24.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 17, 2021

Jinsi Wizara ya Maji ilivyowatua ndoo kichwani wanamke

Na Jumbe Ismailly, MANYONI 

DHANA ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, kupitia Wizara ya Maji ni kumtua mwanamke ndoo kichwani, kwa kuhakikisha anapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yake.

Katika kuhakikisha dhana hiyo inafanikiwa kama ilivyopangwa, wizara imeanzisha miradi ya maji lukuki kwa kuchimba visima virefu na vifupi katika maeneo mbalimbali nchini.

Miradi hiyo ya maji imekuwa ikisimamiwa na wahandisi waliopo kwenye mikoa ambayo wakandarasi wanaendelea na ujenzi wa miundombinu ya miradi hiyo ya visima kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa kiwango kinachotakiwa kulingana na thamani ya fedha zilizotumika.

Ili kuhakikisha fedha zilizotolewa na serikali zimetumika kulingana na shughuli zilizofanyika katika miradi hiyo, ndipo Mei 22, mwaka huu, Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, alifanya ziara ya siku moja katika Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida, kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya maji wilayani humo.

Wakati wa ziara hiyo, Aweso alitembelea na kukagua mradi wa maji wa Kintinku – Lusilile, uliopo Kijiji cha Lusilile kabla ya kuzungumza na uongozi wa wilaya pamoja na wataalamu wa maji ngazi ya mkoa na wilaya.

Baada ya kutembelea na kukagua mradi huo, Aweso pamoja na kuridhishwa na utekelezaji wake, lakini alionekana kukerwa na kutokuwapo kwa mkandarasi wa mradi na badala yake alikuwapo msaidizi wake.

Licha ya kukosekana kwa mkandarasi huyo, ilibainika kwamba mradi huo unasuasua kutokana na serikali kutomlipa mkandarasi na hivyo kusababisha shughuli za ujenzi wa mradi kusimama.

Hata hivyo, changamoto hiyo ya ukosefu wa fedha unaochangia kutokamilika kwa mradi huo kwa asilimia 100, ilitatuliwa na naibu waziri huyo baada ya kuwasiliana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo na kuahidiwa kupatiwa fedha mwezi huu.

Katika makala hii, Aweso anazungumzia tabia iliyojengeka kwa baadhi ya wahandisi wa  maji wanapotembelewa na viongozi wao wakuu wanatoa taarifa zinazoonyesha mafanikio peke yake na kuficha changamoto zilizopo.

Aweso anasema kuwa ametumwa na Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, kufika kwenye mradi wa maji wa Kintinku – Lusilile kuona hali ya upatikanaji maji.

“Amenituma, kaniambia hebu ufike pale uone hali ya utekelezaji wa mradi wa maji ili tujue ni namna gani sasa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaweza ikatekelezeka na wananchi wanapata huduma ya maji kwa hiyo, ni watu wenye bahati, nina imani mambo yataenda vizuri,” anafafanua Aweso.

Anasema jambo kubwa alilokuwa anataka kutoka kwa mhandisi wa maji ni amsaidie kwamba anapokuja kiongozi katika wizara ya maji au hata kiongozi yeyote yule, pamoja na taarifa inayotolewa haina budi kuonyesha na changamoto zilizopo katika mradi husika.

Anaweka bayana kuwa mhandisi anapoonyesha na changamoto ambazo anafikiri utakuwa ni msaada kwani anaweza akasema mambo ni safi lakini kumbe kuna jambo ambalo likifanywa na mamlaka husika wanaweza kuwasaidia wananchi.

Anasema mradi wa Kintinku – Lusilile ni mkubwa, ni wa kujivunia na ambao zaidi ya watu 55,000 wanaweza wakapata huduma ya maji safi na salama.

“Mkandarasi yuko wapi, anatakiwa awe wapi? Sitaki tuanze siku nzuri tu, mimi nilitegemea hapa kuwe kuna kazi zinazoendelea, kazi zinazofanyika si ndiyo…mbona hakuna kazi yoyote ile inayofanyika, wewe si ndiyo msimamizi, shughuli zipi ndogo ndogo zinazofanyika?” anahoji Aweso.

Anasema yeye siyo mtoto mdogo kwani anapofika kwenye eneo la mradi anaona kabisa kama kuna shughuli zozote zinazofanyika au zinazoendelea hapa hakuna, hivyo alimwagiza mhandisi kuhakikisha anamsimamia ili kazi ndogo ndogo ziiishe kwani wananchi wanahitaji maji yatoke bombani.

“Hakuna kitu kingine zaidi ya maji bombani, hakuna kitu kingine na uzuri mmeshafanyakazi kubwa, mnaweza mkasema hizi kazi ndogo ndogo zikatumia muda mrefu, mradi haukamiliki badala ya kuwa na wema na manufaa makubwa kwa wananchi, mwishowe ikajenga chuki,” anasisitiza.

Hata hivyo, Aweso akataka kujua kinachokwamisha mradi wa Kintinku – Lusilile kukamilika kwani hadi sasa umeshakamilika kwa asilimia 90, na kuhoji kama mkandarasi wa mradi anadai na ndipo Mhandisi wa Ruwasa Manyoni, alipokiri kwamba serikali inadaiwa zaidi ya Sh milioni 370 na madai hayo yameshapelekwa wizarani.

Akizungumza na viongozi wa chama na serikali, Aweso licha ya kuwapongeza kwa kujituma, anasema kuna baadhi ya maeneo utakuta watu wamedorora kwa kisingizio cha ugonjwa wa corona, lakini wao pamoja na corona wameendelea kuchukua tahadhari lakini wanaunga mkono pia kauli ya Rais Magufuli ya Hapa Kazi Tu.

Anasema kutokana na dhamira hiyo iliyoonyeshwa na watendaji wa Wilaya ya Manyoni, hivyo akaahidi kuwa wao kama wasaidizi wa Rais hawatakuwa kikwazo cha miradi ya maji na baada ya kuona kazi kubwa iliyofanyika Kintinku, lakini wanatambua ugonjwa wa corona usiwe sababu kwa wakandarasi kutelekeza miradi ya maji.

“Mtusaidie wenzetu wa habari kwamba wakandarasi wote ambao wametelekeza miradi kwa visingizio vya ugonjwa wa corona, warudi ‘site’ kwa sababu moja ya silaha ya kupambana na ugonjwa huu ni maji.

“…na sisi wizara lazima tuhakikishe upatikanaji wa maji, ipo miradi iliyotekelezwa kwa asilimia 90 na mingine asilimia 80; wawepo ‘site’ ili waweze kuikamilisha, nasi viongozi wa wizara tutaisimamia na kuifuatilia, yeyote atakayekiuka haya tunayozungumza tutaachana naye,” anasisitiza huku akiwakodolea macho watendaji wa wizara hiyo.

Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa Mji wa Manyoni wakizungumzia suala la upatikanaji wa maji safi na salama katika Mji wa Manyoni, waliipongeza mamlaka ya kwa kuwawezesha kupata maji kwa kiwango kizuri, ikilinganishwa na ilivyokuwa huko nyuma kabla ya kuanzishwa kwa mamlaka hiyo.

Mmoja wa wakazi hao, Bahati Matonya, anasema maji yanapatikana na utaratibu wa ugawaji wa maji hayo umekuwa mzuri, kwani kwa walio na mabomba majumbani baada ya kutumia maji hulipia gharama za matumizi hayo kwa njia ya simu na kupitia benki.

“Kwa kweli shida ya maji mjini Manyoni,kwa kweli nakataa ila sijui kwa kweli mimi kwangu nimevuta bomba sijui watu wengine lakini maji ni mengi maana nimekuwa nikiwaona watu wanazunguka na ndoo, lakini maji yapo,” anasisitiza mkazi huyo.

Hata hivyo, anasema pamoja na maji kutoka nyumbani kwake na maeneo ya jirani na kwake, lakini hajui kama kwenye maeneo ya Mtaa wa Majengo na Mwembeni iwapo yanatoka kama inavyotakiwa.

Naye mkazi wa Mtaa wa Mjini Kati, anasema Mji wa Manyoni, hauna shida ya maji, ambapo mkazi wa Mtaa wa Samaria,  Halima Rashidi, anapingana na kauli hiyo, akisema haina ukweli kwasababu bado kuna maeneo yenye shida ya upatikanaji wa maji safi na salama katika Mji wa Manyoni.

Halima hata hivyo, anasisitiza kwamba kuna baadhi ya maeneo kama vile Mtaa wa Kipondoda, Tambukareli, Chang’ombe, Samaria, Mguruwang’ombe na Majengo wakazi wake wamekuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma ya maji.

Anasisitiza kwamba pamoja na maeneo yote ya mitaa hiyo kusambazwa mabomba ya maji, lakini cha kushangaza huwa hayatoi maji, hadi kusababisha mabomba  kuweka kutu hivyo endapo maji yataanza kutoka kuna hatari kwa wananchi wake kupatwa na magonjwa.

Akitoa taarifa fupi ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira, Meneja wa mamlaka hiyo Manyoni, Marycella Hagila, anasema eneo lake linakadiriwa kuwa na wakazi wapatao 32,814 na idadi ya wanaopata maji safi na salama ni wastani wa watu 19,616 wakiwamo watumiaji wa majumbani, taasisi, wafanyabiashara, viwanda na kwenye vituo vya kuuza maji sawa na asilimia 59.8.

Akizungumzia hali ya upatikanaji wa maji, vyanzo na matanki, meneja huyo anafafanua kuwa mahitaji ya maji kwa wananchi wa Manyoni ni lita 2,246,160 kwa siku na kwamba hata hivyo, mamlaka ina uwezo wa kuzalisha lita 1,205,000 kwa siku.

Anasema huduma ya maji katika Mji wa Manyoni inaongezeka pamoja na kuwapo changamoto mbalimbali kwenye vyanzo vya maji na ongezeko la kila siku la watu katika mji huo.

Anautaja mradi wa maji uliopo katika Mji wa Manyoni kuwa ni mradi ni wa kusukuma maji kwa mashine wakati kuna vyanzo tisa vya maji vinavyohudumia wakazi wa Manyoni.

Kwa mujibu wa meneja huyo, visima sita vina uwezo wa kuzalisha lita 60,000 kwa saa wakati visima vitatu vina uwezo wa kuzalisha lita 29,000 kwa saa na hivyo kuvifanya visima hivyo kuwa na uwezo wa kuzalisha lita 89,000.

Kuhusu uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji, Hagila anafafanua kuwa mamlaka inahusika na shughuli za utoaji wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira katika maeneo ya Mamlaka ya Mji mdogo wa Manyoni.

“Mamlaka hii ipo kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Maji Na.5 ya mwaka 1997 sehemu ya 3(3) kama ilivyofanyiwa mabadiliko katika Sheria ya maji na usafi wa mazingira Na12 ya mwaka 2009 sehemu ya 60,”anafafanua meneja huyo.

Anaweka bayana kuwa mamlaka hiyo ipo katika kundi C ambapo inatakiwa kujitegemea katika shughuli za uendeshaji na matengenezo isipokuwa mishahara ya watumishi wake na uwekezaji wa miradi mipya.

Kwa upande wa utekelezaji wa miradi ya maji, anabainisha kwamba huduma ya maji mjini Manyoni kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 hadi mwaka wa fedha wa 2018/2019, halmashauri kupitia Programu ya Maendeleo ya sekta ya maji ilipanga kutekeleza miradi ya maji mjini yenye thamani ya Sh 1,130,601,800.

Anabainisha matarajio baada ya utekelezaji wa miradi yote kukamilika kuwa kupitia kukamilika kwa utekelezaji wa mradi huo, itaongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wanaoishi mjini kutoka asilimia 59 iliyopo sasa hadi kufikia asilimia 63.3 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Kuhusu changamoto, Hagila anazitaja kuwa ni pamoja na uchakavu wa miundombinu iliyopo, hususani kwenye maeneo ya usambazaji wa bomba kuu linalopeleka maji kwenye matanki ya kusambazia maji.

Changamoto zingine kwa mujibu wa meneja huyo ni uchache wa watumishi wa mamlaka katika utekelezaji wa kazi mbalimbali za ofisi kwani kwa sasa kuna watumishi saba tu pamoja na uchache wa vyanzo vya maji na uwezo mdogo wa matanki ya kuhifadhia maji.

Anaaitaja mikakati waliyojiwekea ili kuondokana na changamoto hizo kuwa ni ofisi ya mamlaka kuendelea kuboresha baadhi ya miundombinu chakavu katika maeneo ya usambazaji na bomba kuu na wameomba wizarani watumishi wakapatiwa wawili bado wanaendelea kusisitiza kuongezewa wengine.

Mikakati mingine ni kuweka bajeti ili waweze kuajiri watumishi kwa kutumia mapato ya ndani pamoja na kibali cha uchimbaji wa visima sita ambavyo wamepewa kwenye vibali maalumu kitasaidia kuongeza vyanzo vya maji.

“Pia kuna mpango mkakati wa mradi mkubwa wa Serikali ya India kutoka wizarani utasaidia kuongeza vyanzo vya maji pamoja na miundombinu,” anabainisha.

Naye Meneja wa Ruwasa Manyoni, Mhandisi Gabriel Ngongi, anasema mradi wa maji Kintinku –Lusilile ni mkubwa ambao utahudumia takribani wakazi 55,485 wanaoishi katika vijiji 11 pindi utakapokamilika (idadi ya watu ni kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012).

Anafafanua kwamba mradi huo unategemea kugharimu takribani Sh 10,171,877,293.05 bila kodi ya ongezeko la thamani hadi kukamilika kwake (kwa mujibu wa taarifa za usanifu wa mradi).

Aidha, Mhandisi Ngongi anasema mradi huu umepangwa kutekelezwa katika awamu nne kutokana na bajeti inayopangiwa kila mwaka wa fedha ambapo kwa awamu hii ya kwanza,Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni iliingia mkataba Na.LGA/117/2017/2018/W/01-PKG-VIII na Mkandarasi M/S CMG Constraction Company Ltd S.L.P.235,Mwanza kwa gharama ya shilingi 2,460,437,146.90 bila kodi ya ongezeko la thamani.

Kwa mujibu wa mhandisi huyo, utekelezaji wa mkataba huo wa awamu ya kwanza unategemea kukamilika Agosti 31, mwaka huu mara baada ya kukamilika kwa awamu hii ya kwanza, utekelezaji katika awamu zilizobaki utaanza mara moja kwa ajili ya kusambaza maji kwenye vijiji husika.

“Lengo la mradi ni kutoa huduma ya maji safi, salama na ya kutosha kwa wananchi wapatao 55,385 wanaoishi katika vijiji 11 vilivyopo pembezoni mwa barabara kuu itokayo Singida kwenda Dodoma. 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

12,054FansLike
2,941FollowersFollow
18,400SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Latest Articles