23.9 C
Dar es Salaam
Monday, September 20, 2021

JPM ajipanga upya

Mwamdishi Wetu -Dodoma

JOTO la uchaguzi wa rais kwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) linazidi kupanda, huku Rais Dk. John Magufuli akionekana kujipanga upya kwa kuchukua fomu ya kuomba uteuzi ili kupeperusha bendera ya chama hicho.

Rais Magufuli ambaye anaomba uteuzi huo ili kukamilisha kipindi cha pili cha kuongoza nchi, alichukua fomu jana makao makuu ya CCM jengo la White House, Dodoma.

Katika hali ya kushangaza, Rais Magufuli alipowasili katika ofisi za CCM hakuwa na msafara mkubwa wa magari mengi kama ilivyozoeleka na badala yake alitumia gari moja lililokuwa na namba binafsi za usajili huku akiwa na walinzi wachache.

Baada ya kufika katika jingo hilo, aliingia moja kwa moja ofisini na kwenda kwenye ukumbi maalumu ambako alikabidhiwa fomu na Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, ambaye alimpa maelekezo ya kufuata ikiwamo fomu maalumu za kutafuta wadhamini kama utaratibu wa chama hicho tawala unavyoelekeza.

Katika ukumbi huo, Dk. Bashiru alikuwa pamoja na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Rodrick Mpogolo na Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Uchumi na Fedha Dk. Frank Haule.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu hizo na kulipia ada ya Sh milioni moja, Rais Magufuli aliishukuru CCM kwa kumpa fomu hizo na amewaomba wana CCM na Watanzania wote wamuombee katika safari yake ya kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro cha kugombea kiti cha urais.

“Ninawaomba wana CCM wanidhamini na washiriki katika mchakato wa uchaguzi kwa amani, utulivu na mshikamano,” alisema Rais Magufuli.

Baada ya kukabidhiwa fomu hizo, Rais Magufuli alianza safari ya kutafuta wadhamini na alikwenda Ofisi ya CCM Mkoa wa Dodoma na kumkabidhi fomu ya wadhamini 250 Katibu wa Mkoa, Jamila Yusuph.

Pia alikutana na wanachama wachache wa CCM waliokuwa katika Ofisi ya Makao Makuu na mkoa ambao aliwatakia heri katika mchakato wa uchaguzi unaoendelea na amewataka kuendelea kukiimarisha chama.

HALI YA ZANZIBAR

Kwa upande wa Zanzibar, hekaheka zimeendelea kushika kasi na hadi sasa tayari wanachama watano wamejitokeza kuomba uteuzi wa CCM ili kuwania urais wa visiwa hivyo.

Makada hao kila mmoja ameonekana kuwa na hamu ya kuteuliwa kwa lengo la kutaka  kumrithi Rais anayemaliza muda wake Dk. Ali Mohammed Shein.

Waliochukua fomu jana mjini Unguja ni pamoja na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk.  Hussein Mwinyi, ambaye amejitosa kwenye kinyang’anyiro  hicho kwa kujitokeza kimyakimya katika ofisi za CCM,  Kisiwandui na kuchukua fomu.

Dk. Mwinyi anaungana na makada wengine wanne ambao hadi jana walikuwa wamekwisha kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba.

Kinyang’anyiro cha urais visiwani hapa kimeshika kasi ikiwa ni mkakati wa kutafuta mrithi wa Rais Dk. Ali Mohammed Shein anayehitimisha kipindi chake cha utawala wa miaka 10.

DK. MWINYI

Dk. Mwinyi ambaye hakutaka kuzungumza na vyombo vya habari mara baada ya kuchukua fomu hizo saa 7:30 mchana mbali tu ya kupigwa picha, ni miongoni mwa Wazanzibari ambao wamekuwa wakitajwa na kupewa nafasi kubwa ya kupitishwa na vikao vya uchujaji vya CCM katika uteuzi wa mgombea wa kiti hicho ambacho tangu mwaka 1995 kimekuwa na ushindani mkubwa kutokana na nguvu kubwa ya upinzani visiwani hapa.

Akiwa ni mtoto wa Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, aliingia rasmi katika siasa za ushidani mwaka 1995 alipogombea ubunge Jimbo la Mkuranga mkoani Pwani kisha kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Afya katika Serikali iliyoundwa na Rais Benjamin Mkapa.

Tangu wakati huo, sura ya Dk. Mwinyi haijawahi kutoonekana kwenye Baraza la Mawaziri.

Amehudumu katika Serikali tatu za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – Serikali ya awamu ya tatu ya Rais Mkapa, Serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete na sasa Serikali ya Rais Magufuli.

Kwa sasa ndiye waziri mwandamizi kuliko wengine wote katika Baraza la Mawaziri.

Itakumbukwa kwamba mwaka 1995 Dk. Mwinyi alikuwa kwenye kundi la vijana walioibuliwa na Rais Mkapa na kupewa nafasi za unaibu waziri akiwa pamoja na Rais Magufuli na waziri wa sasa wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Pia walikuwako Kilontsi Mporogomyi na Abdisalaam Issa Khatibu ambao sasa wamepotea katika siasa za ushindani.

Dk. Mwinyi amehudumu katika Wizara ya Afya, Ofisi ya Makamu wa Rais akishughulikia Muungano na sasa Wizara ya Ulinzi na amekuwa  mzingatiaji mkubwa wa maadili ya umma kwani wakati wa utawala wa awamu ya nne wakati mawaziri wengi wakikumbwa na kimbunga kama cha Tokomeza na vingine, yeye alipita bila kuwa na doa lolote.

Katika uchukuaji wa fomu, Dk. Mwinyi hakufuatana na wapambe, aliwasili ofisi za CCM Kisiwandui akiwa ndani ya gari yenye namba za kiraia.

Baada ya kuchukua fomu, alisema haikuwa siku yake ya kuzungumza na waandishi wa habari kwa kuwa ndiyo kwanza amechukua fomu na sharti la kwanza akazisome na kujua zinahitaji nini cha kufanya na kwamba baada ya hapo atapata wasaa wa kuzungumza nao.

Hata hivyo, alikishukuru chama chake kwa kuruhusu demokrasia ndani ya mfumo wa kutafuta viongozi wake na ni kwa maana hiyo ametumia fursa hiyo kujitosa ulingoni.

Mfumo huo wa uchukuaji fomu unafanana na ule aliotumia Rais Magufuli mwaka 2015, kwani hakutaka kuzungumza chochote na waandishi wa habari baada ya kupewa fomu mbali tu ya kuwaomba radhi, kwamba hakuwa amefika katika ofisi hizo kuzungumza na waandishi wa habari bali kuchukua fomu.

WENGINE WALIOJITOSA

Wengine waliochukua fomu ni pamoja na kijana Mbwana Yahya Mwinyi, ambaye alisema kuwa hafanyi utani, ana dhamira ya kweli na uwezo anao na yeyote anaweza kuwa rais kama akiteuliwa na chama chake.

Mwingine aliyejitosa na kuchukua fomu ya kuwania urais wa Zanzibar ni Omar Sheha Mussa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mussa alisema aliwahi kushika nafasi mbalimbali serikalini katika awamu zilizopita.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
156,961FollowersFollow
518,000SubscribersSubscribe

Latest Articles