30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Takukuru yajitosa rushwa ya ngono Saut

Benjamin masese – Mwanza

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza, imebaini kuwapo vitendo vya rushwa ya ngono Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut).

Hatua hiyo inafuatia baada ya kufanyika uchunguzi kuhusu malalamiko ya uwepo wa vitendo vya rushwa ya ngono baina ya wahadhiri na wanafunzi wa chuo hicho.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Stenga, alipokuwa akijibu maswali mbalimbali ya waandishi wa habari kuhusu agizo la Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William ole Nasha aliyeagiza taasisi hiyo pamoja na katibu mkuu wa wizara hiyo kuunda tume kuchunguza malalamiko ya rushwa ya ngono katika chuo hicho.

Kamanda huyo wa Takukuru alisema vitendo hivyo vinajitokeza kutokana na ukosefu wa maadili na makosa ya kinidhamu na tayari uongozi wa Saut umechukua hatua kwa lengo la kudhibiti na kukomesha hali hiyo.

Alisema baada ya uchunguzi huo, walibaini vitendo hivyo vinajitokeza kutokana na baadhi ya wahadhiri kutozingatia maadili ya kiutumishi na kwamba tayari uongozi wa Saut umekwishachukua hatua na kujiwekea mikakati ya kuhakikisha havijitokezi tena.

“Ni kweli naibu waziri wa elimu aliagiza kuundwa tume na kufanyika uchunguzi, jambo lile lilifanyiwa kazi tangu mwaka jana, na kikubwa tulichobaini ni makosa ya kinidhamu kwa wahadhiri pale Saut ndiyo yanasababisha kuwapo na vitendo vya rushwa ya ngono dhidi ya wanafunzi.

“Ukiangalia taarifa yetu ya miezi mitatu ya Oktoba hadi Desemba 2019, tumeweza kupokea jumla ya malalamiko 195 na kati ya hayo 25 ni idara ya elimu, hivyo tunaendelea kupambana na vitendo hivyo kila siku ili kuhakikisha wanafunzi wanapata haki yao bila kubughudhiwa,” alisema Stenga.

Mwishoni mwa mwaka jana, Shirikisho la Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso) lilimwomba Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, kufika chuoni hapo kunusuru unyanyasaji unaofanywa na wahadhiri dhidi ya wanafunzi hao na kusababisha kutofanya vizuri wakati wa mtihani.

Ole Nasha alifika chuoni hapo mwaka jana kwa niaba ya Profesa Ndalichako na kuzungumza na uongozi wa Saut chini ya Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Costa Mahalu na baadaye kufanya kikao na wanafunzi peke yao ambao walimweleza mambo mengi na kuagiza kuundwa tume ya uchunguzi.

Katika kikao hicho, Ole Nasha alibaini baadhi ya mapungufu katika chuo hicho, ikiwa ni ukosefu wa mifumo sahihi inayotumika, baadhi ya wahadhiri kutokuwa waaminifu kwa kuchukua rushwa kutoka kwa wanafunzi, ukosefu wa bima ya afya licha ya wanafunzi kulipa, ubadhirifu wa mikopo na chuo kushindwa kutoa msaada pale mwanafunzi anapokuwa na tatizo.

RUSHWA USAJILI WA LAINI

Kuhusu rushwa katika usajili wa laini kwa alama za vidole unaoendelea, Stenga alisema ipo lakini inakuwa ni vigumu kujulikana kutokana na wananchi kushawishika kuitoa kwa maofisa wa Wakala wa Vitambulisho vya Taifa (Nida) na wachache wasio waaminifu hupokea.

Stenga alisema licha ya Takukuru kuendelea kuweka mitego yake katika maeneo unapofanyika usajili wa laini, lakini wananchi wamekuwa wakishindwa kutoa ushirikiano pale wanapoona vitendo vya rushwa vikitendeka.

“Yaani rushwa ambayo inawanufaisha wananchi wenyewe hawatoi ushirikiano, lakini ile ambayo inamnufaisha mtumishi wanatoa ushirikiano, sasa katika zoezi la usajili wa laini asilimia kubwa ya wananchi ndio wanashawishi kutoa rushwa.

“Mtu anaona kufuata taratibu anachelewa ukizingatia kuna foleni, kwa hiyo wanaanza kuzunguka mlango wa nyuma na kutaka kutoa fedha ili awahishiwe kupata namba.

“Pengine wanatafuta nje ya eneo la kazi wanapeana, sasa sisi kama Takukuru ni vigumu kuwapata, lakini tunawaomba wananchi wakatae,” alisema Stenga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles