JPM ateua wenyeviti wa bodi nne

0
709

Mwandishi wetu -Dodoma

RAIS Dk. John Magufuli amefanya uteuzi wa wenyeviti wa bodi nne, Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) na Mkuu wa Chuo cha Maji.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi jana, ilieleza kuwa uteuzi wa viongozi hao umeanza Januari juzi.

Balozi Kijazi alisema Rais Magufuli amemteua Profesa Maurice Mbago kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), ambaye kwa sasa anashika wadhifa huo kwa kipindi cha pili.

Alisema Rais Magufuli pia amemteua Dk. Masatu Chiguna kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), akichukua nafasi ya Profesa Ninatubu Lema ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na bodi kuvunjwa.

“Rais Magufuli pia amemteua Profesa Zacharia Mganilwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT),” alisema Balozi Kijazi.

Aliongeza kuwa katika uteuzi huo uliofanyika jana, Rais Magufuli amemteua Mariam Nkumbi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mkonge Tanzania.

Balozi Kijazi alisema Rais Magufuli pia amemteua Dk. Godwill Wanga kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC).

Kabla ya uteuzi huo, Wanga alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

“Aidha, Rais Magufuli amemteua Dk. Adam Karia kuwa Mkuu wa Chuo cha Maji,” alisema Balozi Kijazi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here