25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ataka watu kujivunia miradi ya kimkakati

 WAANDISHI WETU -SENGEREMA

MGOMBEA urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amewataka Watanzania kujivunia kuwapo kwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa kwa fedha za ndani, ikiwemo ujenzi wa Daraja la Kigongo – Busisi linalogharimu Sh bilioni 700.

Alisema daraja hilo la kilomita 3.2 ndilo refu kuliko madaraja yote Afrika Mashariki na kwamba litakuwa la mfano kwa kuubadilisha mji wa Sengerema.

Akizungumza jana katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Mnadani Sengerema, Dk. Magufuli alisema maisha yake alianzia kufundisha Shule ya Sekondari Sengerema hivyo anaifahamu vizuri.

“Bilioni 700/- si kidogo, hakuna mtu aliyetegemea tangu tupate uhuru tutatengeneza daraja hilo, ndiyo maana ninawaomba tena kura. Mradi kama huo wa mabilioni mkimleta mtu mwingine anaweza akatoa yale machuma akaenda kuuza ‘sekrepa’.

“Wana Sengerema mimi ni mtoto wenu, Chadema watapita, Cuf watapita, ACT watapita, NCCR Mageuzi watapita, CCM watapita… kwanini mninyime kura,” alisema Dk. Magufuli.

MAFANIKIO SENGEREMA

Dk. Magufuli alisema katika wilaya hiyo kuna miradi mbalimbali yenye thamani ya Sh bilioni 27.2 inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya Nyamazugo, Busisi, Nyakasugwa, Nyakalilo, Kasungamile na Nyaunge.

Katika sekta ya elimu, alisema madarasa 167 yamejengwa, Shule ya Sekondari Sengerema imekarabatiwa kwa Sh bilioni 1.30, vyuo vya maendeleo ya wananchi vimekarabatiwa kwa Sh bilioni 1.18 pamoja na kujenga miundombinu ya shule maalumu.

Dk. Magufuli alisema pia hospitali mbili za wilaya zimejengwa Sengerema na Buchosa kwa Sh bilioni 3.8 pamoja na vituo vya afya katika maeneo ya Kagunga, Kamanga, Katunguru, Nyamkowe na Nyakalilo.

“Tunahakikisha afya za Watanzania zinaimarika kwa sababu maisha yanaendana na afya ndiyo maana tunaomba mtuamini,” alisema Dk. Magufuli.

Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, mafanikio mengine ni ujenzi wa gati la Mtama na MV Mwanza.

Aidha alisema Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) iliwakopesha wakulima matrekta tisa huku akiwatahadharisha kutokuwa na tamaa ya kuuza mazao yao.

“Wakati wa changamoto ya corona watu wote waliofungiwa hawakwenda shambani, wana njaa na nchi inayotegemewa ni Tanzania kwa sababu sisi hatukujifungia.

“Kwahiyo niwaombe sana wana Sengerema na Watanzania kwa ujumla tumepata mazao mengi tusije kuwa na tamaa ya kuyauza haraka haraka tutapata njaa, na tukiuza tusiuze kwa bei ya chini, tutunze vyakula ili baadaye tusije tukapata njaa,” alisema Dk. Magufuli.

Pia aliahidi kutatua changamoto mbalimbali za jimbo hilo, ikiwemo Barabara ya Sengerema – Katunguru – Kamanga Feri kilomita 34.93 kwa kiwango cha lami pamoja na vijiji vilivyosalia kupatiwa umeme.

“Katika maisha yangu nilipoanza kazi nilianzia Sengerema, nilifundisha Sengerema Sekondari miaka ya 1982, 1983 na 1984, kwahiyo maisha ya Sengerema ninayafahamu. Hospitali tuliyokuwa tunategemea ni ya Misheni, ukikosa pale lazima uende Mwanza.

“Hata ombi analolitoa mbunge wenu mtarajiwa (barabara na halmashauri ya mji) nimelibeba, nitaomba siku atakapochaguliwa anikumbushe,” alisema Dk. Magufuli.

Changamoto nyingine ni uanzishwaji wa Baraza la Ardhi, kufufua viwanda vya pamba na kukamilisha maboma 109 ya shule za msingi Sengerema.

LUGOLA, TIZEBA

Akiwa katika eneo la Bukokwa Jimbo la Buchosa, Dk. Magufuli alisema katika mchakato wa kumpata mgombea ubunge wa jimbo hilo, Dk. Charles Tizeba (aliyemaliza muda wake) na Erick Shigongo (anayegombea) walifungana kwa kura hatua iliyosababisha suala hilo kupelekwa kwa viongozi wa juu wa chama kwa uamuzi zaidi.

Aliwaomba wananchi wa jimbo hilo kumchagua Shigongo awe mbunge wao, huku akiahidi kuwa Dk. Tizeba atatafutiwa kazi nyingine kwani nafasi zipo nyingi.

Naye Dk. Tizeba aliwaomba wananchi kumchagua Shigongo kwani yeye aliongoza kwa miaka 10, hivyo sasa ni zamu ya mtu mwingine.

Kwa upande wake, Shigongo aliahidi kuwatumikia wana Buchosa na kuwaomba wamchague Dk. Magufuli, yeye mwenyewe na madiwani.

OMBI LA MSIKITI

Akizungumza katika mkutano huo, Sheikh wa Wilaya ya Sengerema, Hamad Jaha, alimwomba Dk. Magufuli baada ya kuapishwa awajengee msikiti wenye hadhi kwani uliopo haukidhi mahitaji ya waumimi waliopo eneo hilo.

MGOMBEA UBUNGE SENGEREMA

Mgombea ubunge Jimbo la Sengerema, Hamis Tabasamu, alimwomba Dk. Magufuli kuipandisha hadhi wilaya hiyo ili iwe halmashauri ya mji.

“Tuna mambo mengi mazuri yamefanywa na Serikali, tunakupongeza kwa maamuzi sahihi ya kutujengea daraja.

“Sengerema ina miaka 45 toka imeanzishwa, ilikuwa haijawahi kupata hospitali ya wilaya, GN (Tangazo la Serikali) ya mwaka 1990 ilieleza kuwa Sengerema itakuwa ‘township’, wenzetu wote wameshapata halmashauri za mji, ukitupa halmashauri ya mji utakuwa umemaliza matatizo ya wananchi wa Sengerema,” alisema Tabasamu.

Mgombea huyo pia alimwomba Dk. Magufuli kuwasaidia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami angalau kilomita 15 huku akiahidi kuwa taa za barabarani zitakuwa ndani ya uwezo wake.

“Hapa Sengerema zaidi ya watu 142,000 wamejiandikisha, hakikisho hatutapoteza madiwani, wala hatutapoteza mbunge na wala hatutapoteza kura yako,” alisema Tabasamu.

HABARI HII IMEANDIKWA NA NORA DAMIAN, CLARA MATIMO Na SHEILA KATIKULA

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles