27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, December 7, 2023

Contact us: [email protected]

JK avionya vyombo vya habari

kikweteNA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM
RAIS Jakaya Kikwete amesema serikali haitavumilia vyombo vya habari visivyosimamia uadilifu, weledi pamoja na kutumika katika kuchochea ghasia.
Kikwete, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa studio za Azam TV, zilizopo Barabara ya Mandela, Dar es Salaam, aliyasema hayo jana, katika hotuba yake ya ufunguzi rasmi wa kituo hicho kikubwa cha televisheni Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Alisema wakati mwingine ukitafuta kusifiwa kwenye uongozi haufanyi jambo la maana, hivyo katika kusimamia maadili ni lazima ufanye uamuzi mgumu.
“Serikali itaendelea kusimamia maadili ili kuhakikisha sekta ya habari inakuwa katika mwelekeo sahihi,” alisema Rais Kikwete.

Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja wakati ambako serikali imekuwa katika mtanziko mkubwa na wadau wa habari kutokana na uamuzi wake wa kuvifungia baadhi ya vyombo vya habari.
Tayari serikali yake ambayo inalalamikiwa kwa kukumbatia sheria mbovu ya Magazeti ya mwaka 1978, imelifungia gazeti la Mwanahalisi tangu mwaka 2012 kwa muda usiojulikana, huku mwaka 2013 ikiwahi kulifungia gazeti la Mtanzania kwa miezi mitatu na Mwananchi wiki mbili, kwa kile ilichodai kuwa yaliandika habari za uchochezi na uhasama.
Zaidi ya hilo, Rais Kikwete pia aligusia suala la maslahi kwa watumishi wa vyombo vya habari, akisema kuwa iwapo wamiliki watawathamini, ikiwa ni pamoja na kushughulikia suala la mafunzo juu ya uadilifu na maadili, hali hiyo itapunguza kutumiwa na watu wa nje, ambao kimsingi wamekuwa wakisababisha kuporomoka ubora, lakini pia kuchochea ghasia.
Rais Kikwete alisema tangu mwaka 1992 Serikali imejitahidi kusimamia sheria na uadilifu wa vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na kutoa wigo kwa vyombo hivyo kuongezeka kutoka viwili hadi kufikia kuwa na redio 95, machapisho 895 na TV 28.
“Atakayesema kama nchi yetu hakuna uhuru wa vyombo vya habari huyo atakuwa hajatutendea haki, japokuwa wakati mwingine tunawajibika kuchukua hatua katika kulinda maadili, hivyo tumeweka na tutaendelea kuweka mazingira mazuri katika sekta hiyo,” alisema.
Alisema uzinduzi huo wa Studio za Azam TV utaiweka Tanzania katika eneo zuri la matumizi ya dijitali na kuifanya kuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara kuwa na Studio za TV yenye ubora wa kisasa.
Rais Kikwete pia alivitaka vyombo vya habari kuweka utaifa mbele kwa kulinda sera na maslahi ya taifa.
“Msijifanye wa kimataifa halafu mkasahau taifa lenu, kwa mfano hata siku moja Marekani huwezi kuona watu wanaandamana au habari mbaya yoyote ikirushwa BBC au CNN, wao habari mbaya zipo Afrika, kwa kuwa wana sera ya kulinda maslahi ya nchi yao,” alisema.
Mbali na hilo, Rais Kikwete alisifu Kampuni zinazomilikiwa na Alhaji Said Salim Bakhresa kwa ulipaji mzuri wa kodi.
“Kama kungekuwa na kampuni kama hii 20 zenye kuthamini ulipaji wa kodi, nchi yetu ingepiga hatua,” alisema Kikwete.

Katika uzinduzi huo ambao pia ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Waziri wa Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni, Fenella Mukangara, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, na Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, kwa upande wake Mmiliki wa Kampuni hiyo (SSR), Alhaji Said Salim Bakhresa, alisema uwekezaji huo wa studio umegharimu shilingi bilioni 56 na kuifanya kuwa pekee kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kuhusu studio hiyo, ina sehemu nne, ikiwamo ile iliyopewa jina la Studio namba moja, yenye sehemu nne ambazo ni ile ya kurushia matangazo, nyingine kwa ajili ya michezo, chumba cha uchambuzi na kile ambacho ni mahususi kwa habari.
Pia studio namba mbili itatumika kuzalishia vipindi na kufanyia midahalo mbalimbali yenye kukusanya zaidi ya watu 150.

Vyumba vyote vimeundwa kwa mfumo wa kimataifa wa kutumia dijitali wenye kuonekana kwa usahihi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles