23.8 C
Dar es Salaam
Sunday, May 12, 2024

Contact us: [email protected]

JK: Tunataka Tanga School iwe kinara wa ufaulu

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete amesema wamedhamiria kuboresha kiwango cha elimu na mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika Shule ya Sekondari Tanga ili iwe miongoni mwa shule bora kitaifa.

Shule hiyo ya kwanza kuanzishwa wakati wa utawala wa Wajerumani ilijengwa mwaka 1895 ina historia ya kutoa watu muhimu ambao wameshika nyadhifa mbalimbali akiwemo Rais Kikwete ambaye alisoma kati ya mwaka 1970 – 1971.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Tanga, MacMaster Luzilo, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Umoja wa Wanafunzi waliosoma Tanga School (TSAA).

Akizungumza Oktoba 29,2023 wakati wa uzinduzi wa Umoja wa Wanafunzi waliosoma Tanga School (TSAA), Kikwete amesema shabaha yao kubwa ni kuendeleza shule hiyo na kuinua ubora wa elimu.

“Tunaamini sisi ambao tumebahatika kupata elimu pale tunao mchango kwa ajili ya maendeleo ya shule yetu, hatuna uwezo mkubwa lakini kuna ambacho tunaweza kuchangia.

“Focus yetu kubwa tunataka Tanga School iingie kwenye hesabu ya shule bora zenye ufaulu wa hali ya juu, kama wenzetu wanatajwa na sisi tunaweza kutajwa…haiwezekani shule ya kwanza nchini lakini imepotea kabisa watu hawaijui,” amesema Kikwete.

Mkuu wa Shule hiyo, MacMaster Luzilo, amesema wameweka mikakati ya kuhakikisha shule hiyo inaingia kumi bora kitaifa.

Amesema shule hiyo kwa sasa ina wanafunzi 1,126 wakiwemo 163 wenye mahitaji maalumu.

Hata hivyo amesema inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa walimu wa ufundi, sayansi, hisabati na elimu maalumu.

“Karakana zimechoka na zingine zilibadilishwa matumizi, pia nyumba za walimu zimechakaa na tuna upungufu wa kompyuta,” amesema Mwalimu Luzilo.

Mwenyekiti wa TSAA, Meja Jenerali Mstaafu Hamisi Semfuko, amesema umoja huo unalenga kuiangalia shule hiyo kwa jicho la pekee.

“Mafanikio ya jambo hili ni zawadi kubwa kwa kizazi kijacho na taifa letu na sio kwa Tanga School pekee. Dhamira yetu ya kwenda kuanzisha maktaba ya kimtandao inalenga kuboresha kiwango cha ufaulu na ni chachu ya mageuzi makubwa ya maboresho ya miundombinu kulingana na kasi ya teknolojia ya sasa,” amesema Meja Jenerali Semfuko.

Amesema maktaba hiyo itawaondolea wazazi gharama ya kutafuta vitabu na kupanua wigo wa wanafunzi kupata taarifa mbalimbali za kitaaluma.

Katibu wa umoja huo Godwin Mbaga, amesema wanatarajia kuwaunganisha watu wote waliosoma Tanga School kuanzia miaka ya 1960 mpaka 2022 kwa lengo la kuieneza historia ya elimu ya sekondari nchini kupitia shule hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles