamu mahitaji ya wananchi, wenye utayari wa kuwatumikia wananchi na wenye kukubalika kwa wananchi.

Kauli hiyo aliitoa jana jijini hapa wakati akifungua kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichokuwa na jukumu la kufanya uteuzi za mwisho wa majina ya wagombea wa nafasi ya  ubunge katika majimbo mbalimbali.

Rais Magufuli ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, alisema katika vikao walivyokaa kwa siku mbili (Agosti 18 na 19) walijadili majina ya wagombea kwenye ngazi ya Kamati ya Usalama na Maadili na kisha Kamati Kuu kwa uchambuzi wa kina.

Alisema yeye alipitia na kuyasoma majina ya wagombea  wote 1,0367 na kwamba kwamba amekuja na mabegi ili kama kuna mtu atataka kupewa ufafanuzi apewe bila shida yoyote.

“Napenda niwahakikishie uchambuzi wa kina ulifanyika kwelikweli, tulitumia taarifa nyingi ambazo tulizipata kutoka katika vyanzo mbalimbali. Na mimi nataka kuwathibitishia wajumbe nimesoma majina yote 1,0367.

“Na hapa nina mabegi, mengine tunayo huko nyuma (huku akionyesha nyuma alipokuwa amekaa), hebu yainue hayo mabegi pamoja na lingine lipo pale, kwa yule atakayetaka ufafanuzi, kwa mtu yeyote ambaye anataka apewe ufafanuzi wa kina atapewa,” alisema Rais Magufuli.

SABABU YA VIKAO VYA SIKU MBILI

Alisema sababu ya Kamati Kuu kukaa kwa siku mbili ni kurahisisha kazi ambayo ilitakiwa kufanywa na Halmashauri Kuu ya Taifa jana, na pia hawakutaka kumpendelea mtu yeyote kwa sababu kila mmoja ana haki sawa.

“Lakini Kamati Kuu tulikaa vizuri sana na ndiyo maana tumetumia siku mbili ili kurahisisha kazi ambayo ninyi mtaifanya leo (jana). Tulifanya hivyo, kwanza hatutakuwa tumempendelea mtu ama kumnyima mtu haki yake kwa sababu kila mmoja ana haki yake,” alisema Rais Magufuli.

Vilevile alisema iliwalazimu kuwajadili wagombea kwa muda mrefu ili watakaopitishwa wawe wenye uwezo wa kuipeperusha vyema bendera ya nchi na kukipa chama ushindi.

 “Lakini pia ilitulazimu kutumia taarifa nyingi na kuwajadili wagombea kwa muda mrefu ili watakaopitishwa wawe watu wenye uwezo wa kuipeperusha vyema bendera yetu na kukipatia chama ushindi mkubwa ili kiendelee kuongoza nchi yetu,” alisema Rais Magufuli.

Alisema sababu nyingine ni kutokana na unyeti wa nafasi ya ubunge kwani ndio wasemaji wa wananchi ambao pia wana jukumu la kuisimamia Serikali.

“Tatu ilitubidi kufanye uchaguzi wa kina kwa sababu ya unyeti wa nafasi wanazogombea, kama mnavyojua nafasi ya ubunge na uwakilishi ni nyeti na muhimu sana.

“Wabunge na wawakilishi ndio wasemaji wa wananchi, pia wana jukumu la kusimamia Serikali, hivyo basi ilikuwa ni lazima tujiridhishe tutakapowapitisha watakuwa na uwezo wa kutimiza majukumu hayo.

“Lakini zaidi ya hapo kama mnavyofahamu wabunge na wawakilishi ndimo atakapopatikana Waziri Mkuu, na miongoni mwa hao ndimo atakapopatikana Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, lakini pia mawaziri na manaibu. Lakini pia spika na manaibu spika na wenyeviti wa Serikali zote mbili.

“Hivyo ilitulazimu tuwajadili kwa kina ili tujiridhishe kuwa wale tutakaowapitisha wana sifa za kuwa viongozi na wanafahamu dira na sera ya nchi yetu, za chama chetu,” alisema Rais Magufuli.

WAGOMBEA WENYE SIFA ZINAZOHITAJIKA

Aliipongeza Kamati Kuu kwa kazi kubwa waliyofanya kwa siku mbili kwani wamejitahidi kupata wagombea wenye sifa, wenye kujitoa na ambao wanawatumikia wananchi na wanakubalika kwa wananchi.

“Nitumie fursa hii kuishukuru sana Kamati Kuu kwa kazi kubwa waliyofanya kwa siku mbili, nitumie fursa hii kuwahakikishia ndugu wajumbe kuwa Kamati ya Usalama na Maadili pamoja na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu zimejitahidi kuchambua na kupata wagombea wenye sifa zinazohitajika.

“Ikiwemo kupata wagombea wenye uwezo wa kuongoza, wazalendo, wenye kujitoa kwenye chama, wanafahamu mahitaji ya wananchi wenye utayari wa kuwatumikia wananchi  na watanzania wote na pia wenye kukubalika kwa wananchi,” alisema Rais Magufuli.

NENO KWA WAJUMBE

Hata hivyo, Rais Magufuli alitoa wito kwa Halmashauri Kuu ya Taifa kupitisha majina ya wagombea wenye sifa na kutoweka udini, ukabila, undugu na ukanda.

“Wito wangu kwenu tujadili kwa umakini mkubwa na kumtanguliza Mungu mbele na pia kutanguliza mbele  masilahi ya chama na taifa letu, tusiweke mbele undugu, urafiki, ukanda au udini bali uwezo wa mtu kuongoza na hivyo ndivyo waasisi wa chama hiki walivyotufunza na huo ndio msingi wa kukifanya chama chetu kizidi kuaminiwa,” alisema Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine, alisema jumla ya wanachama 43,461 wamejitokeza kuwania nafasi mbalimbali huku 10,367 wakichukua fomu za kuwania ubunge.

 “Wana CCM waliojitokeza kugombea katika Baraza la Wawakilishi walikuwa 786 na waliojitokeza kuwania nafasi za udiwani katika kata, wadi na viti maalumu ni  33,094 kwahiyo mtaona kwamna waliojitokeza kwa ajili ya kuwania nafasi mbalimbali ni 43,461. Haya ni mafanikio makubwa sana kwa chama chetu.

“Walioomba vijana ni wengi, waliomba wafanyakazi, waliomba wakulima, wafugaji, wavuvi wakina mama wakina baba, wasomi, walemavu viongozi wa NG’Os, na hii inadhihirisha kwamba CCM ni chama kinachopendwa sana, hakuna chama kingine ambacho wamejitokeza watu zaidi ya 43,461. Inawezekana tumevunja rekodi hata katika Afrika kwamba CCM ni chama kinachopendwa.

“Haya ni matokeo mazuri ya kusimamia ilani katika kipindi cha miaka mitano, nimewaona wajumbe  mkitembelea miradi mbalimbali na imeweza kukamilika, huu ni ushahidi wajumbe wa NEC mmetimiza wajibu wenu. Na ndio maana mtaona watu wengi wamejitokeza kuomba nafasi mbalimbali,” alisema Rais Magufuli.

ULINZI WA HALI YA JUU

Jana katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM (White House), kulikuwa na ulinzi wa hali ya juu. Askari walikuwa wengi huku magari ya polisi yakiwa yametapakaa  jirani na ofisi hizo na baadhi ya askari wakiwa juu ya paa za nyumba za jirani na ofisi hiyo kuimarisha ulinzi.

Pia barabara zilifungwa na wote waliokuwa wakiingia katika jengo la Makao Makuu ya CCM walinyang’anywa simu walizokuwa nazo, hata wa-NEC nao hawakuruhusiwa kuingia na simu.

KATIBU MKUU 

Awali kabla ya kumkaribisha Rais Magufuli, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally alisema kikao hicho hakitafanya  uteuzi wa wawakilishi kutoka visiwani Zanzibar na badala yake kitafanya uteuzi kwa nafasi za ubunge na ubunge wa viti maalumu kutokana na ratiba ya Tume ya Taifa ya  Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kupishana katika hatua ya uteuzi.

Alisema wajumbe waliohudhuria kikao cha jana ni 113 kati ya 167 na kwamba wajumbe 54 hawakuweza kuhudhuria kutokana na kugombea nafasi mbalimbali.

“Lakini wajumbe 54 hawawezi kuhudhuria kwa sababu za kikanuni, kwani wamegombea nafasi mbalimbali ikiwemo za ubunge ambapo wamegombea watu 42 na uwakilishi watu 12.

“Kwahiyo wajumbe wenzetu 54 hawawezi kushiriki katika uteuzi kwa sababu kanuni yetu inatutaka ukishagombea katika hatua ya uteuzi wa nafasi unayogombea huwezi pia ukawa sehemu ya wajumbe wa kufanya uteuzi,” alisema Bashiru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
191,647FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles