24.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 27, 2021

JPM atafakari kufungua vyuo

Mwandishi Wetu -Dar es salaam

RAIS Dk. John Magufuli, amesema kuwa endapo hali ya ugonjwa wa corona itaendelea kama ilivyo sasa, Serikali inafikiria kufungua vyuo ili wanafunzi warudi vyuoni kuendelea na masomo na pia michezo itaruhusiwa kuendelea kufanyika nchini.

Kauli hiyo aliitoa jana wilayani Chato mkoani Geita, katika ibada ya Jumapili iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Chato iliyoongozwa na Mchungaji Thomas Kangeizi.

Rais Magufuli ambaye aliambatana na mkewe Janeth, waliwashukuru waumini wa KKKT Usharika wa Chato kwa kumkaribisha kusali ibada ya Jumapili pamoja nao, na pia amemshukuru Askofu Mkuu wa KKKT, Dk. Fredrick Shoo na Askofu wa Jimbo la Kusini C (Biharamulo) Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Askofu Abednego Keshomshahara kwa kuwaruhusu waumini kuendelea na ibada huku wakichukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona.

Pamoja na hali hiyo mkuu huyo wa nchi, aliwashukuru viongozi wote wa dini nchini ambao wamemtanguliza Mwenyezi Mungu na kuwaongoza waumini kumuomba Mungu aepushe janga la ugonjwa wa corona na pia kwa kumuombea na kumtia moyo katika kipindi hiki kigumu ambapo dunia inapita katika janga la ugonjwa huo.

UFUNGAJI MIPAKA

Rais Magufuli alisema kuwa hakutoa amri ya kuwafungia ndani wananchi (lockdown) wala kufunga mipaka kwa sababu ingeleta madhara makubwa katika shughuli za uzalishaji mali, utekelezaji wa miradi, ajira za watu na pia upatikanaji wa mahitaji muhimu ikiwemo chakula hali ambayo ingesababisha madhara makubwa zaidi.

“Ninamuamini Mungu aliyehai na ndiyo maana niliamua nimemtanguliza Mungu katika kukabiliana na ugonjwa wa corona kwa maombi ya siku tatu hivyo ni vema viongozi wa dini na Watanzania wote kwa ujumla mtumie tena siku tatu za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili ijayo kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa hivi sasa maambukizi ya ugonjwa corona yameanza kupungua,” alisema Rais Magufuli.

WAGONJWA WAPUNGUA

Hata hivyo alitoa takwimu za mpaka kufikia jana ambapo alisema kuwa kuwa Hospitali ya Amana iliyopo jijini Dar es Salaam iliyokuwa na wagonjwa 198 imebakiwa na wagonjwa 12, Hospitali ya Mloganzila iliyokuwa na wagonjwa 30 imebakiwa na wagonjwa 6, Kituo cha Lulanzi (Kibaha) kulikuwa na wagonjwa zaidi ya 50 wamebaki 22, Agha Khan wamebaki wagonjwa 31.

“Hindu Mandal 16, Regency wamebaki 17, TMJ 7, Rabinisia 14, Moshono (Arusha) 11, Longido 0, Karatu 0, Buswelu 2, Misungwi 2, Ukerewe 0, Magu 0, Mkuyuni 0, Nyahunge 0, Sengerema 0, Kwimba 0, Bugando na Sekou Toure 2, Dodoma 2 (kutoka zaidi ya 40), Kongwa 0, Kondoa 0 nakadhalika. Na kwamba wagonjwa wengi wana hali nzuri.

“Mimi namwamini Mungu na Mungu amejibu maombi yetu, tumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutusikiliza na tuendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu wa corona,” alisisitiza  Rais Magufuli.

Kutokana na takwimu hizo zilizotolewa na Rais Magufuli ni kwamba wagonjwa waliopo nchini ni 144 toka 480 waliotangazwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Aprili 29, mwaka huu.

Hata hivyo Mkoa wa Dar es Salaam ukiongoza kwa kuwa na wagonjwa wa corona 125, Mwanza 6, Arusha 11, na Dodoma 2.

Aprili 29, mwaka huu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alitangaza idadi ya wagonjwa nchini na kufikia 480.

WATALII NCHINI

Rais Magufuli, alibainisha kwamba kuna idadi kubwa ya watalii wanaotaka kuja hapa nchini na ambao tayari wameonyesha nia ya kukata tiketi za kuja, hivyo ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na mamlaka zingine zinazohusika kutowazuia watalii na ndege zinazotaka kuleta wageni hapa nchini.

Aliwataka viongozi na Watanzania wote kutokuwa na hofu kubwa dhidi ya ugonjwa wa corona kiasi cha kusababisha matatizo mengine ikiwemo kutowahudumia ipasavyo wagonjwa mbalimbali ambao baadhi wanaambiwa wana corona ilihali hawajaambukizwa ugonjwa huo, ama kuwazuia watoa huduma wakiwemo madaktari na wauguzi wanaoshukiwa kuwa wameambukizwa corona.

“Wapo watu ambao wanaambiwa wana corona lakini wakipimwa tena wanakutwa hawana,” alisema 

Mkuu huyo wa nchi, wamewataka viongozi waache kuwazuia watu kuzika kwa heshima marehemu wao kama ambavyo wanawazika watu waliokufa kwa magonjwa mengine yakiwemo ukimwi, kifua kikuu na surua.

MTOTO WAKE NA CORONA

“Hata mimi mtoto wangu alipata Corona lakini amepona, alikuwa anakula limau, tangawizi, anajifukiza mpaka amepona, kwa hiyo ugonjwa huu utasambaa na utakwisha, hatuwezi kufunga mipaka, sisi Tanzania tukifunga mipaka nchi zinazotuzunguka watapata shida, hata sasa tulipata tatizo la upungufu wa sukari, nimezungumza na Rais wa Uganda Mheshimiwa Museveni na zimekuja tani 26,000 kwa meli hadi Mwanza, na tani nyingine 10,000 zimekuja kupitia bandari ya Dar es Salaam, tungefunga mipaka ingekuwaje?,” alisema na kuhoji  Rais Magufuli

Alisisitiza kuwa Watanzania waendelee kuchapa kazi hasa kuzalisha chakula kwa wingi kwa kuwa majirani ambao wamefunga mipaka na wamewafungia watu wao (lockdown), pindi watakapofungua watahitaji chakula na watakuja Tanzania.

“Tutumie mvua hizi za mwisho zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwetu, kuzalisha mazao yanayokomaa haraka ili baadaye wenzetu watakapofunguliwa tuwauzie chakula, endeleeni kuchapa kazi,” alisema 

TUME YA UCHUNGUZI MAABARA

Akizungumza kuhusu uchunguzi uliofanyika katika Maabara ya Taifa, Rais Magufuli alisema tume iliyoundwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu imefanya kazi nzuri na matokeo ya uchunguzi wake yatatangazwa na waziri mwenyewe.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,310FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles