25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

JPM amtumbua Katibu Mkuu Wizara ya Fedha

Dk. Servacius Likwelile
Dk. Servacius Likwelile

Na Mwandishi Wetu – DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amemteua Doto James kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Kabla ya uteuzi huo, James alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango (Sera). Ataapishwa leo Ikulu, Dar es Salaam.

Kutokana na uteuzi huo, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk. Servacius Likwelile atapangiwa kazi nyingine.

Likwelile anakuwa Katibu Mkuu wa kwanza kuondolewa katika nafasi yake, akitanguliwa na wakuu wa mikoa wanne pamoja na mkuu wa wilaya mmoja ambaye aliishia kusikiliza kikao na kutumbuliwa kimyakimya.

Wakuu wa mikoa waliotumbuliwa ni Anne Kilango, aliyekuwa Mkoa wa Shinyanga, Magesa Mulongo (Mara), Felix Ntibenda (Arusha) na Said Mwambungu wa Ruvuma ambaye naye alirudishwa Ofisi ya Waziri Mkuu akisubiri kupangiwa majukumu mengine.

Uamuzi wa jana unatanguliwa na ziara ya Machi 10, mwaka huu ambayo Rais Magufuli alitangaza kusitisha utoaji wa Sh bilioni 925 kwa ajili ya kulipa malimbikizo ya madeni ya Serikali ambazo tayari zilikwishaidhinishwa na Wizara ya Fedha na Mipango.

Mbali na hilo, Rais Magufuli aliagiza Kitengo cha Madeni ya Nje ambacho awali kilikuwa chini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na baadaye kupelekwa wizarani, kirejeshwe mara moja ili kuimarisha udhibiti wa ukopaji na ulipaji wa madeni.

MSIGWA ATHIBITISHWA

Wakati huo huo, Rais Magufuli amemthibitisha Gerson Msigwa kuwa Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Ikulu, Peter Ilomo, ilieleza kuwa Msigwa amethibitishwa kuanzia jana kushika wadhifa huo.

Kabla ya uthibitisho huo, Msigwa alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Rais, katika Ofisi ya Rais Ikulu tangu Novemba 17, mwaka jana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles