24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 28, 2023

Contact us: [email protected]

JOAQUIN GUZMAN: Bwana unga anayezawadia wafanyakazi wake magari ya kifahari

JOSEPH HIZA NA MTANDAO

NDIYE mfanyabiashara mkubwa na namba moja wa dawa za kulevya duniani kwa wingi wa shehena anazouza hadi utajiri katika miaka ya karibuni.

Bwana unga huyu Joaquin ‘El Chapo’ Guzman kwa sasa yuko mahakamani akikabiliwa na mashitaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya nchini Marekani, huku msaidizi wake wa zamani wa karibu akitoa ushahidi wa ‘kumgandamiza’.

El Chapo jina la utani linalomaanisha ‘mtu mfupi’, ambaye pia anajulikana kama Osama bin Laden wa Mexico, alikuwa gumzo duniani jana baada ya kutoroka jela kwa mara ya pili.

Mhimili huyo wa dawa za kulevya duniani alitoroka kutoka jela lenye ulinzi mkali la Altiplano maili 50 kutoka mji mkuu wa Mexico, Mexico City kabla ya kukamatwa na kisha kupelekwa Marekani.

Ujasiri wake wa kutoroka ulimshuhudia akipitia katika mfumo mrefu wa njia iliyochongwa ardhini hadi katika selo yake gerezani ambao ulimwongoza hadi katika jengo moja linaloendelea kujengwa zaidi ya maili moja kutoka jela hilo, kisha kutokomea.

Sababu ya kushitakiwa nchini humo ni za kiusalama pamoja na ukweli kuwa aliiathiri zaidi jamii ya Marekani kwa kusafirisha humo dawa hizo haramu.

Kwa mfano, asilimia 80 ya dawa haramu za kulevya katika jiji la tatu kwa ukubwa nchini Marekani-Chicago imetoka genge la Guzman, Sinaloa kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya upelelezi jijini humo.

Guzman ni sababu ya watoto wengi kupigana kavu kavu, visu au kurushiana risasi na hivyo kuharibika kitabia katika umri wao mdogo.

Sehemu kubwa ya machafuko yanayotokana na silaha moto katika jiji hilo (asilimia 80) yametokana na mihadarati ya Sinaloa, eneo la Mexico ambako El Chapo’ alizaliwa katika familia masikini ya kijijini.

El Chapo alipanda ngazi ya umaarufu kutokea eneo hilo na kuja kuongoza mtandao mkubwa kabisa kwa sasa wa wafanyabiashara haramu, wauzaji, wauaji, ununuzi wa wanasiasa na polisi ili kufanikisha malengo yake.

Guzman amemwumiza kila mtu katika jiji hilo, watumiaji wa jiji na vitongoji vyake, wapita njia wasio na hatia na watoto wadogo wanaojikuta katika magenge ya kihuni ya mitaani.

Guzman aliajiri watu mahiri wenye kila aina ya ubunifu uliofanikisha biashara pasipo kukamatwa na hivyo kusaidia genge lake kutengeneza mabilioni ya dola kwa kumimina tani ya shehena za mihadarati kama vile heroin, methamphetamine, cocaine na bangi katika majiji mbalimbali ya Marekani.

Guzman alikuwa tajiri mno kiasi kwamba alikuwa na bustani yake binafsi ya wanyama, ambako paka wakubwa wakali walitamba.

Tajiri mno, kiasi kwamba alinunua nyumba ya ufukweni kwa dola milioni 10 na tajiri mno kiasi kuwa alikuwa akisafiri kwenda Uswisi kwa ajili ya tiba ya kumwepusha na uzee.

Yote hayo ni baadhi ya yaliyofahamika Jumanne wiki hii wakati wa usikilizaji wa kesi dhidi yake nchini Marekani.

Ni wakati mwanagenge wa zamani aliyegeuka shahidi wa serikali, Miguel Angel Martinez alipokuwa akiieleza mahakama kuwa kushamiri kwa cocaine mapema miaka ya 1990 kulichochea matumizi ya kufa mtu ya Guzman, watoto wake na watu wake.

Alikuwa na nyumba katika kila fukwe. Alikuwa na ranchi kwa kila jimbo la Mexico. Na alizawadia wafanyakazi wake magari ya kifahari, alisema Martinez, rafiki wa zamani wa karibu na msaidizi mwandamizi wa El Chapo.

Martinez alilieleza namna genge la Sinaloa lilivyovusha kimagendo tani za cocaine kuingia Marekani kupitia njia za ardhini mpakani kwa kutumia magari ya muundo ya maroli ya kusafirishia mafuta, ambayo yalikuwa na vyumba vya siri.

“Wafanyakazi walijikuta wakiathirika na unga kwa vile kila unapobonyeza kilo, itapeperusha cocaine hewani,’ Martinez aliiambia mahakama.

Kilichofuata baada ya hatua hiyo ni ujio wa makumi kwa mamilioni ya dola taslimu, alisema.

Sehemu kubwa ya fedha hizo iliishia Tijuana, ambako Guzman alituma ndege zake tatu binafsi kila mwezi kwenda kuyabeba, Martinez alisema. Kwa wastani kila ndege ilibeba zaidi ya dola milioni 10.

Genge hilo lilitumia nyumba maalumu kufikisha sehemu kubwa ya fedha hizo, Martinez alisema.

Mabegi yaliyotuna fedha za Kimarekani yalipelekwa katika mabenki ya Mexico, ambako wafanyakazi walihongwa ili kuzibadili kwa pesos za Mexico, hakuna maswali yaliyoulizwa hapo, alisema.

Guzman pia alitumia ndege zake kuzunguka Mexico nzima akiwa na walinzi wenye silaha nzito kutembelea nyumba zake zote, ikiwamo nyumba ya ufukweni mwa Acapulco yenye bustani ya wanyama na treni ndogo ya kuizunguka bustani hiyo kuangalia simba, tigers na chui weusi, alisema. Kulikuwa na boti ya kifahari ifahamikayo ‘Chapito,’ alisema .

Miongoni mwa matanuzi yake ghali ni wanawake wanne hadi watano warembo katika maisha ya Guzman, Martinez alisema huku mkewe wa mshitakiwa huyo akisikiliza. “Ilitubidi tuwalipe wote,”alisema.

Kikaja kipindi ambacho bwana unga huyo, ambaye alizaliwa katika umasikini akaibua tabia ya kupenda kusafiri duniani.

Msafara wake ulitembelea visiwa vya Macau kucheza kamali na Uswisi ambako alifanyiwa tiba ya kumfanya aonekane kijana,’alisema.

Hata hivyo, nyakati nzuri za raha ziliharibiwa na vita baina ya magenge hasimu, ambayo ilikuwa moto mno kiasi cha kutuma timu ya wadunguaji kwenye uwanja wa wa Guadalajara kujaribu kummaliza Guzman, Martinez alisema.

Badala yake mpango huo ukaenda kumuua Kardinali wa Kanisa la Roman Katoliki na kuufanya umma wa Mexico kupiga kelele na kusababisha msako mkubwa dhidi ya Guzman.

Baada ya msako wa miaka kadhaa, hatimaye Guzman akakamatwa kabla ya kuendesha mpango wowote wa kujificha kule El Salvador, alisema.

Guzman aliletwa Marekani mwaka jana kutoka Mexico, ambako alitoroka mara mbili kutoka jela zenye ulinzi mkali.

Amekana mashitaka ya kusafirisha dawa za kulevya, ambayo wanasheria wake wanadai ametolewa kafara.

Katika harakati zake za kibiashara, Guzman alitambua kuwa angetumia fursa ya wingi wa magari barabaraani baina ya Mexico na Magharibi ya Kati.

Mihadarati hufichwa ndani ya malori makubwa na magari mengine yanayopita kila siku na kila saa.

Kwa mfano anapotuma magari 10 kuvuka mpaka, hata kama wapelelezi watabaini na kukamata, watakuwa na tatizo na lori moja au mawili tu na kuruhusu mengine manane.

Katika kuwafanya maofisa wawe na shughuli nyingi za kuchosha na kuwapoteza umakini wao au maboya kama wasemavyo vijana wa mitaani, hutumika magari, malori hadi watu walio katika pikipiki.

Lakini pia Guzman alihitaji maofisa waandamizi mjini Chicago na kwingineko, ambao walihakikisha shehena zake zinawafikia salama wawakala wakubwa, ambao walizisambaza kwa wauzaji wadogo, waliozifikisha kwa watumiaji mitaani au watumiaji katika vitongoji tajiri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,224FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles