JOSHUA KUMKABILI TAKAM LEO

0
667

CARDIF, Wales

BONDIA wa uzito wa juu duniani,  Anthony Joshua, leo anatarajia kupanda tena ulingoni kuzichapa na Mcameroon, Carlos  Takam, kugombea  mkanda wa IBF katika ulingo wa Principality  uliopo jijini Cardif nchini Wales.

Joshua anapewa nafasi kubwa ya kushinda katika pambano hilo lakini atatakiwa kuwa makini na mpinzani wake ambaye anaaminika kuwa bora na imara katika mchezo huo.

Awali kila shabiki wa mchezo huo alitarajia pambano la marudio kati ya Joshua na Wladimir Klitchko Aprili 29, mwaka huu lakini baada ya raia huyo wa Ukraine kutangaza kustaafu mchezo huo ukafutwa, baada ya hatua hiyo, Joshua alitakiwa kupambana na Kubrat Pulev, iwapo alitaka kutetea mkanda wake.

Ni mchezo ambao wengi walitabiri ungekuwa mkali kutokana na uimara na ubora wa mpinzani wa Joshua ambaye alidaiwa kufanana kimbinu na Klitchko.

Lakini kabla ya wiki mbili ya mchezo huo, Joshua alibadilishiwa bondia wa kupambana naye badala yake alitakiwa kuzichapa na Mcameroon, Takam, baada ya mpinzani wake kuumia bega.

Hata hivyo, Takam alisisitiza kwamba, anaweza kumsambaratisha mpinzani wake na kutengeneza jina lake katika uzito wa juu duniani.

Promota wa mchezo huo, Eddie Hearn, alieleza kwamba, litakuwa pambano lenye msisimko mkubwa kutokana na Takam kutojulikana na watu wengi katika mchezo huo ukilinganisha na Joshua.

Takam anafahamika zaidi Cameroon na Ufaransa na limekuwa jambo la ghafla kuwa mbadala na mpinzani wakati Joshua atakapojaribu kutetea mikanda yake minne ya WBA na ABF.

Mcameroon huyo ambaye amepoteza michezo mitatu kati ya mapambano 39 aliyowahi kupambana, anatarajiwa kupata sapoti ya mtoto wake au mkewe atakapokuwa akizichapa leo: “Najaribu kuyafanya maisha yangu kuwa siri, lakini rafiki zangu wengi wanatarajia kuja  kushuhudia pambano hili wakitokea nchini Ufaransa.

“Watu wengi kutoka Cameroon wamenieleza wanahitaji kuja kushuhudia pambano hili, hiyo ndiyo nchi yangu, kuna wakati napenda kwenda kutembelea familia yangu.”

Takam ambaye anaishi Jiji la Paris,  ana uraia wa nchi ya Ufaransa, aliamua kuishi kwenye jiji hilo baada ya michuano ya Athens Olympics kumalizika.

“Mimi nafahamika kwa ubora  zaidi nikiwa Ufaransa na Cameroon, lakini baada ya mzunguko wa tatu au wa nne katika pambano la leo, natarajia watu 80 ndani ya ukumbi huo watanifahamu mimi ni nani.

“Waingereza wanataka kufahamu kitu baada ya kukiona, wako sawa katika hilo, nikipata nafasi ya kumdondosha Anthony, maisha yangu kwenye ngumi yatabadilika. Katika soka Cameroon tukicheza dhidi ya Nigeria ni zaidi ya mchezo maana unakuwa na upinzani mkubwa, lakini sasa tuna pambano la ngumi ambalo ni kubwa ndani ya ulingo,” alisema Takam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here