Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Rais John Magufuli, ameonyesha kukerwa na ucheleweshaji wa kesi mahakamani kwa kisingizio cha upelelezi unaendelea.
Aidha, amewataka wapelelezi kuhakikisha wanafanya upelelezi mapema ili wananchi wenye kesi watendewe haki.
“Matatizo ya ucheleweshaji kesi, na kutotolewa kwa hukumu kwa wakati bado yapo, mwaka jana niliambiwa mahakama ilifuta kesi 1,986 kwa ajili ya ucheleweshaji, hii ni changamoto.
“Na kwa ndugu zangu wapelelezi kapelelezeni haraka, unakiona kitu kipo unakwenda kupeleleza nini.
“Unamuona mtu anaiba na kidhibiti anacho, unakwenda kupeleleza nini kwamba wakati anaiba alikuwa amelala au amekaa, unakwenda unamwambia hakimu upelelezi unaendelea,” amesema Rais Magufuli wakati akiwahutubia wanasheria katika kilele cha Wiki ya Sheria leo Februari 6, jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine, amesema ucheleweshaji huo wa kesi unazalisha malalamiko kwa wananchi kuwa mahakimu na majaji wanachelewesha kesi kumbe aliyechelewesha ni mpelelezi.
“Na ninyi wanasheria mnakutana usiku mnapanga kesi itakavyokwenda na mnaacha wakili wa kujitegemea ashinde dhamira zenu ziwasute, tuzingatie maadili ya kazi zetu.
“Mnachelewesha na ndiyo maana kesi zaidi ya 1,000 zimefutwa mahakamani kwa ajili ya ucheleweshaji na ushahidi uko wazi,” amesema.