24.8 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Janeth Magufuli akabidhi misaada kwa wahitaji

MWANDISHI WETU – DODOMA

JANETH Magufuli ambaye ni mke wa Rais Dk. John Magufuli, ametoa wito kwa taasisi mbalimbali, mashirika, wafanyabiashara na watu wenye mapenzi mema kujitolea kusaidia watu wenye uhitaji maalumu kwani kwa kufanya hivyo ni kutimiza amri kuu ya upendo ya Mwenyezi Mungu isemayo pendaneni kama mimi nilivyowapenda ninyi.

Mke huyo wa rais aliyasema hayo jana wakati akitoa misaada mbalimbali kwa vituo vya kulelea watoto wenye mahitaji maalumu vya Cheshire Home na Nyumba ya Matumaini katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu Chamwino jijini Dodoma.

Alikabidhi misaada hiyo kwa wawakilishi wachache wa watoto hao walioongozana na baadhi ya walezi wao, ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa agizo la Serikali la kuepuka mikusanyiko ya watu isiyo lazima kutokana na janga la ugonjwa wa mafua makali ya corona.

Janeth alisema hivi sasa ni kipindi cha Kwarezma ambayo ni kumbukumbu ya mateso ya Yesu Kristo, na kwamba kwa mujibu wa Isaya 58:7 waumini wanahimizwa kufunga, kuomba na pia kujitoa kwa wenzao wenye mahitaji mbalimbali.

“Kwa kuzingatia hilo nami leo (jana) nimewaita hapa ili kutoa kazawadi kangu kadogo kwa wanangu hawa”, alisema Janeth.

Misaada aliyotoa ni pamoja na mchele tani mbili, unga wa sembe tani mbili, maharage kilo 830, mafuta ya kupika lita 830, sukari, vinywaji, biskuti, sabuni za kufulia na kuogea, mafuta ya kupaka, mashuka, nguo, viatu pamoja na vyandarua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles